2023
Kuwa Pale kwa ajili ya Kijana Wako
Januari 2023


“Kuwa Pale kwa ajili ya Kijana Wako,” Liahona, Jan. 2023.

Sauti za Watakatifu wa Siku za Mwisho

Kuwa Pale kwa ajili ya Kijana Wako

Baada ya Roho kuzungumza na Baba yangu wakati wa kutawazwa kwangu katika ukuhani, aliyageuza maisha yake.

mvulana akiwa anatawazwa

Vizazi Vinne, na Kwani Povi Winder

Nilikuwa mhudhuriaji kamili katika Kanisa wakati mjomba wangu Bill alipowachukuwa dada zangu wawili pamoja na mimi kwenda darasa la Msingi. Mwalimu wangu wa Msingi, Jean Richardson, alikuwa mwalimu mwenye ukarimu wa mfano wa mama. Nilimpenda yeye na rafiki zangu wapya wa Kanisani, ambao walikuwa wakarimu zaidi kwangu kuliko watoto wa mtaani kwangu. Kwa hiyo, niliamua kubaki Kanisani.

Nilipokuwa nikikaribia kumbukizi ya miaka 12 ya kuzaliwa, Askofu Dal Guymon alinialika kupokea Ukuhani wa Haruni na kutawazwa kama shemasi. Sikuwa na uhakika hilo lilimaanisha nini, lakini nilisema ndiyo. Kisha alisema, “Kwa nini usimuombe baba yako akuleta hapa Jumapili ijayo, na sisi tutakutawaza.”

Baba na familia yake waliacha kuhudhuria kanisani wakati alipokuwa na miaka 13. Kama mtu mzima, alitumia karibu wikiendi zake zote katika vilabu vya mtaani au kuvua samaki kwa nzi bandia. Alikuwa amehudumu katika Kikosi cha Jeshi la Wanamaji la Marekani wakati wa vita kuu ya pili na Vita vya Korea. Alivuta biri, alikunywa pombe na kuapa, lakini alikuwa na sifa katika mji wetu mdogo wa Montana kwa kuwa mwaminifu na mtenda haki.

Wakati Baba aliponipeleka kanisani Jumapili iliyofuata lilikuwa jambo kubwa. Muda ulipofika, Askofu Guymon aliniita nisimame na alinitaka kukaa mbele kwenye kiti. Wanaume kadhaa—lakini siyo baba yangu—waliweka mikono yao kichwani kwangu na kunifanyia ibada.

Nilihisi uzito mkubwa wa mikono kadhaa mikubwa juu yangu. Baba, akiwa amekaa juu ya benchi futi chache mbali nami, alihisi aina fulani ya msukumo tofauti—ndani ya kifua chake. Sauti ilizungumza naye ndani, ikisema, “Unahitaji kuwa pale kwa ajili ya mtoto wako wakati mwingine hili linapotokea.”

Katika wiki ambazo zilifuata, Baba aligeuza maisha yake na alianza kuhudhuria kanisani kila jumapili. Punde, Kanisa likawa fokasi kubwa ya maisha ya familia yetu.

Baba akawa mshauri wa akidi zangu za mashemasi, walimu na akidi za makuhani; mwalimu wangu wa shule ya Jumapili na kocha wangu wa mpira wa kikapu, softball na voliboli. Wakati tulipokuwa wenza wa kufundisha nyumbani, baba aliwasaidia wanaume wengine na familia kurudi kwenye shughuli za Kanisa.

Nikisaidiwa na baba yangu, nilipata uzoefu wangu binafsi na mabadiliko ya uongofu. Tangu hapo, nimejaribu kuwa mwepesi kuhisi kwa watu ambao kama vile baba yangu, wangeweza kuitikia mwaliko wa kuwa baba mwema kadiri wanavyoweza kuwa.

Nitakuwa mwenye shukrani milele kwa kile mjomba wangu Bill, mwalimu mkarimu wa Msingi, askofu mwenye hekima na baba yangu walichonifanyia miaka 60 iliyopita.