Kanuni za Kuhudumu
Kupata Msaada ili Kuwasaidia Wengine
Ni kwa namna gani tunawahusisha wengine wakati tunapohitaji msaada katika juhudi zetu za kuhudumia? Shiriki katika usaili wa kuhudumu na mikutano ya baraza la Jumapili ya kwanza.
Wakati Kathy alipolazimika kuwa kwenye kiti cha walemavu kutokana na ugonjwa wa seli za mishipa ya fahamu ya uti wa mgongo na ubongo, alijikuta akihitaji msaada kila usiku kutoka kwenye kiti chake kwenda kitandani. Kazi hii ilikuwa kubwa sana kwa mwanafamilia yoyote. Kwa hiyo akidi ya wazee ilishauriana kuhusu hali yake na kuamua kuunda ratiba kumsaidia kila jioni.1
Tunapokuja kujua mahitaji na uwezo wa wale tunaowahudumia, tunaweza kukuta kwamba tunahitaji msaada ili kuweza kutimiza mahitaji yao. Usaili wa kuhudumu na mkutano wa baraza wa Jumapili ya kwanza ni fursa mbili za kujadiliana ni namna ipi inayofaa ya kuwahusisha wengine.
Usaili wa Kuhudumu
Usaili huu wa robo ya mwaka kati ya dada wanaohudumu na urais wa Muungano wa Usaidizi wa akina Mama au kati ya akina kaka wanaohudumu na urais wa akidi ya wazee ni ripoti rasmi pekee tunayotoa kuhusu wale tunaowahudumia. Usaili ni fursa angalau kila robo ya mwaka ili (1) kushauriana kuhusu uwezo, mahitaji, na changamoto za familia na watu binafsi tunaowahudumia; (2) kuamua ni mahitaji gani akidi, Muungano wa Usaidizi wa akina Mama, au baraza la kata wanaweza kusaidia; na (3) kujifunza kutoka kwa viongozi na kutiwa moyo katika juhudi za kuhudimia.
Rais wa akidi ya wazee na wa Muungano wa Usaidizi wa akina Mama huwasilisha mahitaji maalum moja kwa moja kwa askofu na watapokea ushauri na mwongozo kutoka kwake.
Unaweza kupata taarifa zaidi kuhusu usaili wa kuhudumu katika ministering.lds.org.
Kufanya Usaili wa Kuhudumu Kuwa Wenye Tija
Katika kuunga mkono kauli ya Rais Russell M. Nelson kwamba programu ya kuhudumia itakuwa ni bawaba ambayo kwayo nia ya Kanisa itashikizwa, Mzee Gary E. Stevenson wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili alifundisha, “Utambuzi wa ono lake … unaweza kutabiriwa kwa kuangalia ni kwa namna gani kina kaka na dada wanaohudumu wanafundishwa na kuhusishwa katika usaili wa uhudumu.”2
Dondoo nne kwa ajili ya akina kaka na dada wanaohudumu:
-
Nenda kwenye usaili ukitafuta ushauri. Kuwa tayari kujifunza.
-
Kuwa tayari kujadili mahitaji ambayo unahitaji msaada kuyatimiza.
-
Zingatia kwenye nguvu na uwezo wa mtu, si tu mahitaji.
-
Wasiliana na urais kwa ajili ya kushauriana katikati ya usaili wa robo ya mwaka kama itakavyohitajika.
Dondoo tano kwa ajili ya viongozi:
-
Usaili hauhitaji kuwa mrefu, lakini panga muda wa kutosha wa kukutana mahali ambapo panaruhusu mazungumzo yenye tija.
-
Chukua fursa ya kuwahudumia akina kaka na dada wanaohudumu.
-
Usiulize maswali ambayo yanatoa ishara kwamba unahesabu matembezi au kuangalia waliotembelewa (“Je, uliweza kutimiza kuhudumu kwako?”). Usiulize maswali ambayo yanatilia mkazo tabia pendwa (“Ni msukumo gani umeupata wakati ukisali kwa ajili ya familia? Nini kilitokea wakati ulipofanyia kazi misukumo hiyo?).
-
Kwa moyo wa dhati sikiliza na andika maelezo.
-
Shaurianeni kwa pamoja. Wenza katika kuhudumu wana dhamana ya kupokea ufunuo kwa ajili ya wale waliopewa kuwahudumia.
Maswali na Majibu kuhusu Usaili wa Kuhudumu
Usaili wa kuhudumu ni nini?
Ni majadiliano kati ya kina kaka wanaohudumu na mshiriki wa urais wa akidi ya wazee au kati ya kina dada wanaohudumu na mshiriki wa urais wa Muungano wa Usaidizi wa akina Mama katika mazingira ambayo yanawaruhusu kutafuta na kupokea mwongozo wa kiungu kutoka kwa Roho Mtakatifu. Kama matokeo, kina kaka na kina dada wanaohudumu wanaweza kupokea mwongozo wa kiungu wa kuangalia, kupenda, kufundisha, na kufariji katika njia ya Mwokozi.
Je, usaili huu wa robo ya mwaka unahitaji kuwa wa uso kwa uso?
Kawaida hufanyika uso kwa uso, lakini huweza pia kufanyika kwa njia ya simu au kwenye mtandao wakati ambapo kukutana uso kwa uso haiwezekani. Kiujumla, wenza wote wawili wangeshiriki katika usaili inapowezekana.
Dhumuni la usaili wa kuhudumu ni lipi?
Usaili wa kuhudumu ni fursa kwa akina kaka na dada wanaohudumu kupitia hali za sasa, kuweka mipango ya baadae, na kupata msaada unaohitajika kwa familia au mtu binafsi waliyepewa kumhudumia. Ni nafasi ya kuzungumza kuhusu rasilimali zipi akidi na Muungano wa Usaidizi wa akina Mama wanaweza kutoa.
Je, ninashughulikia vipi taarifa ya siri na masuala nyeti?
Akina kaka na dada wanaohudumu hushiriki taarifa ya siri na rais wa akidi ya wazee au rais wa Muungano wa Usaidizi wa akina Mama pekee—au moja kwa moja na askofu. Kushiriki taarifa ya siri au nyeti hakupaswi kufanyika kwenye mikutano ya baraza ya Jumapili ya kwanza.
Mikutano ya Baraza ya Jumapili ya Kwanza
Katika kuongezea kwenye usaili wa uhudumu, mikutano baraza ya Jumapili ya kwanza ni njia nyingine ya kuwahusisha wengine katika kuhudumia. Katika mikutano ya Muungano wa Usaidizi wa akina Mama na akidi ya wazee mwongozo wa kiungu unaweza kuja kwa wale wanaohudhuria kupitia Roho na kutoka kwa wengine kwenye kikundi.
Dhumuni la mkutano wa baraza ni:
-
“Kushauriana kwa pamoja kuhusu majukumu, fursa, na changamoto za eneo husika;
-
“Kujifunza kutoka kwenye umaizi na uzoefu wa kila mmoja wetu; na
-
“Kupanga njia za kutendea kazi mawazo yaliyopokelewa kutoka kwa Roho.”3
Mikutano ya baraza ni zaidi ya majadiliano tu: mikutano hutupeleka katika kutenda kama watu binafsi na kama kikundi kama ilivyoshawishiwa na Roho. Washiriki wanaweza kuhisi hamu ya kutimiza kazi ya Bwana kama matokeo ya mikutano hii.
Mwaliko wa Kutenda
“Sala yetu leo,” alisema Mzee Jeffrey R. Holland wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, “ni kwamba kila mwanaume na mwanamke—na vijana wetu wakubwa wa kiume na wa kike—[wata] kuwa na msimamo zaidi katika kujaliana kwa moyo wa dhati, wakihamasishwa tu na upendo msafi wa Kristo katika kufanya hivyo.”4