Mayai, Fyuzi, na Imani
Alvaro Alcaino
Antofagasta, Chile
Moja kati ya malengo yetu kama familia ni kuweka akiba fedha za kutosha ili kulipia kiasi cha awali cha nyumba yetu. Bila lengo hilo, ningeweza kupoteza siku zangu za mwisho wa wiki nikiangalia runinga, nikisubiri fursa za kupata fedha zinijie.
Kama dereva wa kampuni ya uchimbaji madini kaskazini mwa Chile, nilifanya kazi kwa siku nne mbali na nyumbani kwenye migodi na kisha nilikuwa na siku tatu za kupumzika—Jumamosi mpaka Jumatatu. Ili kuongezea katika kipato chetu na akiba kwetu fedha kwa ajili ya nyumba, tuliamua kuanza kuuza mayai. Lengo letu lilikuwa kuchukua maagizo kutoka kwa rafiki zetu, majirani, na waumini wa Kanisa; tukinunuliwa karibu mayai 1,000 kila wiki kutoka kwa muuzaji wa jumla; na kisha kuchukua na kuyasambaza siku za Jumamosi na Jumatatu.
Mimi pamoja na mke wangu, Laura, tuliamua tungewachukua watoto wetu wawili pamoja nasi katika usambazaji na kufurahia muda kwa pamoja. Wakati tulipokuwa njiani kununua mzigo wetu wa kwanza wa mayai, hata hivyo, maafa yalitokea. Mmoja wa watoto wetu, akichezea kichongeo kidogo cha penseli cha chuma, alikirusha na kikatua mraba kwenye kiwashio pokezi cha sigara kilichokuwa wazi. Cheche ziliruka, na gari letu likapoteza umeme na kusimama katikati ya barabara. Fyuzi ilikuwa imeungua.
Wakati tukiwa tumesimama pale tukisababisha foleni na kushangaa tutafanya nini, tuliudhika sana mpaka tukahisi kama tutalia. Lakini kwa wakati huo, nilikumbuka kwamba Bwana aliahidi kutuinua na kutusaidia kama tutaweka tumaini letu Kwake. Utulivu ulinijia. Nilitambua nisingeweza kukaa tu pale na kunung’unika. Tulikuwa na tatizo, na kwa msaada wa Mungu, tungeweza kulitatua.
Mimi pamoja na Laura tuligeukiana na kusema “Tunahitaji kuonyesha imani.” Tukasali na kufuta machozi yetu. Kisha, laura akiwa kwenye usukani wa gari, nilishuka na kulisukuma. Baadhi ya watu walishuka kwenye magari yao na kunisaidia.
Tulisukuma gari kwa umbali wa takribani mita 200 kabla ya kupata mahali salama pa kuliegesha pembeni ya barabara. Wakati gari likisimama, niligundua kwamba tulikuwa tumeliegesha mbele ya duka la vifaa vya muziki vya magari.
Nilichukua fyuzi iliyoungua, nikaenda dukani, na kuuliza, “Je, mnayo kama hii?”
Muuzaji akajibu, “Bila shaka.”
Nilinunua fyuzi na kuiweka katika sehemu yake, gari liliwaka mara moja na tukaondoka. Muuzaji wa jumla wa mayai alikuwa karibu kufunga wakati tulipofika. Tulinunua mayai yetu na kuyasambaza.
Tunapokuwa na changamoto, tunatakiwa kukumbuka kumwomba msaada Baba yetu wa Mbinguni. Najua atatujibu tunaposonga mbele na kuonyesha imani yetu Kwake.