Kukua kwa Kanisa la Kristo
Hii ni sura ya 8 ya simulizi ya historia ya juzuu nne mpya ya Kanisa yenye kichwa cha habari Watakatifu: Hadithi ya Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Kitabu hiki kinapatikana katika lugha 14 zilizochapishwa, katika sehemu ya Historia ya Kanisa ya programu ya Gospel Library, na mtandaoni kwenye saints.lds.org. Sura za nyuma zilichapishwa katika matoleo yaliyopita na zinapatikana katika lugha 47 katika programu ya Gospel Library na katika saints.lds.org.
Mapema Julai 1828, akiwa na muswada mkononi, Joseph alijua ya kwamba Bwana alimtaka achapishe Kitabu cha Mormoni na kueneza ujumbe wake kwa marefu na mapana. Lakini biashara ya uchapishaji haikuwa ikijulikana kwake pamoja na familia yake. Alihitaji kuuweka muswada salama, kupata mpiga chapa, na kwa njia fulani kuwapa kitabu watu ambao walikuwa radhi kuzingatia uwezekano wa kuwepo kwa maandiko mapya.
Kuchapisha kitabu kikubwa kama Kitabu cha Mormoni pia haingegharimu pesa kidogo. Hali ya kifedha ya Joseph haikuwa imeimarika tangu alipoanza kufanya tafsiri hiyo, na pesa zote alizopata zilitumika kwa kuikimu familia yake. Hiyo pia ilikuwa hali kwa wazazi wake, ambao walikuwa wakulima masikini waliofanya kazi katika shamba ambalo hawakulimiliki. Rafiki pekee wa Joseph ambaye angeweza kutoa fedha kwa ajili ya mradi huo alikuwa ni Martin Harris.
Joseph alianza kufanya kazi kwa haraka. Kabla ya kumaliza tafsiri, alikuwa amesajili kwa ajili ya haki miliki ya kitabu hicho ili kulinda maandishi dhidi ya mtu yeyote ambaye angeweza kuiba maandishi ya kitabu hicho.1 Kwa usaidizi wa Martin, Joseph pia alianza kumtafuta mpiga chapa ambaye angekubali kuchapisha kitabu hicho.
Kwanza walimwendea Egbert Grandin, mpiga chapa kutoka Palmyra ambaye alikuwa na umri sawa na Joseph. Grandin aliukataa mradi huo mara moja, akiamini kitabu hicho hakikuwa cha kweli. Pasikukata tamaa, Joseph na Martin waliendelea kutafuta na kumpata mpiga chapa aliyekuwa radhi kupiga chapa katika mji uliokuwa karibu. Lakini kabla ya kukubali kuweka ahadi, walirudi Palmyra na kumuuliza Grandin kwa mara nyingine tena ikiwa alitaka kukichapisha kile kitabu.2
Wakati huu, Grandin alionekana kuwa tayari kuutekeleza mradi huu, lakini alitaka alipwe $3,000 kupiga chapa na kujalidi nakala elfu tano kabla hata ya kuanza kazi. Martin tayari alikuwa ameahidi kutoa msaada kwa kulipia uchapishaji huo, lakini kupata fedha hizo, aligundua kwamba angehitaji kuweka rehani shamba lake. Ilikuwa ni mzigo mkubwa kwa Martin, lakini alijua hakuna yeyote miongoni mwa marafiki wa Joseph ambaye angeweza kumsaidia kwa fedha hizo.
Akiwa ametaabika, Martin alianza kuwa na wasi wasi kuhusu busara ya kutoa fedha kwa ajili ya Kitabu cha Mormoni. Alikuwa na mojawapo ya mashamba mazuri zaidi katika eneo hilo. Kama angeliweka rehani shamba lake, alikuwa katika hatari ya kulipoteza. Utajiri ambao ulikuwa umemchukua maisha yake yote kuupata ungeweza kupotea mara moja ikiwa Kitabu cha Mormoni hakingeuzwa kwa wingi.
Martin alimwelezea Joseph wasi wasi wake na kumuomba atafute ufunuo kwa niaba yake. Katika kujibu, Mwokozi Alizungumzia dhabihu Yake ya kufanya mapenzi ya Baba Yake, bila ya kujali gharama. Alielezea mateso Yake ya mwisho alipokuwa akilipa gharama ya dhambi ili wote waweze kutubu na kusamehewa. Kisha Alimuamuru Martin aweke kando maslahi yake ili kufanikisha mpango wa Mungu.
“Usitamani mali yako mwenyewe,” Bwana alisema, “bali itoe bure kwa uchapishaji wa Kitabu cha Mormoni.” Kitabu kilikuwa na neno la kweli la Mungu, Bwana alimhakikishia Martin, na kitakuwa na manufaa kwa wengine kuamini injili.3
Ingawaje majirani zake hawangeelewa uamuzi wake, Martin alimtii Bwana na kuweka rehani shamba lake ili kudhamini malipo.4
Grandin alisaini mkataba na akaanza kufanya mipango ya mradi huu mkubwa.5 Joseph alikuwa ametafsiri maandishi ya Kitabu cha Mormoni katika muda wa miezi mitatu, akisaidiwa na mwandishi mmoja kwa wakati. Ingewachukua Grandin na wanaume dazeni miezi saba kupiga chapa na kujalidi nakala za kwanza za kazi hii yenye kurasa 590.6
Huku mpiga chapa akiwa ameajiriwa, Joseph alirudi kule Harmony Oktoba ya 1829 kufanya kazi shambani mwake na kuwa pamoja na Emma. Oliver, Martin, na Hyrum, kwa sasa, wangesimamia uchapishaji na kumtumia Joseph ripoti za mara kwa mara kuhusu maendeleo ya Grandin.7
Akikumbuka jinsi alivyohisi kufa moyo baada ya kupoteza kurasa za kwanza alizokuwa ametafsiri, Joseph alimwambia Oliver anakili muswada wa Kitabu cha Mormoni ukurasa baada ya ukurasa, na kutengeneza nakala ya kupelekwa kuchapishwa ili vituo vya uandishi viweze kuongezwa na chapa kuandaliwa.8
Oliver alifurahia kunakili kile kitabu, na barua alizoandika wakati huo zilikuwa zimejawa na lugha yake. Akirudia maneno ya Nefi, Yakobo, na Amuleki kutoka kwenye Kitabu cha Mormoni, Oliver alimuandikia Joseph kuhusu shukrani zake kwa ajili ya Upatanisho wa Kristo usio na kikomo.
“Ninapoanza kuandika kuhusu rehema za Mungu,” alimwambia Joseph, “Sijui wakati wa kumaliza, lakini muda na karatasi vinaniishia.”9
Roho sawa na hiyo iliwavutia wengine kwenye Kitabu cha Mormoni wakati kilipokuwa kikichapishwa. Thomas Marsh, mwanafunzi wa awali wa ufundi wa kupiga chapa, alikuwa amejaribu kutafuta nafasi yake katika makanisa mengine, lakini hakuna lolote lililohubiri injili aliyoipata katika Biblia. Aliamini kwamba karibuni kungetokea kanisa jipya ambalo lingefundisha ukweli uliorejeshwa.
Wakati wa majira hayo ya joto, Thomas alihisi kuongozwa na Roho kusafiri mamia ya maili mbali na nyumbani kwake kule Boston kuelekea magharibi mwa New York. Aliishi katika eneo hilo kwa muda wa miezi mitatu kabla ya kuelekea nyumbani, bila uhakika ni kwa nini alikuwa amesafiri mbali kiasi hicho. Katika kituo cha mapumziko njiani akirudi, hata hivyo, mwenyeji wake alimuuliza kama alikuwa amesikia kuhusu “kitabu cha dhahabu” cha Joseph Smith. Thomas alimwelezea mwanamke yule bado hakuwa amesikia na akahisi kuvutiwa sana kujifunza zaidi.
Alimwambia azungumze na Martin Harris na kumuelekeza Palmyra. Thomas alienda huko mara moja na kumkuta Martin katika duka la kupiga chapa la Grandin. Mpiga chapa alimpa kurasa kumi na sita za Kitabu cha Mormoni, na Thomas akazichukua na kwenda nazo Boston, akiwa na hamu ya kushiriki kionjo cha kwanza cha imani hii mpya na mkewe, Elizabeth.
Elizabeth alisoma kurasa hizo, naye pia akaamini zilikuwa kazi ya Mungu.10
Majira hayo ya majani kupukutika, wapiga chapa walipokuwa wamefikia maendeleo imara kwenye Kitabu cha Mormoni, hakimu wa awali kwa jina Abner Cole alianza kuchapisha gazeti kwenye duka la chapa la Grandin. Akifanya kazi dukani usiku, baada ya wafanyakazi wa Grandin kwenda nyumbani, Abner aliweza kuziona kurasa zilizochapishwa kutoka kwenye Kitabu cha Mormoni, ambacho kilikuwa bado hakijajalidiwa au tayari kwa kuuzwa.
Punde Abner alianza kuifanyia mzaha “Biblia ya Dhahabu” katika gazeti lake, na wakati wa majira ya baridi alichapisha dondoo kutoka kwenye kitabu hicho pamoja na maoni ya dhihaka.11
Wakati Hyrum na Oliver walipojua kuhusu kile Abner alikuwa akikifanya, walikabiliana naye. “Una haki gani kuchapisha Kitabu cha Mormoni katika njia hii?” Hyrum aliuliza. “Je, haujui ya kwamba tumepokea haki miliki?”
“Haikuhusu,” Abner alisema. “Nimekodisha chapa na nitachapisha kile ninachotaka.”
“Ninakukataza kuchapisha zaidi ya kitabu hicho katika gazeti lako,” Hyrum alisema.
“Sijali,” Abner alisema.
Bila kuwa na uhakika nini cha kufanya, Hyrum na Oliver walituma ujumbe kwa Joseph kule Harmony, ambaye alirudi Palmyra mara moja. Alimkuta Abner katika ofisi ya kupiga chapa, akisoma gazeti lake kijuujuu.
“Unaonekana kufanya kazi kwa bidii,” Joseph alisema.
“Unaendeleaje, Bwana Smith,” Abner alijibu kwa kejeli.
“Bwana Cole,” Joseph alisema, “Kitabu cha Mormoni na haki za kukichapisha ni yangu, na ninakukataza usiingilie kazi hiyo.”
Abner alivua koti lake na kuikunja mikono ya shati lake. “Je, unataka kupigana, bwana?” alifoka, akitwanga ngumi zake pamoja. “Ikiwa unataka kupigana, njoo tu.”
Joseph alitabasamu. “Ni vema uvae koti lako,” alisema. “Kuna baridi, na sitapigana nawe.” Aliendelea kwa upole, “Lakini ni lazima ukome kuchapisha kitabu changu.”
“Kama unafikiri wewe ndiye mwanaume bora zaidi,” Abner alisema, “livue tu koti lako na ujaribu.”
“Kuna sheria,” Joseph alijibu, “na utajua hili kama haukulijua hapo awali. Lakini sitapigana nawe, kwa maana hakutakuwa na manufaa yoyote.”
Abner alijua alikuwa upande uliokuwa kinyume na sheria. Alitulia na akasitisha kuchapisha dondoo kutoka Kitabu cha Mormoni katika gazeti lake.12
Solomon Chamberlin, mhubiri aliyekuwa njiani akielekea Kanada, kwa mara ya kwanza alisikia kuhusu “Biblia ya Dhahabu” kutoka kwa familia iliyokuwa imempa mahali pa kulala karibu na Palmyra. Kama Thomas Marsh, alikuwa amehama kutoka kanisa moja hadi lingine maishani mwake lakini alihisi kutotosheka na yale aliyoona. Baadhi ya makanisa yalihubiri kanuni za injili na kuamini katika karama za kiroho, lakini hayakuwa na manabii wa Mungu au ukuhani Wake. Solomon alihisi kwamba wakati ulikuwa unakaribia ambapo Bwana angeleta Kanisa Lake.
Solomon akiwa anasikiliza familia hiyo ikizungumzia kuhusu Joseph Smith na mabamba ya dhahabu, alihisi kama shoti ya umeme kutoka kichwani hadi vidole vya miguuni, na alinuia kuitafuta familia ya Smith na kujifunza zaidi kuhusu kitabu hicho.
Aliondoka kwenda nyumbani kwa Smith na kukutana na Hyrum mlangoni. “Amani iwe kwenye nyumba hii,” Solomon alisema.
“Natumai itakuwa amani,” Hyrum alijibu.
“Kuna mtu mahali hapa,” Solomon aliuliza, “ambaye anaamini katika maono na ufunuo?”
“Ndio,” Hyrum alisema, “sisi ni nyumba ya maono.”
Solomon alimwelezea Hyrum kuhusu ono alilokuwa ameliona miaka kadhaa iliyopita. Katika ono hilo, malaika alikuwa amesema kwamba Mungu hakuwa na kanisa duniani lakini karibuni angeanzisha moja ambalo lilikuwa na nguvu kama kanisa la kale la mitume. Hyrum na wengine waliokuwa katika nyumba walielewa kile ambacho Solomon alisema na wakamwambia kwamba wao pia walikuwa na imani kama yake.
“Natamani ungefichua baadhi ya utambuzi wako,” Solomon alisema. “Nafikiri naweza kuuhimili.”
Hyrum alimualika kukaa katika shamba la Smith kama mgeni na akamuonyesha muswada wa Kitabu cha Mormoni. Solomon alikisoma kwa muda wa Siku mbili na kwenda pamoja na Hyrum hadi ofisi ya kupiga chapa ya Grandin, ambapo mpiga chapa alimpa kurasa sitini na nne zilizopigwa chapa. Akiwa na kurasa mkononi ambazo zilikuwa hazijajalidiwa, Solomon aliendelea hadi Kanada, akihubiri kila alichokijua kuhusu hii imani mpya safarini.13
Kufikia Machi 26, 1830, nakala za kwanza za Kitabu cha Mormoni zilikuwa zimejalidiwa na tayari kwa kuuzwa kwenye orofa ya chini ya ofisi ya kupiga chapa ya Grandin. Zilikuwa zimejalidiwa na kubanwa kwa ngozi ya ndama yenye rangi ya kahawia na zilikuwa na harufu ya ngozi na gundi, karatasi na wino. Maneno Kitabu cha Mormoni yalionekana mgongoni katika herufi za rangi ya dhahabu.14
Lucy Smith alithamini maandiko haya mapya na kuyaona kama ishara kwamba Mungu karibuni angewakusanya watoto Wake na kurejesha agano Lake la kale. Ukurasa wa jina ulitangaza kwamba lengo la kitabu hiki lilikuwa ni kuonyesha vitu vikubwa ambavyo Mungu alikuwa amewatendea watu Wake katika siku za nyuma, kuzitoa baraka sawa na hizo kwa watu Wake leo hii, na kuushawishi ulimwengu wote kwamba Yesu Kristo alikuwa Mwokozi wa ulimwengu.15
Katika upande wa nyuma wa kitabu kulikuwa na Ushahidi wa Mashahidi Watatu na Mashahidi Wanane, wakiuelezea ulimwengu kwamba walikuwa wameyaona yale mabamba na tafsiri yake ilikuwa ya kweli.16
Licha ya shuhuda hizi, Lucy alijua ya kwamba watu wengine walifikiri ya kwamba kitabu hiki kilikuwa cha ubunifu. Wengi wa majirani zake walidhani kwamba Biblia ilikuwa maandiko ya kutosha kwao, wakishindwa kutambua ya kwamba Mungu alikuwa ameyabariki mataifa zaidi ya moja kwa neno Lake. Pia alijua ya kwamba watu wengine walikataa ujumbe wake kwa sababu waliamini Mungu alikuwa amenena mara moja kwa ulimwengu na hangenena tena.
Kwa sababu hizi na zingine, watu wengi kule Palmyra hawakununua kile kitabu.17 Lakini wengine walijifunza kurasa zake, wakahisi nguvu za mafundisho yake, na wakapiga magoti kumuuliza Mungu ikiwa kilikuwa cha kweli. Lucy mwenyewe alijua Kitabu cha Mormoni kilikuwa neno la Mungu na alitaka kushiriki na wengine.18
Karibu punde tu baada ya Kitabu cha Mormoni kuchapishwa, Joseph na Oliver walijiandaa kuunda kanisa la Yesu Kristo. Miaka kadhaa kabla ya hapo, mitume wa kale wa Bwana Petro, Yakobo, na Yohana walikuwa wamewatokea na kuwatunukia Ukuhani wa Melkizedeki, kama Yohana Mbatizaji alivyokuwa ameahidi. Mamlaka haya ya nyongeza yaliwawezesha Joseph na Oliver kutunuku kipawa cha Roho Mtakatifu kwa wale waliowabatiza. Petro, Yakobo, na Yohana pia walikuwa wamewatawaza kuwa mitume wa Yesu Kristo.19
Karibu na wakati huo, wakiwa wanaishi nyumbani kwa Whitmer, Joseph na Oliver walikuwa wamesali kwa ajili ya ufahamu zaidi kuhusu mamlaka haya. Katika kujibu, sauti ya Bwana iliwaamuru watawazane kila mmoja kama wazee wa kanisa, lakini wasifanye hivyo kabla ya waaminio kuridhia kuwafuata kama viongozi katika kanisa la Mwokozi. Pia waliambiwa wawatawaze maafisa wengine wa kanisa na kuwatunuku kipawa cha Roho Mtakatifu kwa wale ambao walikuwa wamebatizwa.20
Mnamo Aprili 6, 1830 Joseph na Oliver walikutana nyumbani kwa Whitmer kutimiza amri ya Bwana na kuunda Kanisa Lake. Ili kutimiza matakwa ya sheria, walichagua watu sita wawe washiriki wa kwanza wa kanisa hili jipya. Karibu wanawake na wanaume arobaini pia walijaa ndani na kuzunguka ile nyumba ndogo kushuhudia tukio hilo.21
Kwa kutii maagizo ya awali ya Bwana, Joseph na Oliver waliomba mkusanyiko huo wa watu kuwakubali kama viongozi katika ufalme wa Mungu na kuonyesha ikiwa waliamini ilikuwa sawa kwao kuanzisha kanisa. Kila mshiriki wa mkusanyiko aliridhia, na Joseph akaweka mikono yake juu ya kichwa cha Oliver na kumtawaza kama mzee wa kanisa. Kisha wakabadilishana nafasi, na Oliver akamtawaza Joseph.
Baadae, walitoa mkate na divai ya sakrameti kwa ukumbusho wa Upatanisho wa Kristo. Kisha waliweka mikono juu ya wale waliokuwa wamewabatiza, kuwathibitisha kama waumini wa kanisa na kuwapa kipawa cha Roho Mtakatifu.22 Roho wa Bwana alishushwa juu ya wale waliokuwa katika mkutano ule, na baadhi katika mkusanyiko walianza kutoa unabii. Wengine walimsifu Bwana, na wote walifurahia pamoja.
Joseph pia alipokea ufunuo wa kwanza uliolenga muundo mzima wa kanisa hili jipya. “Tazama, pawepo na kumbukumbu itakayotunzwa miongoni mwenu,” Bwana aliamuru, akiwakumbusha watu Wake kwamba walipaswa kuandika historia yao takatifu, wakihifadhi historia ya matendo yao na kushuhudia wajibu wa Joseph kama nabii, mwonaji, na mfunuzi.
“Yeye nimemwongoza kuendesha kusudi la Sayuni katika uweza mwingi kwa ajili ya mema,” Bwana alitangaza. “Kwani neno lake mtalipokea, kama vile linatoka kinywani mwangu, katika uvumilivu wote na imani yote. Kwani kwa kufanya mambo haya milango ya jahanamu haitawashinda.”23
Baadae, Joseph alisimama pembeni mwa kijito na kushuhudia ubatizo wa mama na baba yake katika kanisa. Baada ya miaka mingi ya kuchagua njia tofauti katika kutafuta kwao ukweli, hatimaye waliungana katika imani. Baba yake alipokuwa anatoka majini, Joseph alimshika kwa mkono, akamsaidia kufika ukingoni, na kumkumbatia.
“Mungu Wangu,” alilia, na kufunika uso wake kifuani mwa baba yake, “Nimejaliwa kuishi na kumuona baba yangu akibatizwa katika kanisa la kweli la Yesu Kristo!”24
Jioni hiyo, Joseph alikwenda katika kijisitu kilichokuwa karibu, moyo wake ukiwa umejaa hisia. Alitaka kuwa peke yake, mbali na marafiki na familia. Katika kipindi cha miaka kumi tangu Ono lake la Kwanza, alikuwa ameshuhudia mbingu zikifunguka, akahisi Roho wa Mungu, na kufunzwa na malaika. Alikuwa pia ametenda dhambi na kupoteza kipawa chake, akatubu, akapokea rehema ya Mungu, na kutafsiri Kitabu cha Mormoni kwa Uwezo na neema Yake.
Sasa Yesu Kristo alikuwa amerejesha kanisa Lake na kumwidhinisha Joseph na ukuhani ule ule ambao mitume walikuwa nao katika siku za kale walipoieneza injili duniani.25 Furaha aliyohisi ilikuwa nyingi kupindukia, na wakati Joseph Knight na Oliver walipomuona baadae usiku huo, alikuwa akilia.
Shangwe yake ilikuwa timilifu. Kazi ilikuwa imeanza.26