Baraka za Kujitegemea
Biashara Inashamiri
Shukrani kwa kile alichojifunza katika madarasa ya kujitegemea, wakati mlango mmoja ulipofunga kwa Teddy Reyes, mwingine punde ulifunguka.
Ni saa 10:00 alfajiri huko Santo Domingo, Jamhuri ya Dominika, na Teddy Reyes tayari amekwisha amka na anafanya kazi. Ana mengi ya kufanya leo kuendeleza biashara yake inayoshamiri. Anaanza kukatakata nyanya na mikate. Kisha anatengeneza mchuzi wake maalumu.
Ifikapo saa 12:00 asubuhi, wafanyakazi wawili wanafika kumsaidia, na matayarisho yanashika kasi. Ifikapo saa 2:00 asubuhi, tayari wamekwisha tengeneza mikate 300, ikifungwa kila mmoja kwenye kifungashio cha plastiki na kupangwa kwenye mabegi. Wafanyakazi wengine sita hutokea, na kundi lote linatoka kwenda kuuza.
Ifikapo saa 3:00 asubuhi, mikate yote isipokuwa michache—mitatu au minne ambayo Teddy alitunza kuwalisha timu yake—imekwisha uzwa.
Biashara ni nzuri kwa Teddy. Lakini mambo daima yamekuwa si rahisi. Kwa kweli, kwa miaka mitano iliyopita, hakuweza kupata kazi imara katika taaluma yake aliyochagua—kama mwanasheria.
Hivyo ni kwa jinsi gani Teddy alifanya badiliko kutoka kwenye kushauri wateja kwenda kwenye kuuza mikate? Ilichukua juhudi kubwa, ndiyo, lakini pia ilichukua matumizi makini ya kanuni alizojifunza darasani zilizotolewa kupitia mafunzo ya Kanisa ya Huduma ya Kujitegemea.
Kupoteza Kazi Yake
Miaka mitano iliyopita, maisha kwa Teddy yalionekana ya kupendeza. Alikuwa na kazi nzuri kama mwanasheria, alikuwa ameoa karibuni, na alikuwa amembatiza mke wake. “Lakini tulipata baadhi ya changamoto,” alisema, “na nikapoteza kazi yangu.”
Kwa miaka minne iliyofuata Teddy alihangaika kutafuta kazi. “Kulikuwa na kazi nyingi ambazo ningeweza kufanya, lakini hakuna aliyetaka kunilipa. Nilijaribu kuanzisha ajira tofauti tofauti mimi mwenyewe, lakini hilo halikufanikiwa.”
Mke wake, [Stephany], alikuwa na kazi nzuri, lakini mshahara wake pekee usingeweza kulipa gharama zote. Punde wanandoa walipata mtoto. Walifurahia, lakini kipato chao kilizidi kubana. Walipoteza nyumba yao, ilibidi wauze gari yao, na walitumia akiba yao yote. Hatimaye ilibidi wahamie kwenye nyumba ndogo iliyomilikiwa na mama ya [Stephany].
Lakini Teddy hakukata tamaa. Punde fursa isiyotarajiwa ilijitokeza.
Nguvu ya Kujitegemea
Baada ya miaka ya mahangaiko, Teddy alijua ulikuwa ni muda wa mabadiliko.
“Niliamua kuchukua kozi ya Kanisa ya kujitegemea,” anasema. “Nilisikia kuhusu kozi hizo lakini mara zote nilidhani hazikuwa kwa ajili yangu. Nilidhani zilikuwa tu kuhusu kufanya mambo peke yako. Madarasa yalikuwa ya kuvutia.”
Kwanza, Teddy alijiunga na kundi la Kusimamia Fedha Binafsi. Kisha akajiunga na kundi la Kuanzisha na Kukuza Biashara Yangu. Makundi ya madarasa yalimsaidia Teddy kwenye uelewa wa biashara yake lakini pia yalimsaidia kujijenga kiroho.
“Kuchukua madarasa haya kulibadili kila kitu,” anasema. “Niliamua kufanya kila kitu walichofundisha. Na kipato changu kilibadilika mara moja. Nilianza kulipa zaka kamili, kusali kila siku, kusoma maandiko, na kuonyesha imani. Na mambo yalibadilika—nilianza kuweka akiba ya pesa na kuitakasa sabato. Kila kanuni ilinibariki.”
Katika kundi hili la Kuanzisha na Kukuza Biashara Yangu, Teddy alijifunza jinsi ya kuainisha bidhaa zenye kuwezekana ambazo zingeweza kuwanufaisha wateja pale wanapoishi. Alipotathmini kile ambacho watu walikuwa wakihitaji, mwongozo ulianza kutiririka. Katika eneo lake, watu walipenda mikate iliyotengenezwa siku hiyo hiyo, lakini pia walipenda kuipata kwa kuagiza—na kupelekewa.
“Hoteli nyingi zina mchuzi maalumu ambao hufanya chakula chao kupendwa,” Teddy anasema. “Hivyo nilitengeneza mchuzi wangu mwenyewe maalumu kwa ajili ya mikate!”
Kukuza Biashara Yake
Siku alipofungua biashara yake, Teddy alitengeneza mikate 30.
“Dakika thelathini baadaye, nilikuwa nimekwisha rudi nyumbani,” anasema. “Mke wangu alisikitika aliponikuta kwenye kochi. Aliniuliza nilikuwa nafanya nini nyumbani muda ule—sikupaswa kuwa nauza mikate? Nilikuwa tayari nimeuza yote!”
Wiki chache baadaye, Teddy aliwasiliana na shule na wafanya biashara wa eneo lake. Wengi walitamani kununua mikate yake, na biashara yake ikaanza kukua. Alijifunza haraka jinsi ya kutunza mboga mbichi ili zikae kwa muda mrefu. Anajua pia muda kamili wa mchuzi wake maalumu kutumika. Anaagiza na kuchukua mikate kila asubuhi. Ananunua mboga zenye punguzo la bei Jumamosi, ambazo zina gharama ndogo lakini bado zitakuwa nzuri jumatatu.
Punde alikuwa akipokea mahitaji kwa ajili ya aina maalumu za mikate, na hata idadi kubwa kwa ajili ya matukio maalumu. Alihitaji msaada na alianza kuajiri watu.
Kwa kutengeneza mahusiano chanya na shule na wafanya biashara wa eneo lake, Teddy alianzisha uteja hai, na wenye muendelezo. Ndani ya miezi minne, alikuwa na wafanyakazi nane na alikuwa akiuza mikate 300 kwa siku, siku tano kwa wiki. Timu yake ya mauzo ilikuwa na ufanisi kiasi kwamba waliuza kila mkate hata wakati wa majira ya jua ambapo shule zilikuwa zimefungwa. Sasa Teddy yuko tayari kupanuka tena.
Kwa sababu alihudhuria madarasa ya kujitegemea, alipata mwongozo wa kuja na wazo la biashara ya mikate. “Kwa sababu ya mwongozo huu kutoka Kanisani na baraka nilizopokea,” anasema, “nina ushuhuda imara wa Kanisa la Yesu Kristo.”