Mlango wa 40
Kristo anasababisha kuwepo ufufuo wa binadamu wote—Wenye haki wakifa wataenda peponi na waovu nje gizani kungojea wakati wa ufufuo wao—Vitu vyote vitarudishwa kwa umbo lao jema na kamilifu kwenye Ufufuo. Karibia mwaka 74 K.K.
1 Sasa mwana wangu, hapa nina mengine mengi ningependa kukwambia; kwani nafikiria kwamba akili yako ina wasiwasi kuhusu ufufuo wa wafu.
2 Tazama, nakwambia, kwamba hakuna ufufuo—au, ningesema, kwa maneno mengine kwamba mwili wenye kufa haujiviki kutokufa, ya uharibifu haijiviki kutoharibika—mpaka baada ya kuja kwa Kristo.
3 Tazama, anawezesha ufufuo wa waliokufa kutendeka. Lakini tazama, mwana wangu, ufufuo haujatimizwa bado. Sasa, nafichua kwako siri; walakini, kuna siri nyingi ambazo zimefichwa, ambazo hakuna azijuaye isipokuwa Mungu mwenyewe. Lakini ninakuonyesha kitu kimoja ambacho nimemwuliza Mungu kwa bidii ili nipate kujua—ambayo inahusu ufufuo.
4 Tazama, kuna wakati ambao umewekwa kwamba wote watatokea kutoka wafu. Sasa wakati huu utakapotimia hakuna ajuaye; lakini Mungu anajua wakati ambao umewekwa.
5 Sasa, kama kutakuwa wakati mmoja, au wakati wa pili, au wakati wa tatu, kwamba wafu watafufuka kutoka kwa wafu, haijalishi; kwani Mungu anajua hivi vitu vyote; na ninatosheka kujua kwamba hii ndiyo hali—kwamba kuna wakati ambao umechaguliwa kwamba wote watafufuka kutoka kwa wafu.
6 Sasa lazima kuwe na nafasi kati ya wakati wa kifo na wakati wa kufufuka.
7 Na sasa nitakuuliza ni nini kitatokea kwa roho za binadamu kutoka wakati huu wa kifo hadi wakati uliowekwa wa kufufuka?
8 Sasa kama kutakuwa na zaidi ya wakati moja ambao umewekwa kwa watu kuamka haijalishi; kwani wote hawafi wakati mmoja, na hii haijalishi; wakati wote ni kama siku moja kwake Mungu, na wakati hupimwa tu na watu.
9 Kwa hivyo, kuna wakati ambao umewekewa watu kwamba wataamka kutoka kwa wafu; na kuna nafasi kati ya wakati wa kifo na ufufuo. Na sasa, kuhusu nafasi hii ya muda, kitakachotokea kwa roho za watu ni kitu ambacho nimeuliza kwa bidii kwa Bwana nijue; ni hiki ndicho kitu ninachojua.
10 Na wakati majira yatapofika wakati wote wataamka, ndipo watakapojua kwamba Mungu anajua wakati wote ambao amewekewa mtu.
11 Sasa, kuhusu hali ya roho kati ya kifo na ufufuo—Tazama, nimejulishwa na malaika, kwamba roho za watu wote, mara zinapotoka kwa mwili huu wa muda, ndiyo, roho za watu wote, zikiwa njema au ovu, zinachukuliwa nyumbani kwa yule Mungu ambaye alizipatia uhai.
12 Na ndipo itakuja kuwa kwamba roho za wale walio haki zinapokelewa kwa hali ambayo ni ya furaha, ambayo inaitwa peponi, hali ya kupumzika, hali ya amani, ambapo zitapumzikia kutoka kwa taabu zao zote na kutoka kwa mashaka yote, na masikitiko.
13 Na ndipo itakuwa kwamba, zile roho za waovu, ndiyo, ambazo ni ovu—kwani tazama, hazina kipande au sehemu ya Roho wa Bwana; kwani tazama, walichagua matendo maovu kuliko matendo mema; kwa hivyo roho wa ibilisi aliingia ndani yao, na akamiliki nyumba yao—na hawa watatupwa nje katika giza la nje kabisa; huko kutakuwa na kulia, na kuomboleza, na kusaga meno, na hii ni kwa sababu ya uovu wao wenyewe, wakiongozwa kifungoni kwa mapenzi ya ibilisi.
14 Sasa hii ni hali ya roho ya waovu, ndiyo, kwenye giza, na kwa hali ya kutisha, na kuogopesha wakitarajia hasira na uchungu wa ghadhabu ya Mungu juu yao; hivyo wanabaki kwenye hali hii, na vile vile walio wenye haki huko peponi, hadi wakati wao wa ufufuko.
15 Sasa, kuna wachache ambao wanaelewa kwamba hii hali ya furaha na hii hali ya taabu ya roho, kabla ya ufufuo, ilikuwa na ufufuo wa kwanza. Ndiyo, nakubali inaweza kuitwa ufufuo, kuamka kwa roho au nafsi na upatanisho kwa furaha au taabu, kulingana na maneno yaliyozungumzwa.
16 Na tazama, imezungumziwa tena, kwamba kuna ufufuo wa kwanza, au ufufuo wa wale ambao wamekwisha kuwepo, au ambao wako, au watakaokuwa, hadi ufufuo wa Kristo kutoka kwa wafu.
17 Sasa, hatuwezi kudhani kwamba huu ufufuo wa kwanza, ambao umezungumziwa kwa njia hii, unaweza kuwa ufufuo wa roho na upatanisho wao kwa furaha au taabu. Huwezi kudhani kwamba hii ndiyo inamaanisha.
18 Tazama, nakwambia, Hapana; lakini inaamanisha kuunganisha roho na mwili, kwa wale kutoka siku za Adamu hadi kwa ufufuo wa Kristo.
19 Sasa, kama roho na miili ya wale ambao wamezungumziwa itaunganishwa yote mara moja, waovu sawa na wenye haki, sisemi; ni ya kutosha kwangu kusema kwamba, wote watainuka; au kwa njia nyingine, ufufuko wao utakuja kupita kabla ya ufufuko wa wale ambao hufa baada ya kufufuka kwa Kristo.
20 Sasa, mwana wangu, sisemi kwamba ufufuko huja wakati wa kufufuka kwa Kristo; lakini tazama, ninatoa kama maoni yangu, kwamba roho na miili zitaunganishwa, za wale wenye haki, katika ufufuko wa Kristo, na kupaa kwake mbinguni.
21 Lakini kama itakuwa wakati wa ufufuko wake au ya baadaye, sisemi; lakini hii yote nasema, kwamba kuna nafasi kati ya kifo na ufufuko wa mwili, na hali ya roho ndani ya furaha au shida mpaka wakati ambao umechaguliwa na Mungu kwamba wafu wataamka, na kuunganishwa, vyote roho na mwili, na kuletwa na kusimama mbele ya Mungu, na kuhukumiwa kulingana na vitendo vyao.
22 Ndiyo, hii italeta kurudishwa kwa vitu ambavyo vimezungumziwa na midomo ya manabii.
23 Roho itarudishwa kwa mwili, na mwili kwa roho; ndiyo, na kila sehemu na kiungo kitarudishwa kwa mwili wake; ndiyo, hata nywele ya kichwa haitapotea; lakini vitu vyote vitarudishwa kwa umbo lake sahihi na kamilifu.
24 Na sasa, mwana wangu, huku ni kurudisha ambako kumezungumzwa na midomo ya manabii—
25 Na ndipo wale wenye haki wataangʼaa ndani ya ufalme wa Mungu.
26 Lakini tazama, kifo cha kutisha kitawajia waovu; kwani wanakufa kulingana na vitu vilivyo vya haki; kwani hawako safi, na hakuna kitu kichafu kitakachorithi ufalme wa Mungu; lakini watatupwa nje, na kutolewa kupokea matunda ya vitendo vyao au kazi zao, ambazo zimekuwa mbovu; na wanakunywa machicha ya kikombe kikali.