2019
Ufunuo Binafsi
Aprili 2019


Vijana Wakubwa

Ufunuo Binafsi Mahususi

Ni kwa jinsi gani unaweza kuonyesha tofauti kati ya ufunuo na mawazo yako mwenyewe?

woman reading book

Kazi ya sanaa na Brian Kershisnik

Tunaishi katika ulimwengu wenye fursa nyingi. Tuna uhuru wa kuchagua kazi zetu wenyewe, shule, mwenza, wapi tunataka kuishi, na mengine mengi zaidi. Kweli ni baraka kubwa katika kizazi chetu. Lakini kwa upande mwingine, inafanya chaguzi hizi zote kuwa ngumu zaidi kwa sababu ni vigumu kufanya maamuzi wakati kukiwa na njia na fursa nyingi ambazo zitaongoza kwenye mambo mazuri. Tunawezaje kuchagua mema wakati kuna fursa nyingi ambazo ni njema? Unapohisi kupotea na kuchanganyikiwa katika dhoruba hii ya maamuzi, jua kwamba Baba wa Mbinguni anataka kukuongoza. Unaweza kuchagua njia sahihi na kupata majibu unayotafuta ikiwa utafuata sauti Yake. Tambua jinsi anavyozungumza na wewe, muamini Yeye, mfuate nabii, kuwa mvumilivu, kuwa mwenye msimamo wa kutegemea mazuri, na kuwa na imani, na hatimaye utaongozwa katika uelekeo sahihi.

—Vira Vashchenko, Kyiv, Ukraine

Kote katika maisha yangu nimeona jinsi Bwana alivyoniongoza, na kutambua kwamba mafanikio yangu yote ni shukrani Kwake na kwa mwongozo Wake. Hata katika nyakati ninapofikiri ninatembea peke yangu, mwishoni, huniacha nijue na kuhisi kwamba Yeye daima amekuwepo pale pamoja nami. Hiyo ndiyo maana nimefanya maamuzi ya kusonga mbele daima kwa imani, hata wakati ninapohisi kwamba niko peke yangu. Kwangu mimi, njia yangu haiko wazi wakati mwingine, na siwezi daima kuona kile kinachonisubiri huko baadaye, lakini daima ninachukua hatua za imani, na kisha ninaanza kuona nuru na kutambua mkono wa Mungu katika maisha yangu. Najua kwamba Baba yetu wa Mbinguni na Mwanawe, Yesu Kristo, wanatupenda na Wapo tayari kutuongoza, lakini Wao pia wanategemea sisi tuweke imani Kwao na kutenda pale tunapopokea msukumo wa kiungu kutoka kwa Roho.—

Indhira Mejia, Jamhuri ya Dominika

Pale ninapozidi kukua, imenibidi nijifunze lugha ya Roho. Roho huzungumza nami kupitia mawazo rahisi. Imechukua mazoezi kadhaa kuzoea hilo, lakini mara nyingi Roho huja kwangu katika mahali patulivu, kama vile nikiwa ndani ya gari yangu kuelekea kazini. Najua si mawazo yangu kwa sababu Roho mara nyingi atajipenyeza wakati ambapo sifikirii hata mada ile.

—Clarissa Mae Taylor, Utah, Marekani

Nadhani kwamba moja kati ya mbinu za kuvutia tunazopaswa kuwa na ujuzi nazo ni uwezo wa kutambua minong’ono laini ya Roho Mtakatifu. Kusoma maandiko kwa bidii kumenisukuma kuongeza ujuzi huo. Mara zote nimekuwa nikiamini kwamba yeye atafutaye kwa bidii atapata; na atafunuliwa siri za Mungu, kwa nguvu ya Roho Mtakatifu (ona 1 Nefi 10:19). Kwa maneno mengine, ikiwa ninataka kumtambua Roho, siwezi kujiacha niongozwe kwenye mawazo yasiyofaa au shughuli za kila siku za maisha, lakini badala yake ninapaswa kuzama kwenye kazi ya kujisahau. Hapo ndipo nitakuwa mzuri zaidi kuweza kumtambua Roho kwa sababu niko tayari kwa ajili ya hilo! Kama vile ambayo meli haiwezi kwa urahisi kusafiri katikati ya tufani, hatuwezi kumsikia Roho kama tumechukuliwa mbali na shughuli za maisha ambazo ziko nje ya uwezo wetu.—

Emmanuel Borngreat Dogbey, Accra, Ghana

couple

Katika familia yetu ndogo, tunamtambua Roho kwa sababu ya amani tunayohisi, hasa mimi na mume wangu pamoja kama wanandoa. Kama ni mawazo yetu wenyewe, hatuhisi kamwe kwamba ni kitu sahihi hasa—daima kunakuwepo na shaka au hofu. Lakini kama ni ufunuo, daima tunahisi amani, hata kama tunajaribu kujipa moyo na mambo hayaonekani kuleta maana mwanzoni. Tunapoufuata na kuufanyia kazi, daima tunaona mambo yakiwa sawa na kila kitu kinatendeka ilivyopaswa. Hapo ndipo tunapotazamana na kusema, “Ee sasa inaleta maana!”

—Maryana Wright, Utah, Marekani

Japokuwa sote tunaweza kupokea ufunuo binafsi kwa njia tofauti, kitu kimoja hakika ni cha kweli: Mungu huzungumza nasi mara kwa mara. Tunapaswa tu kuwa tayari kuweka juhudi ili kuongeza uwezo wetu wa kutambua na kusikia sauti Yake. Kama Rais Russell M. Nelson alivyoshauri: “Omba katika jina la Yesu Kristo kuhusu matatizo yako, hofu zako, udhaifu wako—ndio, mahitaji ya moyo wako. Na kisha sikiliza! Andika mawazo ambayo yanakuja kwenye akili yako. Andika hisia zako na zifuatilie kwa vitendo ambavyo unashawishiwa kufanya. Unaporudia mchakato huu siku baada ya siku, mwezi baada ya mwezi, mwaka baada ya mwaka, “utakua katika kanuni ya ufunuo.’” (Ufunuo kwa ajili ya Kanisa, Ufunuo kwa ajili ya Maisha Yetu,” Liahona, Mei 2018, 95).