2018
Kujifunza katika njia ya Bwana
Oktoba 2018


Kujifunza katika Njia ya Bwana

Kutoka kwenye ujumbe uliotolewa kwenye semina ya marais wapya wa misheni mnamo Juni 25, 2014.

Kumwalika Roho Mtakatifu kuwa mwalimu ni dhumuni kuu katika utaratibu wote wa Bwana wa kujifunza.

two girls talking

Kuharakisha kazi ya Bwana kunatuhitaji sisi kujifunza bila kukoma, kubadilika, na kusonga mbele kwa imani katika Mwokozi.

Utaratibu katika Mambo Yote

Katika ufunuo uliotolewa kupitia Nabii Joseph Smith mnamo Juni ya 1831, Bwana alitangaza: “Na tena, nitatoa kwenu utaratibu katika mambo yote, ili msidanganyike; kwani Shetani amezagaa katika nchi, na anaenda akiwadanganya mataifa” (M&M 52:14).

Cha kushangaza, Bwana alitupatia “utaratibu” na si “utaratibu mmoja” kwa vitu vyote. Siamini kwamba Bwana anapendekeza kwa lugha “utaratibu katika mambo yote” kwamba Yeye ana utaratibu mmoja tu wa kutumika katika kila hali. Badala yake, njia ya Bwana hujumuisha taratibu tofauti tofauti ambazo zinaweza kutumika kutimiza malengo mbalimbali ya kiroho.

Lengo la juu katika uzoefu wowote wa kujifunza na kufundisha halina budi kuwa la kuamua na kutumia utaratibu au taratibu ambazo zinatimiza mahitaji yetu vizuri zaidi na kufikia matokeo tarajiwa ya kujifunza.

Roho Mtakatifu ni Mwalimu

Roho Mtakatifu ni mshiriki wa tatu wa Uungu na Mfunuzi, Mwalimu, Mfariji, Mtakasaji, na huleta vitu vyote katika kumbukumbu zetu (ona Yohana 14:16–17, 26; 3 Nefi 27:20). Mzee James E. Talmage (1862–1933) wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili alielezea, “Ofisi ya Roho Mtakatifu katika Huduma Yake kati ya watu inaelezewa katika maandiko. Yeye ni Mwalimu aliyetumwa kutoka kwa Baba; na kwa wale ambao wanastahiki usaidizi Wake atawafunulia vitu vyote vya umuhimu kwa ajili ya ukuaji wa nafsi.”1 Kumwalika Roho Mtakatifu kuwa mwalimu ni dhumuni kuu katika utaratibu wote wa Bwana wa kujifunza na kufundisha.

young woman reading Preach My Gospel

Mwanafunzi anayetumia uhuru wake wa kuchagua na kutenda kulingana na kanuni sahihi hufungua moyo wake kwa Roho Mtakatifu—na hivyo hualika mafundisho Yake, nguvu Yake ya kushuhudia, na ushahidi wenye kuthibitisha. Kujifunza kwa imani kunahitaji jitihada za kiroho, akili, na kimwili na si upokeaji usio na matendo. Kwa moyo wa dhati na uthabiti wa matendo yetu yanayoongozwa na imani, tunaonyesha kwa Baba yetu wa Mbinguni na Mwanaye, Yesu Kristo, utayari wetu wa kujifunza na kupokea maelekezo kutoka kwa Roho Mtakatifu.

Fikiria jinsi gani wamisionari huwasaidia wachunguzi kujifunza kwa kutumia imani. Kuweka na kutunza ahadi za kiroho, kama vile kujifunza na kusali kuhusu Kitabu cha Mormoni, kushika amri, na kuhudhuria mikutano ya Kanisa humwitaji mchunguzi kutumia imani na kutenda. Kanuni hii pia hutumika kwa waumini wote, ikijumuisha wazazi, walimu, na viongozi.

Kufundisha, kuhimiza na kufafanua—muhimu kama vilivyo—haviwezi kufikisha kwa mchunguzi, mtoto, mwanafunzi au muumini ushuhuda wa ukweli wa injili ya urejesho. Pale tu imani yao inapoanzisha tendo na kufungua njia kuelekea kwenye moyo ndipo Roho Mtakatifu anaweza kutoa ushuhuda thabiti. Wamisionari, wazazi, waalimu, na viongozi ni wazi kwamba lazima wajifunze kufundisha kwa nguvu ya Roho. Muhimu sawa na hilo, hata hivyo, ni wajibu walionao kuwasaidia wengine kujifunza wao wenyewe kwa kutumia imani.

Kujifunza ninakoelezea kunafika mbali zaidi ya utambuzi wa uelewa pekee na kutunza na kukumbuka taarifa. Aina ya kujifunza ambayo ninaizungumzia hutusababisha sisi kuamka katika Mungu (ona Alma 5:7), kuuvua uanadamu wa asili (ona Mosia 3:19), kubadili mioyo yetu (ona Mosia 5:2), na kuongoka katika Bwana na kutoasi kamwe (ona Alma 23:6). Kujifunza kwa kutumia imani huitaji vyote moyo na utayari wa akili (ona M&M 64:34) na ni matokeo ya Roho Mtakatifu kubeba nguvu ya neno la Mungu katika moyo na ndani ya moyo. Kujifunza kwa kutumia imani hakuwezi kutolewa kutoka kwa mwelekezi kwenda kwa mwanafunzi, kutoka kwa mmisionari kwenda kwa mchunguzi, kupitia mhadhara, au mifano ya mazoezi kwa vitendo; isipokuwa mwanafunzi lazima atumie imani na kutenda ili kupata uelewa yeye mwenyewe.

Mpangilio wa Kujifunza na Kufundisha

1. Jitayarishe kujifunza. Kama unahudhuria darasa lako la shule ya Jumapili na kumsikiliza mwalimu wako akitambulisha mada, basi hivyo ni vizuri. Lakini kama umefanya kazi na kujiandaa, kama unafikiria kuhusu vitu ambavyo mwalimu wako amekualika kuvisoma, kutafakari na kusali kuvihusu kabla ya darasa, kunaweza kuwa na miminiko la nguvu za Roho, na Roho Mtakatifu anakuwa mwalimu wako. Maandalizi hualika ufunuo.

2. Changamana na wengine ili kujengana. Nataka kuleta umakini wenu kwenye mstari huu. “Chagueni mwalimu miongoni mwenu, na wote wasiwe wazungumzaji kwa wakati mmoja; bali azungumze mmoja na wengine wote wasikilize maneno yake, ili wote watakapokuwa wamezungumza wote wapate kujengana, na kwamba kila mmoja apate kuwa na nafasi sawa” (M&M 88:122).

young man teaching

Huu ni mpangilio mmojawapo wenye nguvu wa Bwana kwa ajili ya kujifunza na kufundisha. Ninaweza kupendekeza njia nyingine ya kuuangalia mstari huu: “Chagueni mwalimu miongoni mwenu.” Mwalimu ni nani? Roho Mtakatifu. Je, ingekuwa ni kama mnataka Roho Mtakatifu kuwa mwalimu, basi “wote wasiwe [wazungumzaji] kwa wakati mmoja; bali azungumze mmoja na wengine wote wasikilize maneno yake, ili wote watakapokuwa wamezungumza wote wapate kujengana”? Mmoja pekee ambaye anaweza kuleta kujengana huko ni Roho Mtakatifu.

Kuchangamana na wengine ili kujengana hualika ufunuo. Kwa sasa Kanisani, tunajifunza na kutumia kwa unyeti zaidi wa kiroho, kwa umakini wa hali ya juu, na uangalifu wa mpangilio wa kujifunza na kufundisha. Je, tutafanya kile ambacho mara zote tumefanya na kupata matokeo yaleyale ambayo kila mara tumeyapata, au tutatubu na kujifunza na kubadilika na kufundisha kwa wingi zaidi katika njia ya Bwana?

3. Alika Kutenda. Swali moja jepesi husaidia kufikia lengo hili. Je, utafanya nini na kile ulichojifunza? Kufanyia kazi ufunuo hualika ufunuo zaidi.

Ni sala yangu kuwa tutaenda sambamba na kasi ya uharakishaji wa Bwana, kwamba hatutafanya tu kile ambacho tumekuwa tukifanya mara zote katika njia ambayo tumekuwa tukitumia mara zote.

Ninatangaza ushahidi wangu wa uhalisia wa Bwana Yesu Kristo. Ninatoa ushahidi kwamba Anaishi. Amefufuka. Anasimama katika kichwa cha Kanisa hili na anaongoza mambo yake. Anatuomba sisi sote tuweze kuwa sambamba na kasi ya uharakishaji Wake na kufuata mpangilio ambao Ameuweka kwa ajili ya ukuaji wetu na kujifunza.

Muhtasari

  1. James E. Talmage, Makala ya Imani, 12th ed. (1924), 162.