“Tafadhali Okoa Maisha ya Mama,” Liahona, Machi. 2024.
Sauti za Watakatifu wa Siku za Mwisho
Tafadhali Okoa Maisha ya Mama
Nilikuwa na hofu wakati mama yangu alipohitaji upasuaji wa wazi wa moyo, lakini mwalimu wa msingi mwenye bidii alinifundisha kuomba.
Nilipokuwa na umri wa miaka 10, mama yangu alipata mshtuko mkubwa wa moyo. Alikaa wiki nyingi hospitalini akipigania maisha yake.
Wakati huu, mwalimu wangu wa Msingi, Dada Ellen Johnson, alikuja nyumbani kwetu mara moja kwa wiki kuniangalia. Ndiyo kwanza nilikuwa nimeanza tu kuhudhuria Msingi na nilikuwa na upeo mdogo wa uelewa wa injili. Kila wiki Dada Johnson alitoa ushuhuda kwangu na alizungumza kuhusu sala. Alinifundisha kwamba kama ningeomba, Baba wa Mbinguni angejibu.
Baada ya wiki kadhaa, afya ya mama ilififia zaidi. Alikuwa na valvu ya moyo iliyoharibika ambayo ilihitaji kurekebishwa. Daktari wake alisema angekufa bila majaribio ya upasuaji wa moyo. Nafasi yake ya kupona, hata hivyo, ilikuwa tu takribani 50/50.
Upasuaji wa wazi wa moyo ulikuwa mpya na hatarishi mwanzoni mwa miaka ya 1960. Madaktari wa upasuaji walipanga kumfungua mama kuanzia kifuani mpaka kwenye uti wake wa mgongo na kisha kugawanya kizimba cha mbavu zake ili kuufikia moyo wake. Wagonjwa wengi hawakunusurika katika upasuaji huu. Nilihuzunika na kuogopa kwamba mama yangu angekufa.
Baba alikuwa muda mwingi yuko kazini au hospitalini na Mama. Dada yangu mkubwa, Pam, alituangalia mimi na kaka yangu. Usiku, nilihisi mpweke na mwoga, lakini nilifikiri kuhusu kile Dada Johnson alichokuwa akinifundisha kuhusu maombi. Mara nyingi nilipiga magoti karibu na kitanda na nililia, nikimsihi Baba wa Mbinguni ayaokoe maisha ya Mama.
Wakati mmoja wa maombi kama hayo ya kilio, amani kuu ilikuja juu yangu na niliacha kulia. Nilihisi kwamba kila kitu kingekuwa SAWA. Nilihisi kuhakikishiwa kwamba mama yangu ataishi kuniona mimi nikikua na kwamba sihitaji kuwa na wasiwasi. Sikusikia sauti au kuona ono, lakini nilikuwa na hisia ya ukimya, yenye amani. Sikuwa na mashaka na hisia hizo. Baba wa Mbinguni alikuwa amejibu maombi yangu, na nilijua hivyo.
Mama alinusurika kwenye upasuaji huo. Alikuwa dhaifu na mgonjwa muda mwingi wa maisha yake, lakini Baba wa Mbinguni alikwisha jibu sala yangu na aliyaokoa maisha yake. Aliishi kuniona mimi nikikua, kuolewa, na kupata watoto.
Miaka mingi baadaye, wakati Rais Russell M. Nelson alipokuwa Mtume, Mama aliniambia alikuwa ndiye daktari wa moyo ambaye aliokoa maisha yake. Nilimwandikia barua kumshukuru. Wakati alipojibu, alinishukuru kwa ajili ya barua yangu na alikiri msaada wa Mungu katika kazi yake.