“Mtazamo Wangu kutoka Juu,” Liahona, Machi 2023.
Sauti za Watakatifu wa Siku za Mwisho
Mtazamo Wangu kutoka Juu
Nilikuwa karibu kutupilia mbali kitu hasa nilichohitaji ili kufikia lengo langu.
Hivi karibuni, nilienda katika upandaji mlima ulio maarufu sana kwenye Roy’s Peak katika milima ya kupendeza ya Kisiwa cha Kusini mwa New Zealand. Kwa sababu upandaji wa mlima ulichukua masaa kadhaa, nilichukua kile tu nilichohitaji: vitafunwa kadhaa na maji mengi.
Nilipoanza, begi langu la mgongoni tayari lilikuwa zito. Nusu saa katika kupanda kwangu mlima, nilihisi uzito wa begi langu ukinielemea mabegani na mgongoni mwangu. Kwa muda, niliwaza kutupa baadhi ya chupa za maji. Lakini mara moja nilijua ningeyahitaji.
Saa moja na nusu kabla sijafika kileleni, njia ilizidi kuwa na mpando mkali na ilifunikwa na theluji. Nilianza kudhani sitafika kileleni, lakini lengo langu lilinipa msukumo wa kuendelea.
Hatimaye nilipofika kileleni, begi langu la mgongoni lilikuwa jepesi. Kwa wakati huo nilikuwa nimekwishakula vitafunwa vyangu na kunywa maji mengi. Nikiwa nimepumzika na nikiwa mwenye shukrani kwa ajili ya mwonekano wa kupendeza kutokea juu, nilitafakari juu ya safari yangu—kuelekea kilele cha mlima na katika maisha.
Kwa masaa kadhaa, nilitembea juu ya mlima, nikiulisha na kuupa maji mwili wangu ili kwamba nipate nguvu za kuendelea kupanda. Kile kilichoonekana kama mzigo mwanzoni—maji ya kuokoa maisha—yalinibariki mpaka kufikia lengo langu.
Sote tunapitia nyakati nzuri na nyakati mbaya, lakini Roho Mtakatifu hutusaidia tufanye maamuzi mazuri. Nilikuwa karibu kuacha zaidi ya nusu lita ya maji njiani, lakini nilihisi msukumo wa kuyatunza.
Kwa macho yenye machozi nilimshukuru Baba yangu wa Mbinguni kwa tafakuri hizi. Kuwa kwenye milima iliyofunikwa na theluji siku ile kulinipa msukumo wa kutathmini maisha yangu, maamuzi yangu, malengo yangu na begi langu la mgongoni.
Kabla ya kupanda kwangu mlima, nilijawa wasiwasi kuhusu maisha yangu na kazi yangu katika nchi ya ugeni. Lakini sasa ninahisi kwamba kila kitu kitakuwa sawa. Ninajua kwamba Bwana atanilinda.
Nikiwa pamoja na Roho, ninajua ninaweza kufanya maamuzi sahihi ambayo yataniinua kiakili na kiroho. Na ninapohisi kuzidiwa, ninaweza kumgeukia Mwokozi wetu, chanzo cha “maji yaliyo hai” (Yohana 4:10). Ninajua atanilisha na kuufanya rahisi mzigo wangu (ona Mathayo 11:28–30).