2019
Uaminifu wa Kupendeza
Aprili 2019


Uaminifu wa Kupendeza

Mwandishi anaishi huko Colorado, Marekani.

“Fanya lile lililo jema” (2 Wakorintho 13:7).

Sweet Honesty

“Nataka umwangalie mdogo wako,” Mama alisema. “Mimi na baba yako tunakwenda kumsaidia mgonjwa.”

Nilitazama juu nikisimama kufagia sakafu ya nyumba yetu ndogo na kutikisa kichwa kwa kukubali. Mama alikuwa rais wa Muungano wa Usaidizi wa Akina Mama, na mara nyingi alikwenda kuwatembelea akina dada katika kata yetu.

“Asante, Arlyn,” Mama alisema, akibusu paji la uso wangu. “John amelala. Na kuna unga wa mkate unaumuka juu ya kaunta. Tafadhali usiuguse.”

Nilitazama kupitia upenyo wa mlango pale yeye na Baba walipoendesha gari la kukokotwa na farasi kuelekea chini kwenye njia yetu ya vumbi. Nilijisikia fahari kwamba Mama aliniamini.

Nilipokuwa nikifagia jikoni, nilisimama kuangalia unga wa mkate. Nilisubiri kwa shauku Mama auoke usiku. Kwa kawaida tulikula mkate freshi uliookwa ukiwa na jemu iliyotengenezwa nyumbani. Lakini tuliishiwa jemu miezi mitatu iliyopita.

Jemu! Wazo lilinipa njaa ya kitu kitamu. Nilitazama juu kwenye chupa ya sukari, juu kabisa ya rafu. Nilijua Mama alikuwa akiitunza kutengeneza jemu nyingine zaidi.

Lakini kadiri zaidi nilivyofikiria kuhusu sukari, ndivyo nilivyohisi njaa. Hatimaye, nilivuta kiti karibu na rafu na kufika juu. Vidole vyangu vilikuwa karibu viguse chupa ya sukari. Niliivuta karibu kwenye ukingo wa rafu. …

Na kisha chupa iliteleza kutoka kwenye rafu! Nilijaribu kuidaka, lakini ilidondoka kwa kishindo kikubwa katikati kabisa ya unga wa mkate. Sukari ilimwagika kote kwenye mkate na kwenye rafu na juu ya sakafu.

“Jamani!” Nilipiga kelele. Kitendo hicho kilimwamsha mdogo wangu. Alianza kulia. Mimi nilitaka kulia pia. Ni nini mama atasema kuhusu jambo hili?

Baada ya kumbembeleza John, nilijitahidi kadiri niwezavyo kuondoa sukari. Nilivuta chupa kutoka kwenye unga na kuiosha. Nilifuta sukari kutoka kwenye kaunta na sakafuni. Lakini hakuna ambacho ningeweza kufanya kuondoa sukari kutoka kwenye unga.

Nilifikiria kuhusu kurudisha chupa juu ya rafu. Pengine Mama asingegundua ilikuwa tupu. Lakini nilijua kwamba hilo halikuwa sawa. Hivyo niliweka chupa juu ya meza na kumsubiri Mama na Baba warudi nyumbani.

Walipofika nyumbani, Mama aligundua chupa ya sukari mara moja.

Nilivuta pumzi ndefu. “Nilitaka tu kuonja sukari. Lakini niligonga chupa kutoka kwenye rafu. Nilijaribu kuisafisha, lakini sikuweza kuitoa kutoka kwenye unga wa mkate.” Maneno yalitoka kwa kasi pale nilipokuwa nimetazama chini sakafuni.

Mama alikuwa kimya kwa muda.

“Nisamehe,” Nilinong’ona.

Mama alishusha pumzi. “Sawa, nadhani mkate utakuwa mtamu kupitiliza usiku wa leo,” alisema Nilitazama juu. Alinipa tabasamu kidogo. “Asante kwa kutuambia kilichotokea.”

Tulipokula mkate wa sukari usiku ule, Mama na Baba pamoja na mimi tulizungumza kuhusu uaminifu.

“Sote tunafanya makosa mengi katika maisha,” Baba alisema. “Lakini tunapokuwa waaminifu na kujaribu kutubu, Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo wanafurahi. Daima tutabarikiwa kwa kuwa wakweli— hata kama inaonekana vigumu mwanzoni.”

Bado nilikuwa na huzuni kwamba nilimwaga sukari. Nilijua yawezekana tusingekuwa na jemu nyingi mwaka huu kwa sababu ya kosa langu. Lakini nilikuwa na furaha nilisema ukweli. Hiyo ilikuwa ni hisia nzuri ambayo hakuna kiasi cha sukari kingeweza kuileta. ●