“Ulimwengu Wangu Ulipotiwa Kiza, Nilimgeukia Kristo,” Liahona, Machi 2023.
Vijana Wakubwa
Ulimwengu Wangu Ulipotiwa Kiza, Nilimgeukia Kristo
Pamoja na mambo mengi ya kiza yanayotokea kunizunguka, sikuwa na uhakika wa kile ilichomaanisha kuwa na msingi katika Kristo.
Katika ujumbe wa mkutano mkuu wa hivi karibuni, Rais Henry B. Eyring, Mshauri wa Pili katika Urais wa Kwanza, alizungumza kuhusu nyakati za hatari ulimwenguni: “Mtume Paulo alimwandikia Timotheo, ‘Lakini ufahamu neno hili, ya kuwa siku za mwisho kutakuwako nyakati za hatari’ (2 Timotheo 3:1).
“… Kwa hivyo itakuwa vigumu sana, si rahisi, kuheshimu maagano tunayolazimika kuyafanya na kuyatunza ili kuishi injili ya Yesu Kristo.”1
Niliposikia maneno haya, nilihisi wasiwasi. Nilikuwa tayari napambana na changamoto nyumbani kwangu Venezuela. Hivyo maswali kama vile, “Ninawezaje kuwa mwenye tumaini wakati ulimwengu umejawa kiza?” na “Ninawezaje kutazamia wakati ujao angavu katika wakati huu uliopo uliofunikwa na kiza?” yalikuwa moyoni mwangu wakati ule.
Lakini Rais Eyring alitoa suluhisho. Alinukuu Helamani 5:12, ambayo inazungumzia kujenga misingi yetu “juu ya mwamba wa Mkombozi wetu, ambaye ni Kristo.”
Siku zote nimekuwa nikiamini kwamba andiko hili lilikuwa kweli, lakini kujenga msingi wangu juu ya Mwokozi kulionekana rahisi zaidi kusema kuliko kutenda. Hata hivyo, kadiri ambavyo nimesogea karibu na Kristo, nimeona kwamba kila kitu kinafanyika kwa faida yako pale imani yako inapokuwa imara Kwake (ona Mafundisho na Maagano 90:24).
Kuhisi Kukataliwa
Miezi kadhaa iliyopita, nilipokea habari za kusikitisha kutoka kwa familia yangu. Ulimwengu wangu ulionekana kuvunjika mbele yangu. Nilihisi ganzi, kukanganyikiwa na wasiwasi kiasi kwamba niliugua!
Sikuelewa kwa nini tulikuwa tunapitia magumu yale wakati nilikuwa nikijitahidi kuwa mwaminifu. Nilijiuliza ikiwa nilikuwa nimefanya jambo ambalo si sahihi. Kesho yangu ilionekana kuwa na kiza na nilihisi kukataliwa na Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo.
Katikati ya mateso yangu, nilizungumza na rafiki mwema. Aliniambia jambo ambalo kamwe siwezi kulisahau: “nadhani hali hii ni fursa nzuri kwako kutafakari juu ya uhusiano wako binafsi na Bwana. Bila kujali nini kinatokea, ni juu yako kumgeukia Yeye kwa ajili ya msaada. Ikiwa utafanya hivyo, Yeye atakupa upendo na faraja unayoihitaji sasa.”
Maneno hayo yalibadili mtazamo wangu. Nilikuwa mwenye hasira na niliyeumizwa na kuvurugwa kwa hali zangu, lakini nilikuwa na uchaguzi. Bila kujali kile tunachopitia, hofu tulizonazo au hali ngumu tunazopitia, Yesu Kristo daima yupo karibu nasi. Tunao uchaguzi wa kugeuka kumwelekea Yeye kwa imani, si mbali Naye, katika nyakati za matatizo.
Hivyo ndivyo tunavyoimarisha msingi wetu wa imani Kwake na kustahimili magumu katika ulimwengu. Kwa kumchagua Yeye.
Kama vile Mzee D. Todd Christofferson wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili alivyofundisha: “Katikati ya moto huu wa kutakasa, badala ya kumkasirikia Mungu, sogea karibu na Mungu. Mwombe Baba katika jina la Mwana. Tembea pamoja Nao katika Roho, siku hadi siku. Waruhusu Wao kadiri muda unavyosonga wadhihirishe uaminifu Wao kwako. Tafuta kwa hakika kuwajua Wao na kwa hakika kujijua wewe mwenyewe.”2
Kristo alikuwa akiningoja nimgeukie Yeye kwa ajili ya msaada. Hiyo haikumaanisha kwamba angesababisha matatizo yote yaondoke au kurekebisha kila kitu katika maisha yangu na familia yangu papo kwa papo, lakini alinisaidia kuwa bora, kupata shangwe na kutakaswa zaidi.
Na baada ya muda, kadiri nilivyomtafuta Mwokozi kupitia sala, kujifunza maandiko na kupitia imani, Yeye alinisaidia kuwasamehe wanafamilia yangu na kualika shangwe kwenye maisha yangu tena, ingawa baadhi ya changamoto bado hazijatatulika.
Ahadi ya Usalama
Hizi hakika ni siku za mwisho. Tunasikia kuhusu vita na tetesi za vita, kuhusu majanga ya ulimwenguni kote, kuhusu majanga ya asili—na nina hakika zitakuwepo hata nyakati ngumu zaidi mbeleni. Hata hivyo, kujenga juu ya mwamba ambao ni Yesu Kristo na kumtumaini Yeye daima kutatuletea amani na shangwe, licha ya kile tunachopitia. Kama vile ambavyo Rais Eyring pia amefundisha, “Kwa wale kati yetu ambao tunajijali sisi wenyewe pamoja na wale tunaowapenda, kuna tumaini katika ahadi ya Mungu aliyoitoa ya mahali pa usalama katika dhoruba zijazo.”3
Ni ahadi yenye nguvu na ya kupendeza iliyoje. Na nimeona ahadi hiyo ikitimia katika maisha yangu. Ninajua kwamba hii ni injili ya urejesho ya Yesu Kristo na kwamba Yeye ni chemchemi ya baraka zote. Yeye ni nuru, Yeye ni Mwokozi wetu na sisi ni kondoo Wake. Acha tumchague Yeye na tuchague imani.
Mwandishi anaishi Zulia, Venezuela.