Mzee Gerrit W. Gong: Mpende Bwana na Mwamini Yeye
Kama mwanafunzi mzamili aliyeoa karibuni akiwa katika Chuo Kikuu cha Oxford Uingereza, Gerrit W. Gong alijifunza kupitia uzoefu binafsi kwamba wakati tunapompenda Bwana na kumwamini Yeye, Atatusaidia, atatuongoza, na kutuimarisha.
Gerrit alikuwa ni Msomi wa Rhodes akifanya juhudi kumaliza shahada mbili za uzamili, mojawapo ikiwa ni ya shahada ya udaktari. Wakati huohuo, alikuwa akihudumu katika uaskofu wa Kata ya Oxford. Yeye pamoja na mke wake, Susan, walikumbuka ushauri ambao Mzee David B. Haight (1906–2004) wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili aliutoa alipofungishani ndoa yao katika Hekalu la Salt Lake. “Alituambia tuwe na wito mara zote,” Mzee Gong anasema. “Tulijua kama tungemwamini Mungu na kufanya kadiri tuwezavyo, angetusaidia.”
Gerrit pamoja na Susan walipokea “msaada wa kiungu na rehema uroro,” anasema. Wakati akiendelea kutumikia katika uaskofu, Gerrit alikamilisha mahitaji yote ya kielimu ya shahada ya udaktari, isipokuwa tasnifu yake. Alimuomba askofu wa Kata ya Oxford, Alan Webster, baraka ya ukuhani. Katika baraka, Gerrit alipokea ahadi hii: “Endelea kufanya kila uwezacho, na Bwana atakubariki.”
Waumini wawili wa kata waliokuwa na uzoefu wa ukatibu muhtasi walijitolea kumsaidia kuchapa mswada wake, na Gerrit aliweza kukamilisha tasnifu yake katika miezi michache. Hakika, aliweza kumaliza vyote shahada ya uzamili na udaktari katika miaka mitatu tu. Wakati wa mahafali ya kuhitimu pia alikubali ajira katika kitengo cha utafiti katika chuo kikuu. Uzoefu wake huko Oxford uliimarisha kuamini kwake katika Bwana, kuamini ambako kunaendelea hadi leo hii na kutaendelea kumbariki Gerrit W. Gong wakati sasa akitumikia katika Akidi ya Mitume Kumi na Wawili.
Mikate na Samaki
“Bwana ni mkarimu na mwenye neema na hutafuta kutubariki sisi,” Mzee Gong anasema. “Kama tutafanya kadiri ya uwezo wetu, Atatuwezesha kufanya zaidi ya ambavyo tungeweza kufanya. Ni kama kuongezeka kwa mikate na samaki. Bwana huchukua kile kilichopo na kukiongeza zaidi ya kile ambacho tungeweza kufanya sisi wenyewe.”
Kanuni ya mikate-na-samaki pia ni ya kweli katika kujifunza, anasema. “Hata wakati elimu rasmi haipatikani, roho ya kujifunza ndio muhimu, kwa sababu kujifunza ni kwa milele. Sote tunaweza kutafuta nuru na kweli, bila kujali hali zetu. Tufanyapo hivyo, Bwana atatusaidia kuipata.”
Kuwa wa Maagano
Akiwa huko Oxford, Mzee Gong alijifunza kanuni nyingine ya injili, ambayo anaiita “kuwa wa maagano.”
“Tunaposogea karibu na Bwana, pia tunasogea karibu na kila mmoja wetu,” anasema. Tukiwa Oxford, Susan pamoja nami tulithamini uzoefu wetu katika kata sawa na uzoefu wetu wa kielimu. Wengi wa marafiki zetu wapenzi wa karibu mpaka leo ni watu kutoka Kata ya Oxford.”
Kati ya marafiki hao ni Tim na Katherine Witts, ambao wanakumbuka kwenda hekaluni na akina Gong. “Ninakumbuka waziwazi kwamba Ndugu Gong alitoa saa yake ili kwamba asisumbuliwe au kuzuiwa na muda wakati akitafakari mambo ya milele,” Dada Witts anasema. “Tendo hilo dogo limenisaidia mimi kuwa mwenye bidii zaidi katika kuabudu hekaluni kwangu binafsi.”
Akina Gong mara nyingi wanakutana na marafiki wanaowafahamu kwa sababu ya injili. “Watu watasema, tulifanya kazi na wewe wakati ukiwa katika baraza kuu,’ vitu kama hivyo,” Mzee Gong anasema, “na hutendeka pande zote. Nina shukrani kwa rais wa kigingi na baraza la kata ambao walinisaidia mimi kama askofu mchanga. Sote tuna deni kwa wazazi, wakwe, majirani, marais wa misheni, akina dada, na viongozi wa ukuhani ambao ni wakarimu kwetu, ambao hutuongoza na kututia moyo kuja kwa Kristo.
Urithi wa Familia
Historia ya familia ya Mzee Gong hurudi nyuma mpaka vizazi 34 kwa Dragon Gong wa Kwanza, aliyezaliwa miaka 837 Baada ya Kristo. Mababu wa Mzee Gong walihama toka China kwenda Marekani. Mama yake, Jean, alijiunga na Kanisa kama kijana huko Hawaii, Marekani, na baadae alihudhuria Chuo Kikuu cha Brigham Young huko Provo, Utah, Marekani, ambapo alikaa na familia ya Gerrit de Jong, mkuu wa Chuo cha Sanaa za Uchoraji. “Akina de Jongs walinisaidia kuelewa familia yenye injili huwaje,” anasema.
Baada ya BYU, Jean alihudhuria Chuo Kikuu cha Stanford huko Palo Alto, California, Marekani, ambapo alikutana na Walter A. Gong. “Tayari alikuwa ni Mkristo na haraka alielewa kile injili ya urejesho hutoa,” Jean anasema. Alijiunga na Kanisa, na Mwaka mmoja baadae walioana kwenye Hekalu la Salt Lake. Wote walikuwa waelimishaji waliobobea na kwa pamoja walitumia zaidi ya miaka 70 wakifundisha.
“Baba pia alikuja kuwa patriaki,” Mzee Gong anasema, “na kwa sababu baraka za kipatriaki zilikuwa zikitolewa nyumbani kwetu, nyumbani kwetu kulijaa staha ya kina kwa upendo wa Mungu kwa kila mtoto Wake.
Disemba 23, 1953, huko Jijini Redwood, California, mtoto wa kwanza kati ya watatu wa Jean na Walter alizaliwa. “Jina alilopewa, Gerrit, ni la kidachi, kumuenzi Gerrit de Jong,” Jean anafafanua. “Jina lake la kati ni Walter, kumuenzi baba yake. Na jina letu la familia ni Kichina, ambalo huenzi urithi wake.”
Jean anasema Gerrit alikuwa mwenye kujali ndugu zake wadogo, Brian na Marguerite. “Alipenda kuwasaidia,” anasema, “Hata kwa vitu vidogo kama vile kuwafundisha kufunga viatu vyao.” Jean anakumbuka akiwa anatoka kanisani siku moja na akiwasikia Gerrit na Brian wakisema walidhani hotuba ya mkutano wa sakramenti ilikuwa ya kuchosha. “Hivyo niliwapa changamoto: ‘Basi ninyi mje na hotuba nzuri zaidi.’ Waliikubali changamoto na kuanza kuwa makini na hotuba zote,” Jean anasema.
Kama kijana, Gerrit alipenda matembezi ya kupanda milima na wavulana wengine katika kata yake. Wally Salbacka, rafiki wa muda mrefu, anakumbuka safari moja hususan ya kupiga kambi. “Nilikuwa pale pamoja na Gerrit na kaka yake, Brian na rafiki ambaye hakuwa muumini wa Kanisa. Kwa sababu kadhaa tulianza kuimba nyimbo za dini. Gerrit aliimba melodi, Briani aliimba sauti ya tatu, na mimi niliimba sauti ya nne. Nafikiri tuliimba nyimbo za dini 10 au 20, kwa furaha ya kuimba. Ulikuwa ni uzoefu mzuri. Rafiki yetu ambaye hakuwa muumini alivutiwa.”
Kaka Salback pia anakumbuka kwamba katika shule ya Sekondari, Gerrit alimuomba kiongozi wa shamrashamra kuongoza shamrashamra za kimya kimya kwa ajili ya timu ya chesi. “Aliwashawishi kwamba uungwaji mkono wa kihisia ni mzuri kwa kila mtu,” na hatimaye walikuja kwenye mchezo!”
Baada ya shule ya Sekondari, Mzee Gong alihudhuria Chuo Kikuu cha Brigham Young. Kutoka mwaka 1973 mpaka 1975, alitumikia huko Misheni ya Taiwan Taipei, kisha alirudi BYU, ambapo mwaka 1977 alipokea shahada katika masomo ya Kiasia na masomo ya chuo kikuu.
Uchumba na Ndoa
Baada ya misheni, Mzee Gong alijitolea kuandaa mikutano ya jumapili jioni katika Shule ya Mafunzo ya Umisionari ya Provo. Mikutano iliwasaidia wamisionari waliokuwa wakielekea Taiwan kujua watu, mila na tamaduni za huko. Mmoja kati ya wamisionari alikuwa ni Dada Lindsay kutoka Taylorsville, Utah, binti wa Richard P. na Marian B. Lindsay. Kaka Lindsay alikuwa ni mshiriki wa Akidi ya Pili ya Sabini. “Nilihisi Susan alikuwa mtu ambaye nilikuwa nikimjua wakati wote,” Mzee Gong anasema.
Miaka miwili baadae, miezi kadhaa baada ya Susan kurudi BYU baada ya misheni yake, Gerrit alikuwa Provo pamoja na familia yake. Baba yake alikuwa akifundisha katika chuo kikuu, na Gerrit alikuwa amepanga matembezi ya wiki mbili. Matembezi yaliongezwa kuwa ya wiki nne, wakati yeye na Susan wakiwa kwenye miadi kila siku. Kisha Gerrit aliondoka kwa ajili ya mafunzo huko Hawaii kabla ya kurudi Oxford.
“Tulikuwa wapenzi kutoka tufe mbili tofauti,” Mzee Gong anakumbuka. “Nilikuwa nikijaribu kusoma huko Uingereza wakati nikijifunza kila kitu nilichoweza kumhusu kutoka ng’ambo ya bahari ya Atlantiki.”
“Tuliingia katika uchumba kupitia simu” Dada Gong anasema. “Alikuja nyumbani tena Siku ya Shukrani, na tulioana siku ya kwanza ya mwaka mpya hekalu lilipofunguliwa.” Wiki mbili baadae, walienda Uingereza kuanza maisha mapya pamoja.
“Wakati watu wakioana, wanazungumzia kuhusu familia mbili kuwa moja,” Mzee Gong anasema. “Na hicho kwa kweli ndicho kilichotokea kwangu. Ninajihisi ni sehemu ya familia ya Lindsay, kama vile nilivyo sehemu ya familia ya Gong.
Kazi ya Hali ya Juu
Baada ya kutumika muda mfupi kwenye kitengo huko Oxford, kazi ya Gerrit ilihamia katika huduma serikalini huko Washington, D.C., Marekani. Mnamo mwaka 1984 alitumikia kama mfanyakazi kwenye kampeni za uchaguzi wa marudio wa Reagan-Bush ambapo alishiriki sehemu ya ofisi na Mike Leavitt, ambaye baadae alikuwa gavana wa Utah. “Gerrit alikuwa mwangalifu na makini,” kaka Leavitt anasema, “lakini alitofautishwa kwa ukarimu wake usiopungua.
Katika mwaka 1985 Gerrit alihudumu kama msaidizi maalum wa Afisa wa Wizara ya mambo ya nje. Katika mwaka 1987 alikuwa msaidizi maalum wa balozi wa Marekani huko Beijing, China. Na kutoka mwaka 1989 mpaka 2001, alitumika katika sehemu tofauti tofauti katika kitivo cha Mikakati na Masomo ya Kimataifa huko Washington, D.C. Kisha alirudi katika ulimwengu wa kielimu ambapo alikubali ajira kama msaidizi wa rais wa mipango ya kimkakati huko BYU. Alihudumu miaka tisa katika jukumu hilo.
Carri Jenkins, msaidizi wa rais wa mawasiliano ya chuo kikuu BYU, alikuwa katika ofisi jirani. Anakumbuka uwezo wa Gerrit Gong kuwatia moyo wale wanaomzunguka. “Kama hukuwa na ujasiri kwamba ungeweza kufanya jukumu gumu, yeye alikuwa na ujasiri huo kwa ajili yako,” Carri anasema. “Alifanya kila kitu kilicho ndani ya uwezo wake kukushauri, kukupa tumaini, na kukuacha usonge mbele na kuonyesha uwezo wako.
Hakimu Thomas B. Griffith, ambaye alimjua Mzee Gong kote Washington na BYU, alielezea uhusiano pamoja na yeye kwa njia hii: “Mwisho wa maongezi, unatambua kitu muhimu ilikuwa ni wewe. Yeye ni msikilizaji mzuri sana. Na huuliza maswali ambayo hukufanya utafakari.”
Cecil O. Samuelson, aliyekuwa Kiongozi Mkuu Mwenye Mamlaka wa Sabini na rais wa zamani wa BYU, anasema Mzee Gong kwa ujumla ni mkimya, lakini magurudumu siku zote yanaendelea kuzunguka.”
Maisha ya Kifamilia
Gerrit na Susan Gong walikuja kuwa wazazi wa wana wanne—Abraham, Samuel, Christopher, na Matthew—ambao walikulia katika mazingira tofauti tofauti.
“Wakati tulipokuwa Beijing, watoto wetu walikuwa na baraka ya kuwa marafiki wa dhati,” Mzee Gong anasema.
“Kwa upande mmoja, walikuwa na fursa ya kuona taswira iliyopanuka ya dunia,” Dada Gong anaongezea. “Kwa upande mwingine, ilitusaidia kuwa tuliounganika kwa nguvu pamoja kama familia. Wavulana wetu bado husema kitu kizuri tulichofanya kama wazazi kilikuwa ni kuwapa akina kaka.”
“Kwanza tulitumia fursa ya mara kwa mara ya kusafiri kwa ndege,” Mzee Gong anasema. “Tuliacha kila mtu kuchagua mwisho wa safari yake. Tulianza huko Washington, D.C., ambako tulikuwa tukiishi, kisha tukaenda Uingereza, Jamhuri ya Czech, Ugiriki, Uturuki, India, Uchina, na Japani.
“Tulikuwa na sheria moja thabiti wakati wa safari ile,” Susan anasema. “Popote tulipoenda, tulikula kile amabacho wenyeji walikula.” Hatimaye, huko Japani katika mwisho wa safari, Mzee Gong aliwaaambia wanawe kwamba alikuwa akiwapeleka kwenye mgahawa maarufu duniani kwa nyama ya ng’ombe. Wakiwa McDonald, wana wanne na wazazi wawili wenye njaa walimaliza hambaga 17!
“Wote Mama na Baba waliweka thamani ya juu katika kujifunza kupitia uzoefu,” Abraham anasema. “Baba hutafakari kwa kina kuhusu jinsi gani uzoefu huwachonga watu, ikijumuisha tamaduni nzima.” Abraham pia hukumbuka kwamba baba yake “huongea kwa umakini kwa sababu lazima amaanishe na kuamini kikamilifu kile anachokisema.”
Sam hukumbuka kwamba “pamoja na shughuli nyingi alizokuwa nazo katika Idara Serikalini, Baba alichukua muda kila usiku kuniongoza na kunifundisha kwa ajili ya shidano la hesabu za daraja la tatu ambalo nilitaka kushiriki, likiitwa ‘Challenge 24.’ Alisema kama nitashinda tutakuwa na sherehe ya kula aiskrimu ya matundana barafu na mipako 24.” Sam alifika mpaka fainali za kitaifa lakini hakushinda. Hata hivyo familia ya Gong bado walikula aiskrimu ya matunda na barafu. Lakini haikuwa rahisi kupata mipako 24—mtu atakuwa ni mla nyama sana.
Christopher na Matthew walitoa maoni juu ya jinsi gani “wanathamini sana uaminifu, upendo, na kujitolea ambako baba na mama yetu wanashiriki.” Ni upendo wa Mzee na Dada Gong wanaoshiriki wao kwa wao pamoja na kila mwana na kwa familia yote.
“Vile vile kama baba mwenye kujitolea, Gerrit ni mwana na kaka anayejitolea,” Susan anasema. “Majukumu hayo ni muhimu kwake. Hutusaidia sisi kuelewa kwamba mahusiano ya kifamilia ni muhimu sana kuliko vitu yote.”
Uzoefu wa Kanisani
Japokuwa alikuwa na shughuli nyingi katika kazi pamoja na familia, Mzee Gong aliendelea kwa utayari kutumikia Kanisani, akitimiza wito kama mjumbe wa baraza kuu, kiongozi wa kikundi cha makuhani wakuu, rais wa Shule ya Jumapili, mwalimu wa seminari, askofu, rais wa kigingi wa misheni, rais wa kigingi, na sabini wa eneo.
Kwa chochote alichoitwa kufanya, na katika maisha ya familia yake pia, kwa uthabiti alionyesha sifa dhahiri. “Anamuona kila mtu kama mwana au binti wa Baba wa Mbinguni,” Dada Gong anasema. “Lakini juu ya yote, anampeda Bwana. Anatamani kwa moyo wake wote kujenga ufalme na kuwabariki watoto wa Baba wa Mbinguni.”
Na anampenda mke wake. “Chochote ninachoombwa kufanya,” anasema, “Susan yu pamoja nami. Yuko sawa na kila mtu na anaelewana na watu wengine. Amekuwa kila mara tayari kwenda sehemu mpya na kujaribu vitu vipya, kitu ambacho ninashukuru.”
Huduma katika Sabini
Mnamo Aprili 3, 2010, Mzee Gerrit W. Gong alikubaliwa kama Kiongozi Mkuu Mwenye Mamlaka wa Sabini. Alipewa jukumu kwenye urais wa eneo la Asia, lenye makao makuu huko Hong Kong. Baadae alikuja kuwa Rais wa Eneo la Asia. Mnamo Oktoba 6, 2015, Mzee Gong alikubaliwa kwenye Urais wa Sabini, ambako uzoefu wake wa kimataifa uliendelea, ikijumuisha upitiaji upya wa maeneo katika sehemu mbalimbali za ulimwengu kama Afrika na Amerika ya Kati.
“Unakutana na kuwapenda Watakatifu katika sehemu hizi zote,” anasema. “Unahisi kubarikiwa kwa kuwa na watu wakikuambia kuhusu imani yao, kwa sababu ya uzoefu wa Mungu kufanya kazi katika maisha yao huwa sehemu ya uelewa wa Mungu ni nani na jinsi gani Anampenda kila mmoja wetu.”
“Tunapomtuma Mzee Gong katika hali yoyote, wale wanaohusika wanahisi wamepata rafiki,” anasema Rais Ressell M. Nelson. “Ana elimu kubwa, lakini ni mnyenyekevu. Anahusiana na watu katika ngazi zote na mara zote anakuwa amejiandaa kikamilifu na kushawishi.”
Wito kama Mtume
Wakati Rais Nelson alipotoa wito kwa Mzee Gong kutumikia kama mshiriki wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, nabii “kwa upendo aliichukua mikono yangu kwake, [pamoja] na mpendwa wangu Susan akiwa pembeni mwangu, na kutoa mwito huu mtakatifu kutoka kwa Bwana ambao ulinistaajabisha” (“Kristo Bwana Amefufuka Leo,” Ensign au Liahona, May 2018, 97). Kwa kunyenyekezwa, lakini kwa uhakika wa upendo wake kwa Kristo na uaminifu wake, Mzee Gong alikubali wito. Alikubaliwa mnamo Machi 31, 2018. Kwa umakini akiandaliwa na Bwana, sasa atatumikia kama [shahidi] maalumu wa jina la Kristo ulimwenguni kote”(M&M 107:23).