2023
Ukumbusho Wangu wa Mnara wa Kengele
Machi 2023


“Ukumbusho Wangu wa Mnara wa Kengele,” Liahona, Machi 2023.

Sauti za Watakatifu wa Siku za Mwisho

Ukumbusho Wangu wa Mnara wa Kengele

Kama ningefanyia kazi msukumo, tungepata muda zaidi wa kumfundisha Giuseppe injili.

mnara wa kengele

Siku moja ya matayarisho, mimi na mmisionari mwenzangu tulikuwa tumetembelea kanisa kuu la dayosisi huko Parma, Italia. Wakati tukistaajabia michoro ya kupendeza mahala pale, nilimwona mtawa akisoma karibu nasi. Nilipokea msukumo wa kuzungumza naye kuhusu Kitabu cha Mormoni, lakini niliogopa.

Ni kwa jinsi gani mtawa wa Kikatoliki atamkubalia mmisionari anayefundisha injili ndani ya dayosisi? Msukumo ulikuja tena, lakini kwa mara ya pili niliupuuzia.

Wiki kadhaa baadaye, wazee wengine wawili katika makazi yetu walituambia kwamba walikutana na mtawa aliyeitwa Giuseppe wakati wakitafuta watu wa kuwafundisha mtaani. Baada ya kumfundisha somo, alikubali nakala ya Kitabu cha Mormoni.

Wakati wamisionari walipokutana na Giuseppe wiki moja baadaye, alikuwa tayari amesoma sehemu kubwa ya kitabu. Alikuwa amefurahishwa sana kuhusu kitabu.

Kabla ya wamisionari kukutana na Giuseppe tena, mwenzangu alihamishwa, hivyo niliungana nao. Wakati tulipokwenda kumfundisha Giuseppe ndani ya dayosisi, sikushangazwa kuona kwamba alikuwa mtawa yuleyule niliyepata msukumo wa kuzungumza naye siku za nyuma.

Giuseppe alituambia kuwa alikuwa akisoma kitabu cha Alma, ambaye alimfananisha na Mtume Paulo. Tuliamua kumfundisha somo la pili, ambalo lilihitimishwa kwa mwaliko wa kubatizwa. Mwishoni mwa somo letu, punde kabla hatujamwalika Giuseppe kufuata mfano wa Yesu Kristo kwa kubatizwa, kengele za dayosisi zilianza kupiga, zikitupa mshtuko.

Giuseppe alikuwa amesahau kuhusu muda na alisema alihitaji kujiunga na watawa wenzake kwa ajili ya sala za mchana. Kisha aliomba radhi, akisema hatakuwepo katika siku za baadaye kwa sababu alikuwa anakwenda kwenye shughuli za kitawa. Utawazo wake kuwa kuhani ungefuatia shughuli hizo.

Tulishangazwa jinsi wakati huo muhimu ulivyoyeyuka. Ikiwa ningefanyia kazi msukumo wangu wa mwanzo, tungepata muda zaidi wa kumfundisha Giuseppe na angepata muda wa kumaliza kusoma Kitabu cha Mormoni. Kwa kadiri ninavyojua, wamisionari hawakumfundisha tena.

Baada ya uzoefu ule, sauti za kengele za mnara wa saa zilinikumbusha jinsi muda ulivyo wa thamani na mfupi. Kwa misheni yangu yote iliyosalia, kila mara niliposikia kengele ya mnara ikipiga, nilipata motisha ya kuzungumza na mtu yeyote niliyeweza kuzungumza naye kuhusu injili. Leo hii, bado ninajitahidi kufuata msukumo kutoka kwa Roho.