“Msaada na Tumaini kutoka kwenye Mkutano Mkuu,” Liahona, Machi 2023.
Sauti za Watakatifu wa Siku za Mwisho
Msaada na Tumaini kutoka kwenye Mkutano Mkuu
Sikuwahi kutarajia kusikia mkutano mkuu wote ukizungumzia kile hasa nilichokuwa napitia.
Baada ya kujifungua mtoto wangu wa kwanza, nilipata msongo wa mawazo. Ulikuwa wakati mzuri kwangu kwa sababu nilikuwa nimepata mtoto wa kiume, lakini sikupata kamwe shangwe ya kuwa na mtoto kwa sababu nilikuwa na mawazo.
Katika kipindi hiki cha majaribu, niliomba sana kwa Baba wa Mbinguni. Nilimwomba anisaidie nishinde jaribu hili gumu. Mkutano mkuu ukiwa unakaribia katika majira yale ya majani kupukutika, niliomba pia kwamba nipate faraja kutoka kwenye mahubiri ya viongozi wa Kanisa.
Niliposikiliza mahubiri wakati wa kipindi cha kwanza cha mkutano mkuu, nilianza kuhisi kufarijika. Kisha, wakati wa kipindi cha pili, Mzee Jeffrey R. Holland wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili alizungumza kuhusu msongo wa mawazo. Alisema msongo wa mawazo unaweza kutufanya tuhisi kuwa kama “chombo kilichovunjika”1 (Zaburi 31:12). Sikuwahi kutarajia kusikia hubiri lote likihusu kile hasa nilichokuwa napitia.
Huu ulikuwa wakati wa kipekee kwangu. Hubiri lilinisaidia nielewe kwamba Baba wa Mbinguni ananipenda na kwamba ananijua. Yeye alielewa kile nilichokuwa napitia. Alitaka kunisaidia na kunipa tumaini. Alifanya hivyo kupitia maneno ya Mzee Holland.