Liahona
Uso Dirishani
Machi 2024


“Uso Dirishani,” Liahona, Machi 2024.

Sauti za Watakatifu wa Siku za Mwisho

Uso Dirishani

Nilifikiri jirani yangu alikuwa mwenye kuchunguza sana mambo ya wengine, lakini niligundua alihitaji rafiki tu.

picha ya Maija-Kaarina Mäkinen

Picha kwa hisani ya mwandishi

Mara nyingi niliona sura ile ile ikiangalia kutoka dirisha la jengo. Niliwaza, “Je, si ya kusikitisha kwamba mtu fulani mara kwa mara anatazama nje ya dirisha lao, kuchunguza shughuli za majirani zao?”

Kisha siku moja niliwaza pengine ningeenda kuuliza kama ningeweza kuwa mwenye msaada. Niliamua kwenda na mkate uliookwa siku hiyohiyo.

Mkate wa moto uliyeyusha barafu katika moyo wa jirani yangu mkongwe. Kwa machozi aliniambia jinsi alivyojihisi mpweke. Hakuna aliyemtembelea na hakuna aliyempigia simu, hata watoto wake mwenyewe. Kwa mkono unaotetemeka, alipangusa machozi kutoka mashavuni mwake.

Alishusha pumzi na kisha alisema, “Ni vizuri jinsi gani ingekuwa kuondoka tu kwenye ulimwengu huu. Simhukumu yeyote ninapoangalia kutoka kwenye dirisha langu. Nawaangalia tu watoto wakicheza na vitu vingine vikiendelea uwanjani.”

mwanamke akiangalia nje dirishani

Kielelezo na Alex Nabaum

Baada ya muda tulizungumza kuhusu injili. Mara ya kwanza alikuwa kimya kwa sababu mume wake alitumikia kama kiongozi katika kanisa lingine. Lakini kadiri tulivyozungumza zaidi, ndivyo alivyovutiwa zaidi na ukweli nilioshiriki kuhusu Yesu Kristo na injili Yake iliyorejeshwa.

“Ni ajabu kwamba sote tuna Yesu yule yule!” alisema. “Je, tutaonana mbinguni?”

“Ndiyo,” nilijibu, “tutakuwa huko pamoja—tukishikana mkono kwa mkono.”

Kutoka wakati ule na kuendelea, tulikuwa marafiki wazuri kwa miaka mingi, mpaka hatimaye alipofariki kutoka ulimwengu huu.

Sasa ninapenda kuwaza kwamba jirani yangu wa zamani anaangalia kutoka dirisha la nyumba yake ya mbinguni, akifuatilia shughuli zetu na tukitumaini kuwa tunayo amani ya kutosha na upendo kati yetu.