2023
Kama Yeye Anaweza Kuyageuza Maji kuwa Divai …
Januari 2023


Kama Yeye Anaweza Kuyageuza Maji kuwa Divai … ,” Liahona, Jan, 2023.

Miujiza ya Yesu

Yohana 2:4–11

Kama Yeye Anaweza Kuyageuza Maji kuwa Divai …

Mambo matatu nilivyojifunza kutokana na muujiza huu ambao mara kwa mara hautiliwi maanani.

mabirika yenye maji na divai

Yohana ni mwandishi pekee wa Injili ambaye anasimulia Mwokozi akiyageuza maji kuwa divai (ona Yohana 2:1–11). Alihisi msukumo wenye nguvu kuhusu tukio hilo hata kutuambia kuwa ulikuwa ndio “mwanzo wa miujiza” ya Mwokozi (Yohana 2:11).

Kiutamaduni, matokeo ya kuishiwa divai yangeweza kuathiri taswira ya kijamii ya wale waliohusika. 1 Na wakati siamini kwamba muujiza unatakiwa uwe wa kuvutia ili uweze kubadilisha maisha, nimejiuliza kwa nini Yohana alihisi muujiza huu ulikuwa muhimu sana miongoni mwa mingine mingi ambayo ilikuwa ya kuvutia na ya kubadilisha maisha.

Kwa nini Miujiza?

Kwa nini miujiza ilikuwa muhimu sana katika huduma yote ya Mwokozi? Kwa hakika ilikuwa kwa sehemu kwa sababu ya huruma Yake kwa ajili ya wale waliokuwa katika uhitaji (ona Marko 1:41). Kwa nyongeza, miujiza ilikuwa ushahidi muhimu juu ya nguvu na mamlaka Yake ya kiungu (ona Marko 2:5, 10–11). Matukio ya kimiujiza yangeweza pia kuimarisha imani na kuleta usikivu kwenye ujumbe Wake (ona Yohana 2:11; 6:2).

Kisha mtu fulani alisisitiza kwangu kwamba miujiza ya Mwokozi siyo tu iliwaleta watu kusikiliza ujumbe; bali pia ilisaidia kufundisha ujumbe.2 Wakati nilipojiuliza ningeweza kujifunza nini kuhusu Yesu Kristo na misheni yake tukufu kutokana na kuyageuza maji kuwa divai, nilianza kuona mambo mapya.

Haya ni masomo matatu niliyojifunza kutokana na muujiza wa Kana kuhusu Mwokozi na uwezo Wake wa kuokoa.

1. “Saa yangu haijawadia”

Wakati Mariamu alipomwomba Yesu msaada,Yeye alijibu, “saa yangu haijawadia” (Yohana 2:4). Bila maelezo ya kina zaidi, haiko wazi kutoka katika kumbukumbu ya Yohana nini hasa Mariamu alitarajia au nini Yesu alimaanisha kwa jibu Lake kwamba saa Yake haijawadia.

Kifungu hiki cha maneno kilionekana kwangu kuwa muhimu. Inawezekana kwamba Yesu alikuwa akirejelea baadhi ya matukio yajayo karibuni, kama vile kuanza kwa huduma Yake kwa umma. Wakati huo huo, msemo ulikuwa na mwangwi ambao unajirudia katika kumbukumbu yote ya Yohana, mara kwa mara ukionesha mbele kwenye hatma ya muujiza wa dhabihu Yake ya kulipia dhambi (ona Yohana 4:21–23; 5:25–29; 7:30; 8:20). Hatimaye, msemo unajirudia tena mwishoni mwa huduma Yake duniani, wakati “Yesu akijua kwamba saa yake imefika kwamba anapaswa kuondoka katika ulimwengu huu kwenda kwa Baba” (Yohana 13:1, msisitizo umeongezwa; ona pia Yohana 12:23, 27; 16:32). Na kabla ya kuondoka kwenda Gethsemane, Alisali, “Baba, saa imekwisha kufika; mtukuze Mwanao, ili mwana wako naye akutukuza wewe” (Yohana 17:1, msisitizo umeongezwa).

Kumwona Yohana akirudia kifungu hiki katika kumbukumbu yake yote kulinisaidia kuona mwisho kutokea mwanzo. Kwanza, Yesu aliyageuza maji kuwa divai ili kuridhisha kiu ya kimwili. Kisha, mwishoni, alitumia divai ya sakramenti kuwakilisha damu yake ya kulipia dhambi, ambayo ilifanya uzima wa milele uwezekane na kusababisha wale walioamini katika Yeye kamwe wasipate kiu tena (ona Yohana 4:13–16; 6:35–58; 3 Nefi 20:8).

2. “Lolote atakalowaambia, fanyeni”

Baada ya kumwomba Yesu msaada, Mariamu aliwaambia watumishi, “Lolote atakalowaambia fanyeni” (Yohana 2:5). Kuna somo katika maelezo haya na katika mifanano inayovutia kati ya maelezo haya na maelezo ya Yusufu huko Misri.

“Na wakati nchi yote ya Misri ikitaabika na njaa, watu walimlilia Farao kwa ajili ya mkate: na Farao alisema kwa Wamisri wote, Enendeni kwa Yusufu; Atakachowaambia fanyeni” (Mwanzo 41:55, msisitizo umeongezwa).

Yawezekana Mariamu hakukusudia kufanya muunganiko huu, na pengine Yohana hakukusudia pia. Lakini kama nilivyoona mifanano hii, mawazo mawili yalikuja akilini mwangu.

Kwanza, niliona bado kuna njia nyingine ambayo Yusufu na watu mashuhuri kutoka Agano la Kale walikuwa ishara ya Yesu Kristo na huduma Yake. Lakini, muhimu zaidi, hadithi za Misri na Kana zilinikumbusha kwamba siyo tu Yesu Kristo anaweza kutuokoa kutoka dhambi na kifo kupitia Upatanisho Wake—ambao baadaye aliuwakilisha kwa mkate na divai—bali Anaweza pia kutuokoa kutokana na changamoto za kimwili, kijamii, na nyinginezo. Wakati watu walipoishiwa mkate, Farao aliwaambia watu wafanye chochote ambacho Yusufu angewaambia. Walifanya na walipewa mkate na waliokolewa na mateso ya kimwili. Wakati watumishi walipoishiwa divai, Mariamu aliwaambia wafanye chochote ambacho Yesu angewaambia. Walifanya na walipewa divai na wale waliohusika waliokolewa kutokana na kushindwa kutimiza majukumu yao.

Yesu pamoja na mwanamume na mtoto

Kama tupo radhi kufanya lolote Yesu analosema, Yeye anaweza kufanya miujiza katika maisha yetu.

Zeri ya Gileadi, na Annie Henrie Nader, isinakiliwe

Kama tupo radhi kufanya lolote Yesu analosema, Yeye anaweza kufanya vivyo hivyo kwa ajili yetu na kufanya miujiza katika maisha yetu (ona Waebrania 10:35–36). Kuokolewa ni muujiza mkubwa mno kupita miujiza Yake yote na unahitaji utiifu kwa sehemu yetu (ona Mafundisho na Maagano 14:7; Makala ya Imani1:3).

3. “Nao wakayajaza hata juu”

Mwokozi aliwaelekeza watumishi kujaza mabalasi sita ya mawe kwa maji. “Nao wakayajaza hata juu” (Yohana 2:6–7).

Wakati wataalamu wamependekeza viwango tofauti, labda ni salama kusema kwamba kila balasi lilichukuwa magaloni kadhaa. Kama ni vigumu mno kugeuza galoni moja au magaloni 100 ya maji kuwa divai, sijui. Kile kilichobadili maisha yangu ni wazo kwamba Yesu ana uwezo wa kubadili kitu kimoja kuwa kitu fulani tofauti kabisa. Hakufanya tu maji yenye ladha ya divai; alichukuwa maji, na umbile lake la molekyuli ya kawaida na kuyageuza kuwa divai, mchanganyiko usioelezeka kwa urahisi wa mamia ya mchanganyiko wa kemikali.

Kama anaweza kufanya hilo, basi anaweza kugeuza changamoto zangu kuwa baraka—siyo tu kuongeza bitana ya fedha katika tufani bali kiuhalisia kubadili dutu ya majaribu kuwa kitu fulani ambacho kinanibariki mimi (ona Warumi 8:28; 2 Nefi 2:2).

Na kama anaweza kufanya kwa changamoto moja, anaweza kufanya kwa zote. Kwa hiyo wakati maisha yanaonekana kujazwa hata juu kwa majaribu, kumbuka kwamba anaweza kuyageuza maji kuwa divai. Anaweza kubadilisha majivu kuwa maua (ona Isaya 61:3). Anaweza kuchukuwa uovu na kuugeuza kuwa wema (ona Mwanzo 50:20). Anaweza kuyageuza makosa yangu kuwa ukuaji na kuchukuwa dhambi zangu na kuzigeuza kutoka kuwa laana na kuwa maendeleo.3

Na, kwangu mimi, utambuzi huo ni wa kipekee zaidi ya yote. Muujiza huu ambao mwanzo sikuutilia maanani umenifunza kwamba kupitia uwezo Wake, kama tuna imani ya kufanya kile anachotutaka tufanye, Anaweza kutubadilisha sisi kutoka kile tulichokuwa na kuwa kwenye kile tunachoweza kuwa—kama Yeye.

Muhtasari

  1. Ona Peter J. Sorensen, “The Lost Commandment: The Sacred Rites of Hospitality,” BYU Studies, vol. 44, no,1 (2005), 4–32.

  2. Ona Kamusi ya Biblia, “Miujiza.”

  3. Ona Bruce C, Hafen, “Upatanisho: Wote Kwa ajili ya Wote,” Liahona, Mei 2004, 97–99.