Sehemu ya 90
Ufunuo kwa Joseph Smith Nabii, uliotolewa huko Kirtland, Ohio, 8 Machi 1833. Ufunuo huu ni hatua ya kuendelea katika kuanzisha Urais wa Kwanza (ona kichwa cha habari cha sehemu ya 81); kama matokeo yake, washauri waliotajwa walitawazwa 18 Machi 1833.
1–5, Funguo za ufalme zimekabidhiwa kwa Joseph Smith na kupitia kwake kwenda Kanisani; 6–7, Sidney Rigdon na Frederick G. Williams watatumikia katika Urais wa Kwanza; 8–11, Injili itahubiriwa kwa mataifa ya Israeli, kwa Wayunani, na kwa Wayahudi, kila mtu akiisikia katika lugha yake mwenyewe, 12–18, Joseph Smith na washauri wake wataliweka Kanisa katika mpangilio unaostahili, 19–37, Watu binafsi mbalimbali wameshauriwa na Bwana kutembea wima na kutumikia katika ufalme Wake.
1 Hivyo ndivyo asemavyo Bwana, amini, amini ninakuambia mwanangu, dhambi zako zimesamehewa, kulingana na maombi yako, kwani sala zako na sala za ndugu zako zimenijia masikioni mwangu.
2 Kwa hiyo, umebarikiwa wewe kutoka sasa wewe ubebaye funguo za ufalme zilizotolewa kwako; ufalme ambao unakuja kwa mara ya mwisho.
3 Amini ninakuambia, funguo za ufalme hazitaondolewa kutoka kwako, wakati wewe ukiwapo katika ulimwengu, wala katika ulimwengu ujao;
4 Hata hivyo, kupitia kwako mafunuo ya Mungu yatatolewa kwa mwingine, ndiyo, hata kwa kanisa.
5 Na wale wote ambao hupokea mafunuo ya Mungu, na wajihadhari jinsi wanavyoyashikilia wasije wakayahesabu kuwa kitu rahisi, na wakaletwa chini ya hatia kwa njia hii, na wakajikwaa na kuanguka wakati dhoruba ishukapo, na upepo kuvuma, na mvua kushuka, na kupiga juu ya nyumba zao.
6 Na tena, amini ninawaambia ndugu zako, Sidney Rigdon na Frederick G. Williams, dhambi zao zimesamehewa pia, nao wanahesabiwa kuwa sawa na wewe katika kushikilia funguo hizi za ufalme huu wa mwisho;
7 Kama vile kupitia utawala wako funguo za shule ya manabii, ambayo nimeamuru kuanzishwa;
8 Ili hapo waweze kukamilishwa katika huduma yao kwa wokovu wa Sayuni, na wa mataifa ya Israeli, na wa Wayunani, kadiri wengi watakavyoamini;
9 Ili kupitia huduma yako waweze kupokea neno, na kupitia huduma yao neno liweze kuenea hata miisho ya dunia, kwa Wayunani kwanza, na halafu, tazama, na lo, watageuka kwa Wayahudi.
10 Na halafu yaja siku wakati mkono wa Bwana utakapofunuliwa katika uwezo kwa kuyashawishi mataifa, mataifa ya wapagani, nyumba ya Yusufu, juu ya injili ya wokovu wao.
11 Kwani itakuja kutokea katika siku ile, kwamba kila mtu atasikia utimilifu wa injili katika ulimi wake, na katika lugha yake mwenyewe, kupitia wale waliotawazwa kwa uwezo huu, kwa huduma ya Mfariji, aliyemwagwa juu yao kwa ajili ya ufunuo wa Yesu Kristo.
12 Na sasa, amini ninakuambia, ninakupa amri kuwa uende katika huduma na urais.
13 Na utakapokuwa umemaliza kutafsiri ya manabii, utaanza kusimamia shughuli za kanisa na za shule;
14 Na mara kwa mara, kama itakavyofunuliwa na Mfariji, kupokea mafunuo ili kuzifichua siri za ufalme;
15 Na kuyaweka vyema makanisa, na kusoma na kujifunza, na kuvifahamu vitabu vyote vilivyo vizuri, na lugha, ndimi, na watu.
16 Na hii itakuwa shughuli na kazi yenu katika maisha yenu yote, kuongoza katika baraza, na kuweka vyema mambo yote ya kanisa hili na ufalme.
17 Msiaibike, wala kufadhaika; bali nawaonya kuhusu majivuno na kiburi, kwani hivyo huleta mitego juu ya nafsi zenu.
18 Ziwekeni sawa sawa nyumba zenu; uvivu na uchafu viwekeni mbali na ninyi.
19 Sasa, amini ninakuambia, na ipatikane nafasi, haraka itakavyowezekana, kwa ajili ya familia ya mshauri na mwandishi wako, hata Frederick G. Williams.
20 Na mtumishi wangu mzee Joseph Smith, Mkubwa aendelee kukaa pamoja na familia yake mahali anapoishi sasa; na isiuzwe hadi kinywa cha Bwana kitakapotamka.
21 Na mshauri wangu, hata Sidney Rigdon, abaki mahali anapoishi sasa hadi kinywa cha Bwana kitakapotamka.
22 Na askofu atafute kwa bidii ili kumpata wakala, na awe mtu aliye na mali ghalani—mtu wa Mungu, na mwenye imani kubwa—
23 Ili kwamba kwa njia hiyo awezeshwe kufuta kila deni; ili ghala ya Bwana isiweze kudharauliwa mbele za macho ya watu.
24 Tafuteni kwa bidii, ombeni daima, na muwe wenye kuamini, na mambo yote yatafanyika kwa pamoja kwa faida yenu, kama ninyi mnatembea wima na kukumbuka agano ambalo mmeagana ninyi kwa ninyi.
25 Na familia zenu ziwe ndogo, hususani ya mtumishi wangu mzee wa umri Joseph Smith, Mkubwa, juu ya wale ambao si wa familia zenu;
26 Ili vitu vile vilivyotolewa kwa ajili yenu, ili kutimiza kazi yangu, visichukuliwe kutoka kwenu na kupewa wale ambao hawastahili—
27 Na kwa njia hiyo mmezuiliwa katika kukamilisha mambo yale ambayo nimewaamuru.
28 Na tena, amini ninawaambia, ni mapenzi yangu kuwa mjakazi wangu Vienna Jaques apate fedha za kulipia gharama zake, na kwenda katika nchi ya Sayuni;
29 Na masalia ya fedha hizo zaweza kuwekwa wakfu kwangu, naye atapewa thawabu yake katika wakati wangu.
30 Amini ninawaambia, hilo ni jema machoni mwangu kwamba yampasa kwenda katika nchi ya Sayuni, na kupokea urithi kutoka mikononi mwa askofu;
31 Ili akaweze kutulia katika amani ilimradi atakuwa mwaminifu, na asiwe mvivu katika siku zake kuanzia sasa na kuendelea.
32 Na tazama, amini ninawaambia, kuwa ninyi mtaandika amri hii, na kuwaambia ndugu zenu katika Sayuni, katika salamu ya upendo, kuwa nimewateua ninyi pia kuisimamia Sayuni katika wakati wangu mwenyewe.
33 Kwa hiyo, waache kunichosha kuhusu jambo hilo.
34 Tazama, ninawaambia kuwa ndugu zenu katika Sayuni wanaanza kutubu, na malaika wanafurahi juu yao.
35 Hata hivyo, mimi sijapendezwa na mambo mengi; na mimi sijapendezwa na mtumishi wangu William E. McLellin, wala mtumishi wangu Sidney Gilbert; na askofu pia, na wengineo wanayo mambo mengi ya kutubu.
36 Lakini amini ninawaambia, kwamba Mimi, Bwana, nitagombana na Sayuni, na nitawasihi wenye nguvu wake, na kumrudi hadi ashinde na kuwa safi mbele zangu.
37 Kwani hataondoshwa kwenye mahali pake. Mimi, Bwana, nimenena haya. Amina.