“Nuru ya Uzima,” Liahona, Jan. 2023.
Nuru ya Uzima
Mwokozi Yesu Kristo ni nuru yetu, uzima wetu na njia yetu—jana, leo na milele.
Wakati jua lilipozama kwenye Jumapili nyingine ya mwaka 1948, nilijikuta nikitembea kuelekea upande wa chini wa Mto Trent katika mji wa Nottingham,Uingereza. Nikiwa mmisionari mwenye umri wa miaka 20, punde tu nilikuwa nimeitwa kama rais wa wilaya. Ilikuwa imekuwa siku ndefu, ya kuchosha iliyojawa na mikutano na kuhudumu, lakini nilikuwa mwenye furaha na kuridhishwa katika kazi.
Nilipokuwa nikitembea kando kando ya mto, nilisali ndani ya moyo wangu. Nikitegemea kuhisi mwongozo kidogo kutoka kwa Bwana, Niliuliza, “Je, Ninafanya kile Unachotaka?”
Hisia nzito za amani na uelewa zilinifunika. Katika wasaa ule, nilikuja kujua kwamba Yesu Kristo alinijua mimi na alinipenda. Sikuona ono au kusikia sauti, lakini nisingeweza kujua juu ya uhalisia na uungu wa Kristo kwa nguvu zaidi hata kama angesimama mbele yangu na kuliita jina langu.
Tukio hili la upendo wa kuvutia liliyapa umbo maisha yangu. Kutoka siku ile mpaka leo, kila uamuzi wa maana nilioufanya umeshawishiwa na uelewa wangu juu ya Mwokozi. Kwa miaka yote na karibu ulimwenguni kote, nimeshuhudia kwamba Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu, ni Nuru ya Ulimwengu. Ni heshima kwetu sisi kuja kwake, kumfuata Yeye na kuhisi nuru Yake ndani ya maisha yetu.
Nuru ya Ulimwengu
Usiku mmoja miaka mingi iliyopita baada ya tukio lile la kukumbukwa la kimisionari, mke wangu, Barbara na mimi tulikuwa tukilikazia macho anga. Tulipokuwa tukifanya hivyo, niliangalia juu kwa mshangao wa mamilioni ya nyota, ambazo zilionekana kuwa na uangavu wa kipekee na za kupendeza usiku ule. Mawazo yangu yaligeuka kwa kustaajabu juu ya maneno ya Bwana kwa Musa: “Na dunia zisizo na idadi nimeziumba; na pia niliziumba kwa madhumuni yangu mwenyewe; na kwa njia ya Mwana niliziumba, ambaye ndiye Mwanangu wa Pekee” (Musa 1:33).
Kutoka kwa Mwokozi ilikuja nguvu ambayo iliumba na ambayo inatoa nuru kwa jua, mwezi, nyota na dunia (ona Mafundisho na Maagano 88:7–10). Anaweza kwa haki kutangaza, “Mimi ni nuru ya ulimwengu: yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima” (Yohana 8:12; ona pia Yohana 9:5).
Katika maneno ya Rais Dallin H. Oaks, Mshauri wa Kwanza katika Urais wa Kwanza, “Yesu Kristo ni nuru ya ulimwengu kwa sababu Yeye ni chanzo cha nuru ‘itokayo katika uwepo wa Mungu ili kujaza sehemu kubwa’ (Mafundisho na Maagano 88:12].” Nuru ya Mwokozi ni “nuru ya kweli imwangazayo kila mtu ajaye ulimwenguni” (Mafundisho na Maagano 93:2; ona pia 84:46). Kwa nuru hii, tunaweza kujua jinsi ya kuhukumu “mema na maovu” (Moroni 7:16). Nuru hii iliyoenea kote ulimwenguni inajulikana kama “nuru ya ukweli,” “nuru ya Kristo,” na “Roho ya Kristo” (Mafundisho na Maagano 88:6; 88:7; Moroni7:16).1
Mtume Yohana alisema, “Nuru ing’aayo gizani; wala giza halikuiweza” (Yohana 1:5). Katika siku zetu, Shetani anafanya kazi mpaka muda wa ziada ili awaongoze watoto wa Mungu gizani, akizuia “nuru na uzima na ukweli wa ulimwengu” (Etheri 4:12).
Hatuwezi kwa ukamilifu kuelewa—au kumshukuru—Mwokozi na Injili Yake wakati tunapoteza ukweli na nuru Yake. Lakini tunapotubu na kutii, kuhudumu na kumwabudu Yeye, tunalishinda giza. Nuru Yake inarudi na inaondoa vivuli vya ulimwengu kutoka katikati yetu na akilini mwetu.
Kubarikiwa na Nuru
Ulimwengu wetu unapozidi kuwa na giza na zaidi usiokalika, kuhisi nuru ya Bwana ndani ya maisha yetu inaweza kuonekana kama changamoto. Lakini Rais Russell M. Nelson ametukumbusha, “Giza linaloongezeka ambalo linaambatana na taabu linaifanya nuru ya Yesu Kristo iangaze zaidi na zaidi.”2
Nimegundua kwamba Nuru Yake inawaka kwa ung’aavu mkubwa katika nafsi yangu ninapotenga muda kwa ajili ya vitu vya Roho nyakati za utulivu na nyakati za ukimya kama usiku ule nikiwa na Barbara. Hapo ndipo fikra za kiroho, mwongozo na nuru vinakuja kwetu. Hapo ndipo tunapokuja kuelewa jinsi gani hakika tumebarikiwa kuwa na Mwokozi.
Kama Nuru ya ulimwengu, Mwokozi huangaza njia ya safari yetu duniani kwa mfano Wake na mafundisho Yake (ona Yohana 8:12). Anaufanya mwepesi mzigo wetu kwa upendo Wake na huruma Yake (ona Mathayo 11:28–30). Anaifanya miepesi mioyo yetu kwa tumaini na uponyaji kupitia Upatanisho Wake (ona Moroni 7:41). Na Anaangaza akili zetu kwa “Roho wa ukweli” (Mafundisho na Maagano 6:15; ona pia 11:13).
Mzee David A. Bednar wa Akidi ya wale Kumi na Wawili amesema, “Katika kila kipindi cha maisha yetu, katika hali zote tunazoweza kukabiliana nazo na katika kila changamoto tunayoweza kukabiliana nayo, Yesu Kristo ndiyo nuru inayofukuza hofu, inayotoa uhakika na mwelekeo na inasababisha amani na shangwe ya kudumu.”3
Inua Nuru Yako
Fursa ya kushiriki nuru ya Mwokozi pamoja na wengine na kuwaalika waje Kwake na kuhisi upendo Wake kwa ajili yao imekuwa siku zote ya kipekee kwangu. Nilipenda kuwa mmisionari Uingereza. Nilipenda kuwa rais wa misheni Kanada. Na ninapenda wito wangu wa sasa kama mshiriki wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili. Wito wangu unanipa fursa za kushuhudia juu ya Yesu Kristo na kushiriki ujumbe wa Urejesho Ulimwenguni kote.
Hapo kale, Mwokozi aliwaambia wanafunzi Wake:
“Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima. …
“Nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni” (Mathayo 5:14,16).
Kwa watu wa Nefi, Alisema, “Tazama mimi ni mwangaza ambao mtainua juu—kwamba mfanye yale ambayo mmeniona nikifanya. Aliongeza, “Mnajua vitu ambavyo mnahitajika kufanya katika Kanisa langu; kwani vitendo ambavyo mmeniona nikifanya, hivyo pia mtafanya” (3 Nefi 18:24; 27:21).
Katika siku yetu, Mwokozi vilevile anategemea wafuasi Wake watumie nuru Yake “kuifukuza giza kutoka miongoni [mwetu]” (Mafundisho na Maagano 50:25). Nuru yetu hung’aa tunapopenda kama Yesu alivyopenda. Nuru yetu hung’aa tunaposhiriki ushuhuda wetu wa Urejesho na tumaini letu katika Kristo. Nuru yetu hung’aa tunapoinua sauti zetu katika kuulinda ukweli. Na nuru yetu inapong’aa, tunawavuta wengine kwenye chanzo cha nuru hiyo.
Toa huduma isiyo ya uchoyo na utahisi nuru Yake ndani ya moyo wako. Kwa unyenyekuvu sali kwa ajili ya fursa za kushiriki injili na utaongozwa kwa wale walio tayari kuikubali nuru Yake. Wapende wengine kwa njia zilizo ndogo na kubwa na unafanya ulimwengu huu kuwa mzuri zaidi na angavu zaidi.
Nuru Ambayo Haina Mwisho
Daima nina shukrani kwa ajili ya uzoefu nilioupata kama mmisionari kijana huko Uingereza wakati nilipokuja kujua mimi mwenyewe kwamba Yesu ni Kristo. Ninalijua hili kwa uhakika zaidi leo kwani nimepata uzoefu wa maisha pamoja na majaribu yake yote na furaha zake zote.
Huduma yangu katika Kanisa imenibariki kwa matukio mengi ya kiroho ya kustaajabisha na maalum na baadhi ni matakatifu sana hata kuyajadili. Hakuna zawadi muhimu zaidi na ya thamani ambayo ninaweza kuitoa kwa watoto wangu, wajukuu, vitukuu na kwenu nyinyi rafiki zangu ulimwenguni kote, zaidi ya ushahidi wangu wa uhakika kwamba Yesu ni Kristo, Mwana wa Baba yetu wa Milele, Mwokozi na Mkombozi wa wanadamu wote.
Mke wangu wa thamani, Barbara, alifariki mwaka 2018. Nina shukrani jinsi gani kujua kwamba kwa sababu ya kuunganishwa kwetu hekaluni na kwa sababu ya Yesu Kristo, tutakuwa pamoja tena, pamoja na familia yetu, kwa milele yote.
Wakati mwingine, Ninakuwa mchovu. Katika nyakati hizo, ninasimama na kuangalia picha ya Mwokozi. Ninamfikiria Yeye katika Gethsemane na kisha, ghafla, siwi mchovu tena. Ninajua moyoni mwangu kwamba kwa sababu Yeye aliushinda ulimwengu, “giza limepita na ile nuru ya kweli imekwisha kung’aa” (1 Yohana 2:8).
Ninajua kwamba Yesu Kristo yu hai. “Yeye ni … nuru isiyo na mwisho, ambayo haiwezi kutiwa giza” (Mosia 16:9). Yeye ni nuru yetu, uzima wetu na njia yetu—jana, leo na milele. Na tuwe thabiti katika kumfuata Yeye na kuangaza nuru Yake mbele ya ulimwengu.