“Nilizungukwa na Watu lakini Bado Nilihisi Upweke,” Liahona, Machi. 2024.
Vijana Wakubwa
Nilizungukwa na Watu lakini Bado Nilihisi Upweke
Nilipohamia mbali na nyumbani, muunganiko wangu na mbinguni ulinisaidia nishinde upweke.
Unaijua hisia ile pale ambapo umezungukwa na watu lakini bado unahisi mpweke kabisa?
Tangu niondoke nyumbani kwetu Uganda na kuhamia Dubai kwa ajili ya kazi, nimehisi upweke karibu kila mara. Huko nyumbani katika ujirani wangu, watu husalimiana wao kwa wao mtaani. Tulijuana. Tulisaidiana. Nilikuwa na marafiki wengi na familia ambao walikuwa wa imani yangu.
Lakini haikuwa hivyo hapa. Ninaishi katika utamaduni tofauti kabisa, katika jiji kubwa na lililozungukwa na watu wanaofanya kazi za shughuli nyingi. Na hata kama ninahudhuria kata yangu na nimejaribu kutaka kuwajua vijana wakubwa wengine na waumini wa kata, ratiba zetu za kazi zenye shughuli nyingi zinafanya isiwezekane kuonana zaidi ya masaa machache tu tunayoyatumia kanisani kila wiki.
Dubai ni kubwa na yenye mvuto, na ninashukuru kuwa hapa. Lakini inaweza kuwa yenye kuchosha, hususani wakati unapohisi upweke. Watu wana vingi mno hapa, na wanaonekana kuwa na maisha yao yalipangiliwa vizuri. Hata hivyo, ninapoishi miongoni mwa vitu hivi vyote vya gharama na majumba haya mazuri, wakati mwingine ninajiuliza:
Je! ninafanya nini na maisha yangu? Je! hii ni sehemu sahihi kwangu?
Kupata Kuwa wa Mahala fulani Tena
Mzee D. Todd Christofferson wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili alieleza kwamba “hisia ya kustahili kuwa wa mahala fulani ni muhimu kwa ustawi wetu kimwili, kiakili, na kiroho.”1 Nilikuwa sijawahi kutambua jinsi hisia ya kuwa wa mahala fulani ilivyo muhimu hadi pale nilipokuwa siwezi kuhisi tena—siyo kanisani na siyo popote, kwa kweli.
Je! ni kwa jinsi gani nianze kuitafuta sasa, mbali na kila mtu niliyempenda?
Baada ya muda, nilianza kutambua “umuhimu wa Yesu Kristo katika kustahili kuwa wa mahala fulani.”2
Kadiri nilivyoendelea kuwakosa rafiki zangu na familia, nilianza kuona kwamba sikuwa nimetengwa na kila mtu maishani mwangu wakati nilipohama—bado nilikuwa na Mwokozi na Baba wa Mbinguni mwenye upendo ambao siku zote walitaka kubakia wameunganika nami.
Kwa hiyo nilianza kufanya kile nilichoweza ili kuungana na Wao kila siku. Nilianza kusikiliza Njoo,Unifuate ili nijifunze mawasilisho wakati nilipokwenda kukimbia. Nilivaa vipokea sauti kichwani nikiwa kazini na nilisikiliza maandiko nilipokuwa nikitekeleza kazi.
Cha muhimu zaidi, nilijifunza kwamba zawadi ya kupendeza ni kuweza kusali moja kwa moja kwa Baba wa Mbinguni. Ninazungumza Naye sana mara kwa mara na kwa umakini zaidi kuliko nilivyowahi kufanya kipindi cha nyuma. Ninapohisi upweke, ninasali na kuhisi faraja Yake. Ninapoandika barua pepe na kujaribu kubaki mwenye subira kwa wafanyakazi wenzangu, ninasali na kumwomba Yeye msaada.
Ninapenda kile Rais Thomas S. Monson (1927–2018) alichosema kuhusu sala: “Kwa wale … ambao wanahangaika na changamoto na matatizo makubwa na madogo, sala ni mtoaji wa nguvu ya kiroho, ni pasipoti ya amani. Sala ni njia ambayo tunamkaribia Baba Yetu wa Mbinguni, ambaye anatupenda. Zungumza Naye katika sala na kisha sikiliza jibu. Miujiza inaletwa kupitia sala.”3
Kwa kutenga muda kwa ajili Yao katika maisha yangu, hususani kupitia sala ya dhati, nilianza kuona kwamba ingawa sikuwa nimezungukwa na watu wangu na utamaduni wangu mwenyewe, bado niliweza kuzungukwa na Roho na kuhisi upendo wa Mungu.
Tunaweza Siku Zote Kuunganishwa.
Mambo bado ni magumu, lakini nina tumaini kwa ajili ya siku zijazo. Na nimekuja kuamini kile Kaka Milton Camargo, Mshauri wa Kwanza katika Urais wa Mkuu wa Shule ya Jumapili, alichofundisha: “Bwana Yesu Kristo yu hai leo. Yeye anaweza kuwa uwepo hai, wa kila siku katika maisha yetu. Yeye ni suluhu ya shida zetu, lakini sisi lazima tuinue macho yetu na tuinue uoni wetu ili tumwone Yeye.”4
Mimi bado ni mpweke wakati mwingine, lakini ninajua kwamba daima, daima nitaweza kusali kwa Baba yangu wa Mbinguni na kufikia Upatanisho wa Yesu Kristo.
Kwa kusimama au kupiga magoti, peke yangu au katika kundi, ninaweza kusali.
Ninaweza kumlilia Baba wa Mbinguni.
Ninaweza kutoa shukrani.
Ninaweza kuomba kwa ajili ya mwongozo na ulinzi.
Na kupitia muunganiko wangu wa agano, ninajua kwamba mimi ni binti wa Baba wa Mbinguni mwenye upendo, daima nitakuwa Wake. Kupitia mwongozo Wake, ninaweza kuhisi kujiamini kwamba niko mahali sahihi, nikifanya kile ambacho Yeye angependa mimi nifanye.