Mlango wa 30
Korihori, mpinga Kristo, anamfanyia mzaha Kristo, Upatanisho, na roho ya unabii—Anafundisha kwamba hakuna Mungu, hakuna kuanguka kwa binadamu, hakuna adhabu kwa dhambi, na hakuna Kristo—Alma anashuhudia kwamba Kristo atakuja na vitu vyote vinashuhudia kuwa kuna Mungu—Korihori anadai ishara na anaangushwa na kusababishwa kuwa bubu—Ibilisi alikuwa amemtokea Korihori kama malaika na kumfundisha cha kusema—Korihori anakanyagwa chini na kufa. Karibia mwaka 76–74 K.K.
1 Tazama, sasa ikawa kwamba baada ya watu wa Amoni kuimarishwa kwenye nchi ya Yershoni, ndiyo, na pia baada ya Walamani kukimbizwa kutoka nchini, na wafu wao kuzikwa na watu wa nchi hiyo—
2 Sasa wafu wao hawakuhesabiwa kwa sababu ya wingi wa idadi yao; hata wafu wa Wanefi hawakuhesabiwa—lakini ikawa baada ya kuzika wafu wao, na pia baada ya siku za kufunga, na kuomboleza, na sala, (na ulikuwa mwaka wa kumi na sita wa utawala wa waamuzi kwa watu wa Nefi) kulianza kuwa na mfululizo wa amani kote nchini.
3 Ndiyo, na watu walijitahidi kuweka amri ya Bwana; na walikuwa wakamilifu kwa kuweka masharti ya Mungu, kulingana sheria ya Musa; kwani walifundishwa kutii sheria ya Musa hadi itakapotimizwa.
4 Kwa hivyo watu hawakuwa na msukosuko wowote katika mwaka wa kumi na sita wa utawala wa waamuzi juu ya watu wa Nefi.
5 Na ikawa kwamba katika mwaka wa kumi na saba wa utawala wa waamuzi, kulikuwa na mfululizo wa amani.
6 Lakini ikawa kwenye mwisho wa mwaka wa kumi na saba, kulikuja mtu kwenye nchi ya Zarahemla, na alikuwa mpinga Kristo, kwani alianza kuhubiria watu dhidi ya unabii ambao ulizungumzwa na manabii, kuhusiana na kuja kwa Kristo.
7 Sasa hakukuwa na sheria yeyote dhidi ya imani ya mtu; kwani ilikuwa kinyume kabisa cha amri za Mungu kwamba kuwe na sheria inayoleta watu kutokuwa sawa.
8 Kwani hivyo ndivyo yasemavyo maandiko: Chagua wewe siku ya leo, yule ambaye utamtumikia.
9 Sasa kama mtu alitaka kumtumikia Mungu, ilikuwa ni haki yake; kwa usahihi zaidi kama aliamini katika Mungu ilikuwa ni haki yake kumtumikia; lakini kama hakuamini kwake hakukuwa na sheria ya kumwadhibu.
10 Lakini kama aliua aliadhibiwa kwa kifo; na kama alipora aliadhibiwa pia; na kama aliiba aliadhibiwa pia; na kama alizini aliadhibiwa pia; ndiyo, kwa huu uovu wote waliadhibiwa.
11 Kwani kulikuwa na sheria kwamba watu walihukumiwa kulingana na makosa yao. Walakini, hakukuwa na sheria dhidi ya imani ya mtu; kwa hivyo, mtu aliadhibiwa tu kwa makosa ambayo alikuwa amefanya; kwa hivyo watu wote walikuwa sawa.
12 Na huyu mpinga Kristo, ambaye jina lake lilikuwa Korihori, (na sheria haingemshika) alianza kuhubiria watu kwamba hakutakuwa na Kristo. Na jinsi hii alihubiri, akisema:
13 Ee ninyi ambao mmefungiwa chini ya upumbavu na tumaini la bure, kwa nini mnajiweka mzigo na vitu vya upumbavu kama hivi? Kwa nini mnamtafuta Kristo? Kwani hakuna yeyote ajuaye chochote kitakachokuja.
14 Tazama, hivi vitu ambavyo mnaita unabii, ambavyo mnasema vinatolewa na manabii watakatifu, tazama, ni mila za upumbavu za baba zenu.
15 Mnajuaje ukweli wao? Tazama, hamwezi kujua vitu ambavyo hamuoni; kwa hivyo hamwezi kujua kwamba kutakuwa na Kristo.
16 Mnaona mbele na kusema kwamba mnaona msamaha wa dhambi zenu. Lakini tazama, ni matokeo ya wenda wazimu wa akili; na hii michafuko ya akili yenu inawajia kwa sababu ya desturi za babu zenu, ambazo zinawaongoza mbali kwa kuamini kwa vitu ambavyo havipo.
17 Na vitu vingi vya aina hii aliwazungumzia, akiwaambia kwamba hakutakuwa na upatanisho utakaofanywa kwa dhambi za watu, lakini kila mtu hufaulu katika maisha haya kulingana na vile alijiendesha; kwa hivyo kila mtu alifanikiwa kulingana na akili yake, na kila mtu alishinda kulingana na nguvu yake; na chochote ambacho mtu alifanya si kosa.
18 Na hivyo aliwahubiria, akipotosha mbali mioyo ya wengi, na kuwafanya kubeba vichwa vyao kwa uovu, ndiyo, akidanganya wanawake wengi, na pia wanaume, kutenda ukahaba—akiwaambia kwamba mtu akifa, huo ndiyo mwisho wake.
19 Sasa huyu mtu alienda hadi kwenye nchi ya Yershoni pia, kuhubiri vitu hivi miongoni mwa watu wa Amoni, ambao walikuwa awali watu wa Walamani.
20 Lakini tazama walikuwa werevu kuliko wengi wa Wanefi; kwani walimchukua, na kumfunga, na kumbeba na kumpeleka mbele ya Amoni, ambaye alikuwa kuhani mkuu juu ya watu hao.
21 Na ikawa kwamba alilazimisha kwamba atolewe nje ya nchi. Na akaenda kwenye nchi ya Gideoni, na akaanza kuwahubiria pia; na pale hakufaulu sana, kwani alichukuliwa na kufungwa na kupelekwa mbele ya kuhani mkuu, pia mwamuzi mkuu juu ya nchi.
22 Na ikawa kwamba kuhani mkuu alimwambia: Kwa nini unazunguka ukiharibu njia za Bwana? Kwa nini unafundisha hawa watu kwamba hakutakuwa na Kristo, kukatisha furaha yao? Kwa nini unazungumza ubaya dhidi ya unabii wote wa manabii watakatifu?
23 Sasa jina la kuhani mkuu lilikuwa Gidona. Na Korihori akamwambia: Kwa sababu sifundishi desturi za upumbavu za babu zenu, na kwa sababu sifundishi hawa kujizuia wenyewe chini ya masharti na utaratibu ambao uliwekwa na makuhani wa zamani, kujitwalia nguvu na uwezo kwao, kuwaweka katika ujinga, kwamba wasiweze kubeba vichwa vyao, lakini wawekwe chini kufuatana na maneno yako.
24 Unasema kwamba hawa watu ni watu huru. Tazama, nasema wako kwenye utumwa. Unasema kwamba ule unabii wa zamani ni wa kweli. Tazama, nasema kwamba hujui kwamba ni kweli.
25 Unasema kwamba watu hawa wana makosa na ni watu walioanguka, kwa sababu ya dhambi ya mzazi. Tazama, nasema kwamba mtoto si mkosaji kwa sababu ya wazazi wake.
26 Na unasema pia kwamba Kristo atakuja. Lakini tazama, nasema kwamba hujui kwamba kutakuwa na Kristo. Na unasema kwamba atauawa kwa sababu ya dhambi za ulimwengu—
27 Na hivyo unawapoteza hawa watu kufuata desturi za upuuzi za babu zenu, na kulingana na kutaka kwako; na unawaweka chini, hata vile walivyokuwa kwenye utumwa, kwamba ujishibishe na kazi ya mikono yao, ili wasiangalie juu na ujasiri, na kwamba wasifurahie haki na mapendeleo yao.
28 Ndiyo, hawatumii ile ambayo ni yao wasije wakachukiza makuhani wao, ambao wanawataabisha kufuatana na kutaka kwao, na wamewafanya kuamini, kupitia desturi zao na ndoto zao na upuzi wao na maono yao na siri za kujifanya, kwamba, ikiwa hawafanyi kufuatana na maneno yao, watachukiza kiumbe ambacho hakijulikani, ambaye wanasema ni Mungu—kiumbe ambacho hakijaonekana au kujulikana, ambacho hakikuwepo wala hakitakuwepo.
29 Sasa kuhani mkuu na mwamuzi mkuu walipoona ugumu wa moyo wake, ndiyo, walipoona kwamba atatukana hata Mungu, hawakumjibu lolote kwa maneno yake; lakini wakasababisha kwamba afungwe; na walimkabidhi katika mikono ya askari, na wakampeleka katika nchi ya Zarahemla, kwamba angeletwa mbele ya Alma, na mwamuzi mkuu ambaye alikuwa mtawala juu ya nchi yote.
30 Na ikawa kwamba wakati alipopelekwa mbele ya Alma na mwamuzi mkuu, aliendelea kusema kwa njia sawa vile alivyofanya kwenye nchi ya Gideoni; ndiyo, aliendelea kukufuru.
31 Na aliongea maneno kwa sauti kubwa mbele ya Alma, na kuwatukana makuhani na walimu, akiwashtaki kwa kuwapoteza watu kwa kufuata desturi za ujinga za babu zao, kwa nia ya kujishibisha kwa kazi ya watu.
32 Sasa Alma alimwambia: Unajua kwamba hatujishibishi sisi wenyewe kwa kazi ya watu hawa; kwani tazama nimefanya kazi hata kutokea mwanzo wa utawala wa waamuzi mpaka sasa, kwa mikono yangu kwa kujitegemea, ingawa nilikuwa na safari nyingi kuzunguka nchi nikitangaza neno la Mungu kwa watu wangu.
33 Na ingawa nimefanya kazi nyingi kanisani, sijapokea hata zaidi ya senine moja kwa kazi yangu; wala hata mmoja wa ndugu zangu, isipokuwa wakati tulikuwa kwenye kiti cha kutoa hukumu; na wakati huo tumepokea tu kulingana na sheria kwa wakati wetu.
34 Na sasa, kama hatuwezi kupokea chochote kwa kazi yetu kanisani, itatufaidi nini kufanya kazi kanisani isipokuwa tu kutangaza ukweli, ili tuweze kushangilia kwa shangwe kwa raha ya ndugu zetu?
35 Basi kwa nini wewe unasema kwamba tunawahubiria hawa kupata faida, wakati wewe, mwenyewe, unajua kwamba hatupati faida yoyote? Na sasa unaamini kwamba tunadanganya hawa watu, ili tusababishe shangwe ndani ya mioyo yao?
36 Na Korihori akamjibu, Ndiyo.
37 Na kisha Alma akasema kwake: Unaamini wewe kwamba kuna Mungu?
38 Na akajibu, La.
39 Sasa Alma akasema kwake: Utakataa kwamba kuna Mungu, na pia kumkana Kristo? Kwani tazama, nakwambia, najua kuna Mungu, na pia kwamba Kristo atakuja.
40 Na sasa ni ushahidi gani unao kwamba hakuna Mungu, au kwamba Kristo hatakuja? Nakwambia wewe kwamba huna lolote, isipokuwa tu maneno yako.
41 Lakini, tazama, nina vitu vyote kama ushahidi kwamba hivi vitu ni kweli; na wewe pia una vitu vyote kama ushuhuda kwako kwamba ni vya kweli; na utakana hivi vitu? Unaamini kwamba hivi vitu ni kweli?
42 Tazama, najua kwamba unaamini, lakini unaongozwa na roho wa uwongo, na umeweka mbali Roho ya Mungu ili isiwe na pahali ndani yako; lakini ibilisi ana uwezo juu yako, na anakubeba kila mahali, akifanya ujanja ili aangamize watoto wa Mungu.
43 Na sasa Korihori alimwambia Alma: Ikiwa utanionyesha ishara, kwamba ningesadikishwa kuwa kuna Mungu, ndiyo, nionyeshe kwamba ana uwezo, na ndipo nitakubali ukweli wa maneno yako.
44 Lakini Alma akamwambia: Wewe umepata ishara za kutosha; utamjaribu Mungu wako? Unaweza kusema, Nionyeshe ishara, wakati una ushuhuda wa hawa ndugu zako wote, na pia manabii watakatifu? Maandiko yamewekwa mbele yako, ndiyo, na vitu vyote vinaonyesha kwamba kuna Mungu; ndiyo, hata dunia, na vitu vyote vilivyo juu yake, ndiyo, na mwendo wake, ndiyo, na pia sayari zote ambazo huenda kwa utaratibu wao zinashuhudia kwamba kuna Muumba Mkuu.
45 Na bado unaenda ukizunguka, ukidanganya mioyo ya watu hawa, ukitoa ushuhuda kwamba hakuna Mungu? Na bado utakana huu ushahidi wote? Na akasema: Ndiyo, nitakana isipokuwa unionyeshe ishara.
46 Na ikawa kwamba Alma akamwambia: Tazama, nimesikitika kwa sababu ya ugumu wa moyo wako, ndiyo, kwamba utazidi kushindana na roho ya ukweli, kwamba nafsi yako iangamizwe.
47 Lakini tazama, ni afadhali roho yako ipotee kuliko kwamba uwe njia ya kuleta roho nyingi kwenye maangamizo, kwa udanganyifu wako na maneno yako ya kusifu ya uongo; kwa hivyo kama utakana tena, tazama Mungu atakupiga wewe, kwamba uwe bubu, kwamba hutafungua kinywa chako mara nyingine, kwamba hutaweza kudanganya hawa watu mara nyingine.
48 Sasa Korihori akamwambia: Sikatai kuweko kwa Mungu, lakini siamini kwamba kuna Mungu; na ninasema pia, kwamba hujui kuwa kuna Mungu; na isipokuwa unionyeshe ishara, sitaamini.
49 Sasa Alma akamwambia: Hii nitakupatia kwa ishara, kwamba utapigwa na kuwa bubu, kufuatana na maneno yangu; na ninasema, kwamba kwa jina la Mungu, utafanywa bubu, kwamba hutatamka tena.
50 Sasa wakati Alma alipokuwa amenena maneno haya, Korihori alipigwa na akawa bubu, kwamba hangeweza kunena tena, kufuatana na maneno ya Alma.
51 Na wakati mwamuzi mkuu alipoona hivi, alinyosha mkono wake na kuandika kwa Korihori, akisema: Umesadikishwa kwa nguvu za Mungu? Kwake ambaye ulitaka Alma aonyeshe ishara? Ulitaka kwamba atese wengine, akionyesha ishara? Tazama amekuonyesha ishara; na sasa hutabishana zaidi?
52 Na Korihori alinyoosha mkono wake na kuandika, akisema: Najua kwamba mimi ni bubu, kuwa siwezi kuongea; na ninajua kwamba hakuna kingine isipokuwa nguvu ya Mungu pekee ndiyo iliyoweza kuniletea mimi haya; ndiyo, na nilikuwa kila siku najua kwamba kuna Mungu.
53 Lakini tazama, ibilisi amenidanganya; kwani alinitokea kwa mfano wa malaika, na akaniambia; Nenda na urudishe hawa watu, kwani wote wamepotea wakifuata Mungu asiyejulikana. Na akaniambia: Hakuna Mungu; ndiyo, na akanifundisha yale ambayo ninahitaji kusema. Na nimefundisha maneno yake; na niliyafundisha kwa sababu yalikuwa yanapendeza kwa akili ya kimwili; na niliyafundisha, hata ikawa ninafaulu sana, hata kwamba niliamini kwamba yalikuwa ya kweli; hata mpaka nimejiletea hii laana kuu kwangu.
54 Sasa wakati alikuwa amesema haya; alimsihi Alma kwamba amuombee Mungu, kwamba laana itolewe kwake.
55 Lakini Alma alimwambia: Laana hii ikitolewa kwako utapoteza mioyo ya watu tena; kwa hivyo, itakuwa nawe hata vile Bwana atakavyohitaji.
56 Na ikawa kwamba laana haikutolewa kutoka kwa Korihori; lakini alitupwa nje, na akaenda akitembea kutoka nyumba hadi nyingine akiomba chakula.
57 Sasa ufahamu wa yaliyompata Korihori mara moja ilitangazwa kote nchini; ndiyo, tangazo lilitolewa na mwamuzi mkuu kwa watu wote nchini, ikitangaziwa wale ambao walikuwa wameamini maneno ya Korihori kwamba lazima watubu mara moja, isije hukumu sawa ikaletwa kwao.
58 Na ikawa kwamba wote walisadikishwa kwa uovu wa Korihori; kwa hivyo wote walimgeukia tena Bwana; na hii ikaweka mwisho kwa uovu wa aina ya Korihori. Na Korihori alienda kutoka moja nyumba hadi nyingine, akiomba chakula kwa kujiweka hai.
59 Na ikawa kwamba alienda miongoni mwa watu, ndiyo, miongoni mwa watu ambao walikuwa wamejitenga kutoka kwa Wanefi na kujiita Wazoramu, wakiongozwa na mtu ambaye jina lake lilikuwa Zoramu—na alipoenda miongoni mwao, tazama, alishambuliwa na kukanyagwa chini, hadi akafa.
60 Na hivyo tunaona mwisho wa yule ambaye anapotosha njia za Bwana; na hivyo tunaona kwamba ibilisi hatasaidia watoto wake siku ya mwisho, lakini anawachukua kwa mbio hadi jehanamu.