Urithi wa Tumaini wa Thamani Mno
Unapochagua kama utafanya ama utaweka agano na Mungu, unachagua kama utaacha urithi wa tumaini kwa wale ambao huenda wakafuata mfano wako.
Akina ndugu na dada zangu wapendwa, baadhi yenu mlialikwa kwa mkutano huu na wamisionari wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Wamisionari hao huenda wameshawaalika kufanya chaguo kufanya agano na Mungu kwa kubatizwa.
Wengine wenu mnasikiliza kwa sababu mlikubali aliko la mzazi, mke, ama pengine mtoto, lililotolewa kwenu kwa tumaini kwamba mtachagua kuweka maagano ambayo tayari mmefanya na Mungu kuwa msingi wa maisha yenu tena. Baadhi yenu ambao mnasikiliza tayari mmefanya chaguo la kurudi kumfuata Mwokozi na leo mnahisi furaha ya kukaribishwa Naye.
Haijalishi wewe ni nani na mahali ulipo, unao uwezo wa kushawishi furaha ya watu wengi zaidi ya wale unaweza kufikiria sasa. Kila siku na kila saa unaweza kuchagua kufanya ama kuweka agano na Mungu.
Popote ulipo kwenye njia ya kurithi karama ya uzima wa milele, unayo fursa ya kuwaonyesha watu wengi njia inayoelekeza kwa furaha kuu. Unapochagua kama utafanya ama utaweka agano na Mungu, unachagua kama utaacha urithi wa tumaini kwa wale ambao huenda wakafuata mfano wako.
Wewe nami tumebarikiwa na ahadi ya urithi kama huo. Ninawajibika kwa ajili ya wingi wa furaha yangu maishani kwa mtu ambaye sikuwahi kukutana naye katika maisha duniani. Alikuwa yatima ambaye alikuwa mmoja wa mababu zangu. Aliniachia urithi wa tumaini wa thamani mno. Acheni niwaelezee jukumu alilotekeleza katika kujenga urithi huo kwa ajili yangu.
Jina lake lilikuwa Heinrich Eyring. Alizaliwa katika familia iliyokuwa na mali nyingi. Babake, Edward, alikuwa na shamba kubwa kule Coburg, ambako sasa ni Ujerumani. Mamake alikuwa Binti wa kifalme Charlotte Von Blomberg. Babake alikuwa mlinzi wa ardhi kwa ajili ya mfalme wa Prussia.
Heinrich alikuwa mtoto wa kwanza wa Charlotte na Edward. Charlotte aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 31, baada ya kuzaliwa kwa mtoto wake wa tatu. Edward aliaga dunia punde baadaye, akiwa amepoteza nyumba zake na mali yake yote katika biashara iliyoanguka. Alikuwa na umri wa miaka 40 peke yake. Aliwaacha watoto watatu mayatima.
Heinrich, babu yangu, alikuwa amewapoteza wazazi wake wote na urithi mkubwa wa kidunia. Alikuwa hana pesa. Aliandika katika jarida lake la historia kwamba alihisi kwamba tumaini lake la maisha mazuri lilikuwa katika kuenda Marekani. Ingawa hakuwa na familia wala marafiki kule, alikuwa na hisia ya tumaini kuhusu kwenda Marekani. Kwanza alienda Jiji la New York. Baadaye alihama kwenda St. Louis, Missouri.
Kule St. Louis, mmoja wa wafanyikazi wenzake alikuwa Mtakatifu wa Siku za Mwisho. Kutoka kwake alipata nakala ya kijitabu kilichoandikwa na Mzee Parley P. Pratt. Alikisoma na kisha akajifunza kila kitu angepata kuhusu Watakatifu wa Siku za Mwisho. Aliomba kujua kama ni kweli kulikuwa na malaika ambao waliwajia binadamu, kama kulikuwa na nabii aliye hai, na kama alikuwa amepata dini ya kweli iliyofunuliwa na Mungu.
Baada ya miezi miwili ya kujifunza na kuomba kwa makini, Heinrich alikuwa na ndoto ambapo aliambiwa alikuwa abatizwe. Mtu ambaye jina lake na mamlaka ya ukuhani ninaheshimu, Mzee William Brown, angetekeleza agizo hili. Heinrich alibatizwa katika bwawa la maji ya mvua mnamo Machi 11, 1855, saa 7:30 asubuhi.
Ninaamini kwamba Heinrich alijua wakati huo kwamba kile ninachowafunza hivi leo ni kweli. Alijua kwamba furaha ya uzima wa milele huja kupitia uhusiano wa familia ambao huendelea milele. Hata wakati alikuwa amepata mpango wa furaha wa Bwana hivi karibuni, alijua kwamba tumaini lake la furaha ya milele lilitegemea chaguo za kibinafsi za wengine kufuata mfano wake. Tumaini lake la furaha ya milele lilitegemea watu ambao bado hawakuwa wamezaliwa.
Kama sehemu ya urithi wa familia yetu ya tumaini, aliaacha jarida la historia kwa kizazi chake.
Katika jarida hilo la historia ninaweza kuhisi upendo wake kwa wale miongoni mwetu ambao wangemfuata. Kutoka kwa maneno yake ninahisi tumaini lake kwamba kizazi chake kingechagua kumfuata kwenye njia kurudi nyumbani kwetu mbinguni. Alijua kwamba haingekuwa chaguo moja kuu kufanya hivyo lakini chaguo nyingi ndogo. Ninanukuu kutoka kwa historia yake:
“Kutoka mara ya kwanza nilimsikia Mzee Andrus akizungumza … daima nimehudhuria mkutano wa Watakatifu wa Siku za Mwisho na nyakati ambazo nimekosa kuhudhuria mkutano zimekuwa nadra sana, ikiwa ni wajibu wangu kuhudhuria mikutano hii.
“Ninaandika haya katika jarida langu ili kwamba watoto wangu waweze kuiga mfano wangu na kamwe wasipuuze wajibu huu muhimu [kukusanyika pamoja] na Watakatifu.”1
Heinrich alijua kwamba katika mikutano ya sakramenti tungeweza kufanya upya ahadi yetu kumbuka Mwokozi daima na kupata Roho Wake kuwa nasi.
Ni roho hiyo ambayo ilimhimili kwenye misheni yake ambako aliitwa miezi michache tu baada ya kukubali agano la ubatizo. Aliacha kama urithi wake mfano wake wa kubaki mwaminifu kwa misheni yake kwa miaka sita katika sehemu ambayo wakati huo iliitwa Indian Territories. Ili kupokea kuachiliwa kwake kutoka misheni yake, alitembea kutoka Oklahoma hadi Jiji la Salt Lake, umbali wa takribani maili 1,100 (1,770 km).
Muda mfupi baadaye aliitwa na nabii wa Mungu kuhama na kwenda Utah kusini. Kutoka hapo alikubali wito mwingine kuhudumu misheni katika nchi yake ya kuzaliwa, Ujerumani. Kisha alikubali aliko la Mtume wa Bwana Yesu Kristo kusaidia kujenga makoloni ya Watakatifu wa Siku za Mwisho kule Mexico kaskazini. Kutoka hapo aliitwa kwenda Jiji la Mexico kama mmisionari wa muda tena. Alitekeleza wito huu. Amezikwa katika mavani madogo kule Colonia Juárez, Chihuahua, Mexico.
Nasoma mambo haya si kudai ukuu kwa ajili yake ama kwa ajili ya yale aliyofanya ama kwa ajili ya kizazi chake. Ninazisoma kweli hizo ili kumheshimu kwa ajili ya mfano wake wa imani na tuamini liliokuwa moyoni mwake.
Alikubali wito hii kwa sababu ya imani yake kwamba Kristo aliyefufuka na Baba yetu wa Mbinguni walikuwa wamemjia Joseph Smith katika kichaka cha miti katika jimbo la New York. Alizikubali kwa sababu alikuwa na imani kwamba funguo za ukuhani katika Kanisa la Bwana zilikuwa zimerejeshwa na uwezo wa kuunganisha familia milele, kama tu wangekuwa na imani ya kutosha kuweka maagano yao.
Kama Heinrich Eyring, babu yangu, huenda ukawa wa kwanza katika familia yako kuongoza njia kuelekea kwa uzima wa milele kwenye njia ya maagano matakatifu yaliyofanywa na kuwekwa kwa bidii na imani. Kila agano linaleta majukumu na ahadi. Kwa kila mmoja wetu, kama tu vile yalivyokuwa kwa Heinrich, majukumu hayo wakati mwingine huwa ni rahisi lakini mara nyingi huwa ni ngumu. Lakini kumbuka, majukumu lazima wakati mwingine yawe magumu kwa sababu malengo yao ni kutusongesha kwenye njia ya kuishi milele na Baba wa Mbinguni na Mwanawe Mpendwa, Yesu Kristo, katika familia.
Unakumbuka maneno kutoka kwa kitabu cha Ibrahimu:
“Na hapo akasimama mmoja miongoni mwao ambaye alifanana na Mungu, naye akasema kwa wale waliokuwa pamoja naye: Sisi tutakwenda chini, kwani kuna nafasi huko, nasi tutachukua vifaa hivi, nasi tutaifanya dunia mahali ambapo hawa watapata kukaa;
“Na tutawajaribu kwa njia hii, ili kuona kama wao watafanya mambo yote yale ambayo Bwana Mungu wao atawaamuru;
“Na wao ambao watatunza hali yao ya kwanza wataongezewa; na wao ambao hawatatunza hali yao ya kwanza hawatapata utukufu katika ufalme ule ule pamoja na wale walioitunza hali yao ya kwanza; nao wale watakaoitunza hali yao ya pili watapata kuongezewa utukufu juu ya vichwa vyao kwa milele na milele.”2
Kutunza hali yetu ya pili kunategemea kufanya kwetu maagano na Mungu na kwa imani kutekeleza majukumu ambayo yanatutarajia. Inahitaji imani katika Yesu Kristo kama Mwokozi wetu ili kuweka maagano takatifu kwa maisha yetu yote.
Kwa sababu Adamu na Hawa walianguka, kila mmoja wetu hupitia majaribio, mateso, na kifo. Hata hivyo, Baba yetu mpendwa wa Mbinguni alitupa karama ya Mwanawe Mpendwa, Yesu Kristo, kama Mwokozi wetu. Karama hiyo kuu na baraka ya Upatanisho wa Yesu Kristo huleta urithi kwa kila mtu: ahadi ya Ufufuo na uwezekano wa uzima wa milele kwa wote wazaliwao.
Baraka kuu ya zote za Mungu, uzima wa milele, itatujia tu tunapofanya maagano yanayowezeshwa katika Kaniza la kweli la Yesu Kristo na watumishi wake walio na mamlaka. Kwa sababu ya Kuanguka, sote tunahitaji matokeo ya kusafisha ya ubatizo na kuwekelewa mikono ili kupokea karama ya Roho Mtakatifu. Maagizo haya lazima yafanywe na wale ambao wana mamlaka sahihi ya ukuhani. Kisha, kwa usaidizi wa Nuru ya Kristo na Roho Mtakatifu, tunaweza kuweka maagano yote tunayofanya na Mungu, hasa yale ambayo yanatolewa katika mahekalu Yake. Ni kwa njia hii peke yake, na kwa usaidizi huo, yeyote anaweza kudai urithi wake wa haki kama mtoto wa Mungu katika familia milele.
Kwa baadhi wanaonisikiliza, hiyo inaweza kunekana kuwa ndoto isiyowezekana kabisa.
Mmewaona wazazi waaminifu wakihuzunika kwa ajili ya watoto wao ambao wamekataa ama ambao wamechagua kuvunja maagano yao na Mungu. Lakini wazazi hao wanaweza kupata faraja na tumaini kutoka kwa yale wazazi wengine wamepitia.
Wana wa Alma na wana wa Mfalme Mosia walitubu kutoka kwa uasi wao mkuu dhidi ya maagano na amri za Mungu. Alma Mdogo alimuona mwanawe Koriantoni akigeuka kutoka kwa kutenda dhambi mbaya sana hadi kwa utumishi wa imani. Kitabu cha Mormoni kinarekodi muujiza wa Walamani kuweka kando utamaduni wa kuchukia haki na kuahidi hadi kifo kudumisha amani.
Malaika alitumwa kwa Alma mdogo na wana wa Mosia. Malaika alikuja kwa sababu ya imani na maombi ya akina baba zao na ya watu wa Mungu. Kutoka kwa mifano hiyo ya uwezo wa Upatanisho kushawishi fikira na hisia za watu, mnaweza kupokea ujasiri na faraja.
Bwana ametupa vyanzo vyote vya tumaini tunapopambana kuwasaidia wale tunaowapenda kukubali urithi wao wa milele. Ametupa ahadi tunapozidi kujaribu kuwakusanya watu Kwake, hata wakati wanapinga aliko Lake kufanya hivyo. Kupinga kwao kunamhuzunisha, lakini kamwe hakomi, nasi hatupaswi kukoma. Anatoa mfano mkamilifu kwetu sisi na upendo Wake unaoendelea: “Na tena, mara ngapi ningemkusanya kama vile kuku hukusanya vifaranga wake chini ya mabawa yake, ndio, Ee ninyi watu wa nyumba ya Israeli, ambao mmeanguka; ndio, Ee ninyi mnaoishi Yerusalemu, kama vile wale ambao wameangamizwa; mara ngapi ningekuwa nimewakusanya kama vile kuku avikusanyavyo vifaranga vyake na hamnikubali.”3
Tunaweza kuegemea hamu hiyo isiyokwisha ya Mwokozi kumrudisha kila mmoja wa watoto wa kiroho wa Baba wa Mbinguni nyumbani kwao kuwa Naye. Kila mzazi, akina babu, na wahenga waaminifu wanashiriki katika hamu hii. Baba wa Mbinguni na Mwokozi ni mifano yetu kamilifu ya kile ambacho tunaweza kufanya na lazima tufanye. Kamwe hawatulazimishi kuchagua wema kwa sababu wema lazima uchaguliwe. Wao hufanya haki ili tuweze kutambua kile ambacho ni chema, na hutusaidia kuona kwamba furaha huja kutoka kwa kufanya chaguo njema.
Kila mtu azaliwaye duniani hupokea Mwanga wa Kristo, ambao hutusaidia kuona na kuhisi kile ambacho ni cha haki na kile ambacho ni kibaya. Mungu ametuma watumishi binadamu ambao wanaweza, kupitia Roho Mtakatifu, kutusaidia kutambua kile angetaka tufanye na kile ambacho amekataza. Mungu hufanya iwe ya kuvutia kuchagua haki kwa kuturuhusu kuhisi madhara ya uchaguzi wetu. Tukichagua haki, tutapata furaha---hatimaye. Tukichagua mabaya, kunakuja huzuni na majuto---hatimaye. Madhara hayo hakika yatakuja. Hata hivyo mara nyingi huchelewa kwa makusudi. Kama baraka zingekuja mara moja, kuchagua haki hakungejenga imani . Na kwa sababu huzuni pia wakati mwingine hucheleweshwa vikubwa, huchukua imani kuhisi haja ya kuomba msamaha kwa dhambi mapema badala ya baada ya kuhisi madhara yake na huzuni na uchungu.
Baba Lehi alihuzunika kwa sababu ya chaguo zilizofanywa na baadhi ya wanawe na familia zao. Alikuwa mtu mzuri sana na mwenye haki---nabii wa Mungu. Mara nyingi alishuhudia Mwokozi wetu, Yesu Kristo, kwao. Alikuwa mfano wa utii na utumishi wakati Bwana alimwita kuacha mali yake yote ya kidunia ili kuokoa familia yake kutokana na maangamizi. Mwishoni mwa maisha yake, alikuwa bado anawashuhudia watoto wake. Kama Mwokozi---na licha ya uwezo wake wa kubainisha mioyo yao na kuona siku za usoni za kusikitisha na za ajabu---Lehi aliendelea kusaidia familia yake ili kuwaleta kwa wokovu.
Hivi leo mamilioni ya watoto wa Baba Lehi wanatoa sababu ya tumaini lake kwa ajili yao.
Unaweza kufanya nini ili kujifunza kutoka kwa mfano wa Lehi? Tunaweza kujifunza kutoka kwa mfano wake kwa kusoma maandiko kwa maombi na kwa uchunguzi.
Napendekeza kwamba ufikirie kuhusu muda mfupi na muda mrefu unapojaribu kutoa urithi wa tumaini kwa familia yako. Katika muda mfupi, kutakuwa na matatizo, na Shetani atatumia nguvu zake kutujaribu. Na kuna vitu vya kusubiri kwa uvumilivu, kwa imani, mkijua ya kwamba Bwana hutenda kwa wakati Wake mwenyewe na katika njia Yake mwenyewe.
Kuna vitu unavyoweza kufanya mapema, wakati wale uwapendao ni wadogo. Kumbuka kwamba maombi ya familia ya kila siku, kujifunza maandiko kwa familia, na kushirikisha ushuhuda wetu katika mkutano wa sakramenti ni rahisi na ina athari zaidi wakati watoto ni wadogo. Watoto wadogo mara nyingi huwa na mvutio zaidi kwa Roho kuliko vile tunavyotambua.
Wakati wamekuwa kiasi, watakumbuka nyimbo walizoimba pamoja na wewe. Hata zaidi ya kukumbuka muziki, watakumbuka maneno ya maandiko na ushuhuda. Roho Mtakatifu anaweza kuleta mambo yote kwa kumkumbuka kwao, lakini maneno ya maandiko na nyimbo zitakumbukwa kwa muda mrefu zaidi. Kumbukumbu hizo zitawashawishi kurudi wanapotanga kwa muda, pengine kwa miaka, kutoka kwa njia inayoelekeza nyumbani kwa uzima wa milele.
Tutahitaji kufikiria juu ya muda mrefu wakati wale tunaowapenda wanahisi ushawishi wa dunia na wingu la shaka likionekana kushinda imani yao. Tuna imani tumaini na hisani kutuongoza na kuwapa nguvu.
Mimi nimeshaona kwamba kama mshauri wa manabii wawili wa Mungu. Wao ni watu wenye haiba za kipekee. Hata hivyo wanaonekana kushiriki matumaini thabiti. Mtu akileta tahadhari kuhusu kitu katika Kanisa, majibu yao ya kila mara ni “Ee, mambo yatakuwa sawa.” Wao hujua zaidi kuhusu tatizo hilo kwa kiwango kikubwa kuliko watu wanaoleta jambo hilo.
Pia wanajua jinsi Bwana hufanya vitu, na hivyo wao daima huwa na matumaini kuhusu ufalme Wake. Wanajua Yeye ndiye kiongozi. Ana nguvu zote na anajali. Ukimkubali awe kiongozi wa familia yako, mambo yatakuwa sawa.
Baadhi ya wajukuu wa Heinrich Eyring hawajafuata njia ya wema. Lakini wengi wa wajukuu wake huenda mahekaluni ya Mungu saa 12:00 asubuhi kuwafanyia maagizo mababu ambao hawajawahi kukutana nao kamwe. Wao huenda kwa sababu ya urithi wa tumaini aliloacha. Aliacha urithi ambao unadaiwa na wengi wa kizazi chake.
Baada ya yote tunayoweza kufanya katika imani, Bwana atahalalisha matumaini yetu kwa baraka kubwa zaidi kwa ajili ya familia zetu kuliko tunavyoweza kufikiria. Anataka mazuri kwa ajili yao na kwa ajili yetu, kama watoto Wake.
Sisi sote ni watoto wa Mungu aliye hai. Yesu wa Nazareti ni Mwanawe Mpendwa na Mwokozi wetu aliyefufuka. Hili ni Kanisa Lake. Ndani yake kuna funguo za ukuhani, na hivyo basi familia zinaweza kuwa milele. Huu ni urithi wetu wa tumaini wa dhamani mno. Nashuhudia kwamba ni kweli katika jina la Bwana Yesu Kristo, amina.