2023
Kila Kitu Kitakuwa Sawa
Machi 2023


“Kila Kitu Kitakuwa Sawa,” Liahona, Machi 2023.

Sauti za Watakatifu wa Siku za Mwisho

Kila Kitu Kitakuwa Sawa

Masaa yalionekana kutoisha hadi pale mmoja wa madaktari wa upasuaji alipomkaribia mama yangu katika chumba cha kusubiria.

Russell M Nelson akitazama mfano wa moyo

Picha ya Russell M. Nelson iliyopigwa na Eldon K. Linschoten

Mnamo miaka ya 1980, baba yangu, ambaye aliugua ugonjwa mbaya wa moyo, alifanyiwa upasuaji wa moyo ambao tulitarajia ungerefusha maisha yake.

Wakati huo, utaratibu uliogunduliwa ambao daktari wa upasuaji aliutumia ulikuwa mpya kwa nchi ya Uruguay. Daktari wa upasuaji alibadilisha mshipa wa aota kwa mshipa wa bandia. Hatimaye, utaratibu huo ulikuja kuwa maarufu na umeokoa maisha yasiyo na idadi.

Kwa sababu upasuaji ulihusisha utaratibu huu wa kimapinduzi, wataalamu wengi wa moyo walihudhuria, wakifuatilia upasuaji. Wakati madaktari wa upasuaji walipokuwa wakifanya kazi yao, mama yangu aliketi ndani ya chumba cha kusubiria akiwa na hofu. Masaa yalionekana kutoisha.

tulipata shangwe tulipopata taarifa kwamba upasuaji ulimalizika kwa mafanikio. Wakati wakitoka kwenye chumba cha upasuaji, mmoja wa madaktari wa upasuaji alijitenga na madaktari wengine wa upasuaji na alikwenda chumba cha kusubiria. Alikuwa daktari wa upasuaji mwalikwa ambaye alikuwa amekuja Uruguay ili kusimamia upasuaji.

Alimkaribia mama yangu na akamgusa kwa mguso wa hakikisho juu ya bega lake. Kisha, akimtazama machoni, alisema, “Kila kitu kitakuwa sawa.”

Daktari wa upasuaji alikuwa sahihi. Baba yangu aliishi kwa miaka mingine 24, akimtumikia Bwana kwa moyo wake wote—akiwa sasa mwenye afya—mpaka siku ya mwisho ya uhai wake.

Wakati wa mkutano mkuu wa Kanisa wa hivi karibuni, mama yangu alikumbushwa juu ya matembezi yale maalumu miaka mingi sana iliyopita. Bila shaka, anakumbuka kila mara pale daktari wa upasuaji mwalikwa—Rais Russell M. Nelson—anapozungumza na Watakatifu.

Manabii wote wa Bwana ni maalumu kwetu kwa njia fulani. Baadhi ni maalumu kwa sababu walitumikia kama Rais wa Kanisa wakati tukiwa wadogo. Baadhi ni maalumu kwa sababu walitumikia kama Rais wakati tulipobatizwa. Kwangu mimi na mama yangu, Rais Nelson ni maalumu kwa sababu yeye anafahamu kwamba kila utaratibu maalumu wa kitabibu humgusa si tu mgonjwa bali wapendwa wake pia. Anafahamu kwamba wanafamilia wanahitaji maneno ya kutia moyo, nguvu na kuleta hakikisho wakati afya au maisha ya mpendwa wao yanapokuwa hatarini.

Daima tutakuwa na shukrani kwa maneno ya hakikisho ya Rais Nelson miaka mingi iliyopita huko Uruguay na kwa maisha yake ya huduma kwa Baba wa Mbinguni na watoto wa Baba wa Mbinguni.