“Lugha ya Roho,” Liahona, Jan. 2023.
Sauti za Watakatifu wa Siku za Mwisho
Lugha ya Roho
Nilijifunza kwamba Roho anaweza kutusaidia kuelezea upendo wa Baba wa Mbinguni, hata wakati tunapohisi hatutoshi.
Nilizoea kutumia nyakati za majira ya joto kusafiri kupita Ulaya yote na timu ya dansi. Hadhira yetu, maonyesho yetu na viwango vya nguvu vilikuwa tofauti, lakini tulikuwa na desturi moja ambayo siku zote ilibaki vile vile: tulifunga kila onyesho kwa kuimba “Mungu Awe Nanyi Hadi Tutakapokutana Tena”1 katika lugha ya nchi tuliyokuwa tumeitembelea. Kwa sababu wengi wa washiriki kwenye timu yangu ya dansi walikuwa wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, tuliipenda desturi hii. Ilikuwa njia ya kupendeza ya kuunganika na hadhira yetu na kushiriki upendo wa Baba wa Mbinguni.
Karibu na mwisho wa safari hizi, ndio kwanza tulikuwa tumevuka mpaka wa kuingia Ujeremani na tulikuwa tukifanyia mazoezi wimbo wa Kijeremani kwa ajili ya maonyesho yetu yajayo. Lakini katika kuwasili, tuligundua kwamba eneo hili maalum la Ujeremani walizungumza Kisobiani, lahaja ambayo ilikuwa na mfanano kidogo na wimbo tuliokuwa tumeufanyia mazoezi kwa uaminifu.
Tukiwa ndani ya basi kuelekea kwenye onyesho letu, nilikuwa nimechoka na nilitaka kulala tu muda wote wa safari. Lakini wakurugenzi wetu walikuwa na mawazo mengine. Walikuwa wamewaomba waongozaji wetu kutafsiri wimbo wa Kanisa kwa Kisobia. Sasa walitaka basi zima lenye wafanya onyesho zaidi ya nusu waliosinzia kujifunza wimbo masaa machache tu kabla ya onyesho.
Tulifanya vyema kadiri tulivyoweza. Mwishoni mwa onyesho, tulisimama pamoja mbele ya jukwaa na tukaanza kuimba. Nakumbuka kuhisi kushangazwa wakati maneno yasiyoeleweka niliyoyachanganya masaa machache kabla yalikuja kiurahisi akilini mwangu. Nilihisi wasiwasi wangu wa mwanzo kuhusu utayari wetu wa kuimba ukipotea kadiri nilivyomtegemea Roho kunikumbusha maneno.
Hadhira ilionekana kushangazwa na kisha ikasisimka. Wakati wimbo ulipokwisha, mkusanyiko ulikaa kimya. Kisha walisimama na kuanza kuimba wimbo kwa ajili yetu, ambao baadaye walieleza kwamba ulikuwa wimbo wa shukrani ambao kwa kawaida waliuhifadhi kwa ajili ya matukio muhimu.
Nilimhisi Roho kwa nguvu katika wakati ule, japokuwa sikuweza kuelewa kitu walichokuwa wakiimba. Nilikuwa na shukrani kubwa kwamba Bwana alinisaida kuelezea upendo wake licha ya hisia zangu za kutotosha. Nilikumbushwa kwamba upendo wa Baba wa Mbinguni ni ujumbe kwa watu wote. Bila kujali tofauti zozote tunazoweza kuwa nazo, sisi wote tunaweza kuielewa lugha ya Roho.