Siyo Hata Tufani Ingeweza Kutuzuia
Koraima Santiago de Jesus
San Juan, Puerto Rico
Muda mfupi baada ya kurudi kutoka kwenye misheni yangu, nilipokea mwaliko wa kwenda kwenye dansi. Kwenye dansi, nilisahau nilipoweka simu yangu na mvulana alijitolea kunisaidia kuitafuta. Tulipokuwa tukizungumza, tuligundua wote tulikuwa wamisionari waliorudi na tulishiriki mawazo mengi na malengo.
Uhusiano wetu uliendelea kukua, na tukachumbiana. Ilikuwa ndoto yetu kuunganishwa katika Hekalu la Washington D.C. Kabla halijafungwa kwa ajili ya ukarabati mnamo Machi 2018. Lakini baada ya kufanya uamuzi huo, tulijaribiwa. Kwanza, nilipoteza kazi yangu na sikuwa na njia ya kuweka akiba pesa kwa ajili ya safari yetu ya hekaluni. Pili, tufani ilikuwa njiani kupiga Puerto Rico kabla ya siku yetu ya harusi.
Wakati Tufani Maria ilipopiga, iliharibu kisiwa chetu cha kupendeza. Maduka yalifungwa. Hatukuwa na umeme; maji, chakula, na vitu vingine vya muhimu vilikuwa vigumu kupatikana. Tulipoteza kila kitu tulichokuwa tumeandaa kwa ajili ya tafrija yetu. Ilibidi tuahirishe tafrija, na ilionekana kama ingetubidi kuahirisha harusi yetu pia. Kusafiri nje na ndani ya Puerto Rico kulizuiliwa, na hakuna aliyejua ingekua kwa muda gani. Nilianza kuhisi kuvunjika moyo, na nilijawa na mashaka na kuchanganyikiwa.
Usiku mmoja, mimi na mchumba wangu tulizungumzia hali yetu. Kusafiri hakukuwa kwa uhakika, na tusingekuwa na tafrija au mavazi ya harusi, lakini Roho alithibitisha kuwa tulihitaji kumwamini Bwana. Jambo la muhimu zaidi lilikuwa ni kuunganishwa hekaluni. Tuliomba kwa Baba wa Mbinguni kwa ajili ya usaidizi.
Pale usafiri wa kutoka nje ya Puerto Rico uliporejea, tulitakiwa kufanya upya mipango ya safari na kupanga upya tarehe ya kuunganishwa kwetu. Hatukuwa na mawasiliano kwa wiki kadhaa baada ya tufani, lakini simu ya rafiki ilifanya kazi. Alitupatia tuitumie kuwasiliana na watu wa hekaluni. Tuliweza kupanga upya kila kitu hii tuweze kuunganishwa! Wiki chache kabla ya safari yetu, wanafamilia walijitolea viatu na nguo na kutusaidia kupata vitu vingi kwa ajili ya harusi yetu.
Pale hatimaye tulipoingia hekaluni, tuliacha mashaka yetu yote nyuma. Tulishikana mikono kuingia kwenye wakati wetu ujao pamoja. Ninaweza kwa kweli kusema nilihisi mkono wa Bwana ukituongoza na kutuhakikishia kwamba kadiri tulivyomuamini Yeye, kila kitu kingekuwa SAWA. Leo, tumebarikiwa kuwa na mtoto mzuri wa kiume na sisi ni familia iliyounganishwa milele.