“Kufuata Mfano wa Kristo: Kuwajali Walio katika Shida,” Liahona, Machi 2023.
Kufuata Mfano wa Kristo: Kuwajali Walio katika Shida
Kuanzia uzalishaji wa chakula hadi kwenye mwitikio wa dharura hadi kwenye kuhudumu, kuna njia nyingi ambazo kupitia hizo tunaweza kuonesha upendo kwa jirani zetu.
Kama wafuasi wa Yesu Kristo, waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho wanajitahidi kuishi amri kuu mbili: kumpenda Mungu na kumpenda jirani yetu (ona Mathayo 22:37–39). Kufuata amri hizi kuu mbili na mfano wa Yesu Kristo ndicho kinacholiongoza Kanisa na waumini wake kuwahudumia wenye shida.
Kwa hivyo, ni jinsi gani Kanisa husaidia kuwajali wenye shida? Na ni jinsi gani waumini hushiriki katika kazi hii kuu?
Njia za Kusaidia
Kama waumini wa Kanisa, tunajaribu kuwatafuta wenye shida na kutoa msaada kwa watoto wote wa Mungu bila kujali mbari yao, utaifa au dini yao.
Tunawajali wenye shida katika njia nyingi, ikiwa ni pamoja na:
-
Kufunga na kutumia matoleo ya mfungo.
-
kuhudumiana.
-
Programu za kujitegemea.
-
Programu za ulimwenguni za chakula, elimu, maji safi na huduma za afya.
-
Mwitikio wa Dharura.
-
Miradi ya kujitolea katika jumuia.
Wakati baadhi ya juhudi za kibinadamu za Kanisa ni kubwa katika kipimo, hata juhudi ndogo ndogo zinaweza kwa pamoja kuleta matokeo makubwa. Hapa ni baadhi ya mifano ya jinsi waumini wa Kanisa wanavyowasaidia wenye shida.
Kuhudumu katikati ya Migogoro
RaeAnn na Sterling Jarvis—waumini wa Kanisa wa Warsaw, Uholanzi—hawakujua nini cha kutarajia wakati walipochagua kuwapa makazi wakimbizi katika nyumba yao. Lakini walikuwa radhi kusaidia katika njia yoyote ambayo wangeweza.
Punde baada ya migogoro kuanza huko Ulaya, familia ya Kiukreini ya watu watano iliwasili mlangoni kwao mnamo saa 7 usiku. Walikuwa wamesafiri takriban maili 500 (km 800) kutafuta usalama. Akina Jarvis waliwakaribisha Maryna na Serhii Bovt pamoja na watoto wao watatu nyumbani kwao. Baada ya muda walikuza upendo halisi na kujali kwa familia ya Bovt. “Unaposhiriki upendo, upendo huo hukua,” Maryna alisema juu ya mfano wa huduma wa akina Jarvis. “Unatufanya tuwe karibu na kila mmoja na karibu na Bwana.”
Kama waumini wa Kanisa, tunajitahidi kufuata mfano wa Mwokozi kwa kuwahudumia wale walio karibu nasi. Watu hawahitaji kuwa wakimbizi wa vita au mateso ili wahitaji kusaidiwa. Kila tendo la ukarimu kwa upande wetu—bila kujali ni dogo kiasi gani—linaweza kuathiri maisha ya mtu kwa wema.
Jumuia ya Kushirikiana
Kwenye Shamba la Mazao la Laie Hawaii linalomilikiwa na Kanisa, zaidi ya familia 310 hulima mazao ili kusaidia watu wa nyumbani mwao. Kwenye maeneo yao yenye hekari 1.25, familia hizi hulima taro, tapioka, viazi vitamu, matunda mkate, mapera na mazao mengine yanayostawi kisiwani.
Shamba linasimamiwa na wamisionari wanandoa na hupata usaidizi kutoka kwa wamisionari na waumini wengine. Watu hawa wa kujitolea husafisha ardhi, huandaa udongo kwa ajili ya upandaji na hufundisha ujuzi muhimu wa kilimo.
Kwa sababu ya wamisionari hawa, waumini na watu hawa wa kujitolea, wengi wanaohitaji chakula katika Hawaii wanaweza kujikimu vyema pale kazi zinapoadimika. Jumuia huwa imara pale watu wanapofanya kazi kwa kushirikiana ili kulitunza shamba na kushiriki pamoja kile wanachokipanda.
Miradi ya shuguli za kibinadamu ya Kanisa husaidia kutoa usalama wa chakula, elimu, maji safi na huduma za afya kwa mamilioni ya watu ulimwenguni kote. Kanisa pia linatoa rasilimali nyingi ili kukuza wigo wa kujitegemea, ikiwa ni pamoja na ghala la akiba la askofu, vituo vya kazi, maduka ya Deseret Industries, Huduma za ushauri za Familia, kozi za kujitegemea na mashamba yanayomilikiwa na Kanisa na bustani kama vile Shamba la Mazao la Laie Hawaii. Miradi hii mara zote hupata hisani kutoka kwa waumini na wamisionari, ambao michango yao isiyo na ubinafsi ya muda, vipawa na rasilimali zingine huleta tofauti kubwa sana kwa wenye shida.
Tendo la Urafiki
Mnamo 2021, takriban waumini 200 wa Kanisa waliitikia wito wa kusaidia. Walikwenda kwenye vituo huko Ujerumani, Marekani na maeneo mengine kusaidia kuwapanga takriban wakimbizi 55,000 kutoka Afghanistan.
Watu wengi wa kujitolea walihudumu kwenye vituo hivi kwa wiki mbili au tatu na wengine walikaa muda mrefu zaidi. Waumini wa Kanisa walikidhi mahitaji ya dharura ya wale waliohitaji kimbilio kwa kutoa chakula, mavazi na vifaa vingine.
Akina dada wa Muungano wa Usaidizi nchini Ujerumani waligundua kwamba baadhi ya wanawake wa Kiafghani walikuwa wakitumia mashati ya waume zao kufunika vichwa vyao badala ya nguo zao za kitamaduni za kufunikia vichwa, ambazo zilipotea au kuharibika kwenye vurugu za uwanja wa ndege. Akina dada hawa wa Muungano wa Usaidizi walikusanyika kushona nguo za kitamaduni za Kiislamu kwa ajili ya wanawake hawa wenye shida—wakionesha ukarimu na heshima kwa wengine, wakiweka kando tofauti zao za imani.
Dada Sharon Eubank, mkurugenzi wa Hisani za Watakatifu wa Siku za Mwisho, alisema “Juhudi zetu binafsi si lazima zihitaji pesa au maeneo ya mbali; zinahitaji mwongozo wa Roho Mtakatifu na moyo ulio radhi kumwambia Bwana, ‘Mimi hapa; nitume mimi’ [Isaya 6:8].”1
Hamu ya kuhudumu wakati majanga yanapotokea ndiyo sababu ya Kanisa mara zote kuwa moja ya kundi la kwanza kuitikia—kwa vyote msaada wa muda mfupi na msaada wa muda mrefu. Kazi ya waumini wa Kanisa na wamisionari huwasaidia wenye shida wahisi salama, wapokee matunzo ya kimwili na kiakili na wahisi upendo wa Mungu kupitia ukarimu wa wengine.
Kuitwa katika Kazi
Mafundisho na Maagano 4:3 inasema, “ kama unayo tamaa ya kumtumikia Mungu wewe umeitwa kwenye kazi hiyo.” Pamoja na yale yote ambayo Kanisa linafanya, zipo njia nyingi za kutumikia.
Juhudi nyingi zilizopangiliwa za Kanisa za kuwasaidia wenye shida zinawezekana tu kwa huduma ya wamisionari na waumini. Si kila mtu anaweza kuikaribisha familia ya mkimbizi, kukidhi mahitaji ya kimwili ya watu wengine au kuacha kila kitu ili kusaidia kwenye majanga. Lakini kila mtu ana sehemu ya kufanya na mchango wa kila mtu unatambulika na kuthaminiwa.
Moja ya njia muhimu waumini wanayotumia kutoa kwenye kazi hii ni kupitia matoleo ya mfungo na michango ya kibinadamu. Michango hii mitakatifu hutumika kuwasaidia wale wenye shida kubwa na huleta matokeo makubwa kwenye maisha ya wale waliosaidiwa. Waumini wa Kanisa wanaweza kutumikia misheni za shughuli za kibinadamu, kusaidia kuratibu kozi za kujitegemea na kujitolea kwenye ghala la akiba la askofu na maduka ya Deseret Industries. Unaweza pia kuwajali wenye shida kupitia huduma za eneo husika, michango ya damu, majukumu ya kuhudumu, sala na huduma nyingine zaidi.
Sote tumeitwa kwenye kazi. Sote tumeitwa kufuata mfano wa Yesu Kristo na kumpenda Mungu na kumpenda jirani yetu. Vyote tunavyohitaji ni moyo ulio radhi.