Kidijitali Pekee
Kuvunjika kwa Uhusiano Wangu Ilikuwa Kkweli ni Mojawapo ya Baraka Zangu Kubwa Sana.
Wakati mwingine tunaona sababu za ushawishi na wakati mwingine hatuzioni. Kwa vyovyote vile, lazima tutumie imani katika kutenda.
Uhusiano wangu na mpenzi wangu ulivunjika usiku wa majira ya kiangazi.
Mapema siku hiyo, mimi na Carter (jina limebadilishwa) tulikuwa tukigombana—kitu ambacho kilikuwa cha kawaida katika kipindi cha miaka mitatu, ya uhusiano wetu, wa hapa na pale. Tuligombana kuhusu karibu kila kitu—kuhusu kile tutakula hata mipango ya siku za usoni. Mwanzoni, niliweka tofauti zetu kando kwa msemo kwamba “utofauti huvutia.” Lakini utani wetu wa kawaida hatimaye ulibadilika taratibu na kuwa mnyororo wa kuchosha wa kutokukubaliana.
Usiku ule wa majira ya joto, tulikuwa tumechukua hadubini kwenda nayo jangwani kuangalia sayari. Lakini tulikuta kwamba mwangaza wa mwezi dhidi ya anga lenye giza ulizuia uoni wetu. Kwa kuchanganyikiwa, tulianza kubishana—tena.
Niliishia kuondoka ili kutuliza nafsi yangu. “Huyu si mimi,” nilifikiria. Nilijulikana kama mpatanishi kati ya ndugu zangu, na niliongea kwa upole na kwa upendo kwa rafiki zangu wengine. Sasa kwa nini nilikuwa nikipiga kelele kwa mvulana niliyedai nampenda?
Niliangalia anga yenye kiza na kusali ili kujua ni kwa namna ipi ningeweza kuboresha uhusiano wangu na Carter. Ghafla, amani kuu ilichukua nafasi ya hasira yangu, na nikahisi hisia ya kwamba kitu kizuri ambacho ningeweza kufanya kwa ajili yetu ilikuwa ni kusitisha uhusiano wetu.
Uponyaji ulichukua muda. Kulikuwa na nyakati ambazo nilijaribiwa kuondoa msukumo wa kuvunja uhusiano wangu na Carter kwa sababu niliukosa uzoefu wa uhusiano wetu. Wakati mwingine nilihisi kumkasirikia Mungu, nikiamini kwamba Yeye alifunga kwa nguvu mlango mmoja bila kufungua mwingine. Hata hivyo nilishikilia ushauri wa Mzee Jeffrey R. Holland wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili: “Katika nyakati za woga au shaka au nyakati za kutatiza … shikilia kwa nguvu kile ambacho tayari unakijua na simama imara mpaka uelewa wa ziada utakapokuja” (“Bwana Ninaamini,” Liahona, Mei 2013, 93–94).
Sikupokea huo “uelewa wa ziada” kwa miezi mingi, na nilianza kufikiria kama ningeupokea. Baada ya sala moja ya dhati kuhusu kuvunja uhusiano, Roho alinisihi katika moyo wangu, akiniambia kwamba misukumo ya Baba wa Mbinguni ni kwa ajili ya faida ya watoto Wake. Maelezo ya sababu Zake si muhimu kama imani yangu Kwake ilivyo.
Kwa kujua kwamba Baba wa Mbinguni alikuwa na mpango kwa ajili yangu ilinipa tumaini kwa kipindi kijacho na kunisaidia kuanza kufanya miadi tena. Asubuhi moja, nilisoma Mafundisho na Maagano 88:40, ambapo Bwana hufundisha kwamba “nuru huambatana na nuru.” Ghafla niligundua kwamba kanuni hii inaweza kutumika katika kufanya miadi. Nilijua ningekuwa mwenye furaha zaidi na mtu ambaye anashiriki pamoja nami maadili na nuru.
Hatimaye nilikutana na Austin. Tuliunganika mara moja, kutoka kwenye kupenda kwetu chakula aina ya taco hata misheni zetu. Roho yake ya upole ilioneka ya kueleweka na ya kuendana na yangu, na mwishowe tulioana. Ambacho tunacho si uhusiano wa kusisimua kama ambao ungeweza kuutegemea kutoka kwenye sinema maarufu za mapenzi. Ni mzuri na imara—ni kitu ambacho ninaamini kinaweza kudumu milele.
Wengi wetu tunategemea kitu cha mara moja pale tunapopokea ushawishi mgumu. Kutoka kwenye uzoefu wangu, nilijifunza kwamba imani katika Bwana inaweza kutusaidia kubaki watiifu bila kujua sababu. Tunapoamini katika Mungu-ajuaye yote, tunaweza kuhisi amani katika chaguzi zetu kutenda kulingana na msukumo mpaka tunapopokea “uelewa wa ziada” Alioahidi kwa waaminifu.