“Kupitia Magumu katika Mahusiano,” Liahona, Jan. 2023.
Kupitia Magumu katika Mahusiano
Majaribu ya Kifamilia yanaweza kutatuliwa kama tupo tayari kutafuta msaada wa Bwana ili kubadilika na kuwa bora.
Kupitia changamoto katika mahusiano yetu ya familia kunaweza kutujaribu mpaka kikomo cha hisia zetu. Kama mtaalamu wa matibabu, niliona hali nyingi za kuumiza moyo. Lakini pia nilishuhudia baraka katika maisha ya wale waliokabiliana na majaribu ya familia kwa kutafuta msaada wa Bwana ili kuboresha mawasiliano yao, kuongeza mapenzi yao na uelewa na kufanya kazi pamoja ili kufanya mabadiliko muhimu. Pamoja na msaada wa Bwana, walipata nguvu ya kukua kupitia matatizo yao.
Mawasiliano kama ya Kristo yanaweza kuleta upendo na uelewa.
Tom na Joan (majina yamebadilishwa) wote walikuwa wamewapoteza wenzi wao. Mke wa Tom alifariki kutokana na saratani na mume wa Joan, kwa sababu ya kutawaliwa na uraibu, aliondoka kwa ajili ya mahusiano mengine. Tom na Joan walikutana kwenye mkutano wa waseja na walikuwa wanategemea kuoana.
Kila mmoja wao alikuwa na watoto, wenye umri wa miaka 15 na chini ya hapo. Familia zao zilikuwa zimeenda kwenye miadi kadhaa ya pamoja na wote Tom na Joan waliweza kuona kuwepo na matatizo katika kuchanganya familia. Walikuja kwenye ushauri kwa ajili ya mawazo ya jinsi ya kuwasiliana kwa njia zenye tija ili kupita ukurasa huu mpya wa maisha yao.
Nilipendekeza wapitie upya ujumbe juu ya mabaraza ya familia uliotolewa na Rais M. Russell Ballard, Kaimu Rais wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili. “Watoto wanahitaji sana wazazi ambao wako tayari kuwasikiliza,” alifundisha, “na baraza la familia linaweza kutoa muda ambapo wanafamilia wanaweza kujifunza kuelewana na kupendana.”1
Kwa ajili ya mabaraza yao ya familia, waliamua juu ya ajenda zifuatazo:
-
Fafanua tatizo.
-
Jadiliana kupata suluhisho.
-
Chagua mpango.
-
Ufanyie kazi.
-
Tathmini mafanikio ya mpango juma linalofuata na jadiliana upya mpango kama ni muhimu.
Kwa nyongeza ya kushauriana pamoja kama familia, Tom na Joan walijifunza kwamba wakati msongo wa mahusiano unapokuwa juu, kunaweza kuwa na hitaji la kujifunza jinsi ya kuboresha mawasiliano ya mmoja na mwingine.
Tom na Joan walijifunza mbinu kadhaa ambazo ziliwasaidia kuboresha mawasiliano yao na mahusiano yao pamoja na watoto wao.
-
Wazazi walisimama pamoja katika kutafuta suluhisho la matatizo pamoja na watoto.
-
Kama mtoto alikuwa na ugumu wa kumaliza kazi zao za kila siku, mmoja wa wazazi angetumia muda pamoja nao, wakijadiliana juu ya siku hiyo wakati wakisaidiana pamoja kumalizia ile kazi.
-
Walitumia muda kila wiki wakiimarisha mahusiano yao na kila mtoto.
-
Walijiwekea mapema kabla ya muda kwamba wangechukua muda wa kupumzika wakati “hisia” ya akili (hasira) ingetawala dhidi ya akili yenye fokasi ya suluhisho “linalofaa,” (mjadala).
-
Wakati wowote ulipokuwapo mvutano wa mamlaka kati ya mzazi na mtoto, mzazi huyo, anapokuwa amepata msukumo kufanya hivyo, aliondoka na kurudi baadaye ili kutafuta mbinu ya suluhisho jipya.
Wakati familia ilipofanya kwa uwezo wao wote kulikabili jambo katika uhusiano wenye changamoto katika njia za uaminifu na zenye tija—wakiwasiliana kuhusu changamoto zao na kuzifanyia kazi kwa pamoja—Tom na Joan waligundua ukuaji muhimu kwa watoto wao pia kwao wenyewe.
Uelewa na upendo vinatuleta pamoja karibu zaidi
Watoto wanapokuwa watu wazima, siku zote hawafanyi chaguzi ambazo tungetamani wafanye. Jinsi gani tunashughulikia hali kama hizo? Jinsi gani tunaweza kudumisha au hata kuimarisha mahusiano yetu ili kwamba tuweze kuendelea kuwa wenye msaada na ushawishi chanya katika maisha yao?
Terry na Bruce walikuja ofisini kwangu muda mfupi baada ya Terry na mwana wao Seth, kugombana kwenye simu. Seth alikuwa mbali shuleni kwa miaka mitatu. Alikuwa amepatwa na ugonjwa hatari na alikuwa bado hajaruhusiwa kutoka katika uangalizi wa daktari. Kwa sababu ya ugonjwa wake, hakuweza kuhudumu misheni. Terry na Bruce hawakujua wapi ushuhuda wake ulikuwa au hata ikiwa alihudhuria kanisani. Walikuwa na wasiwasi kwamba Jolyn, rafiki mpya msichana wa Seth, hakuwa aina ya ushawishi ambao wangetamani kwa ajili ya maisha ya Seth. Wazazi wote walikuwa wamefadhaishwa kuhusu njia aliyokuwa anaifuata.
Tulipokuwa tukizungumza kuhusu nini wangeweza kufanya, tulijadili kuhusu fumbo la kondoo aliyepotea. Mchunga kondoo yawezekana alikuwa akisikiliza kulia kwa kondoo kabla hajampata, kumpenda na kumrudisha kundini (ona Luka 15:6). Terry na Bruce waligundua kwamba wasingeweza kumbadili Seth, lakini waliamua kujaribu kumsikiliza, kumpenda na kumwalika nyumbani. Hawakuweza kumchagulia mke wake au njia ya maisha kwa ajili yake, lakini wangeweza kumkumbusha juu ya upendo wa familia yao kwa ajili yake na kwa ajili ya injili.
Terry alimpigia simu Seth na aliomba radhi kwa mabishano. Alimsikiliza tu wakati Seth alipokuwa akimwambia kwamba alifedheheshwa kwa sababu hakuweza kuhudumu misheni. Alijiuliza ni jinsi gani yeye angeweza kuwa na miadi na msichana wa kanisani. Waliwaalika Seth na Jolyn nyumbani wakati wa mapumziko ya shule.
Seth na Jolyn walikuja. Dada zake Seth waliwakumbatia wawili wale. Wazazi wote walipenda kuwa na Seth nyumbani na walimwambia hivyo. Terry na Bruce walijiunganisha mara kwa mara na Seth. Terry alituma ujumbe mara kadhaa kwa wiki. Familia ilikuwa na mkutano wa video kila Jumapili. Baba wa Seth alitumia muda kucheza gofu na kuvua samaki pamoja na Seth. Ilitokea pole pole, lakini Seth alichukuliwa upya ndani ya familia. Hatimaye, Seth aliamua kwamba njia iliyochaguliwa na Jolyn ilikuwa siyo sahihi kwake. Baadaye alimwoa mwanamke mzuri ambaye yeye mwenyewe alimbatiza.
Terry na Bruce walimpata mwana kondoo wao aliyepotea kwa kusikiliza, kumpenda na kumwalika arudi katika kundi.
Kufanyia kazi mabadiliko kwa pamoja kunaweza kuimarisha mahusiano na kuhamasisha ukuaji
Marie na mumewe, David, wameoana kwa miaka mingi na walikuwa washiriki walioheshimiwa katika jumuiya yao. Lakini siku moja Marie aliambiwa, bila David kujua, kwamba David alikuwa na mahusiano na mwanamke mwingine.
Marie alikuja ofisini kwangu, akihisi mchanganyiko wa hasira, huzuni na masikitiko. Alipokuwa akilia huku akisimulia hadithi yake, alijua alihitaji kumwambia David jinsi alivyokuwa akihisi lakini sio kwa njia ya hasira, ili kwamba Roho aweze kuwa pamoja nao.
Baada ya maandalizi ya sala, alimwambia David kuwa alimpenda lakini kwamba alikuwa amevunjika moyo kujua juu ya mahusiano yake na mwanamke mwingine. Wangehitaji kukutana na askofu na kufikiria majaliwa ya ndoa yao. David hakutaka kumpoteza mke wake au familia yake. Kwa msaada wa askofu, alianza mchakato wa toba.
Marie alijua kwamba kulikuwa na vitu kila mmoja wao angehitajika kufanya ili kupata uponyaji binafsi na kama wanandoa. Marie alimwomba David kukaa kwa wazazi wake kwa muda wakati akichanganua vyema hisia zake. Alitumia muda hekaluni, akimwomba Bwana msaada. Alibaki katika tiba, akiimarisha ujuzi wake wa mawasiliano na kujifunza kuweka mipaka sahihi.
Kwa pamoja, Marie na David:
-
Walisoma maandiko kila usiku.
-
Walisali.
-
Walielezana yale yaliyotokea kila siku.
-
Walikuwa na miadi ya usiku mara moja kwa wiki.
Waliwasiliana kwa uwazi zaidi. Marie alisema kile alichofikiria, na David alisikiliza. Walianza kuzungumza kama vile walivyokuwa wakati walipooana kwa mara ya kwanza.
Marie aliripoti kwamba haikuwa tu David aliyebadilika; yeye pia alibadilika. Alijihisi mwenye nguvu zaidi na mwenye kujiamini zaidi. David alibaki mwenye kutubu na alirudi nyumbani.
Kumjumuisha Bwana katika maisha yao ya kila siku kulileta tumaini kubwa na upendo kwenye mahusiano yao. Wote walihisi kwamba juhudi ya kushinda changamoto hii kwa msaada wa Bwana ilikuwa imewaimarisha.
Maneno ya Kristo yatatuongoza
Tunapopitia mahusiano magumu ya kifamilia, sote tukumbuke kukaa katika baraza pamoja na Bwana. Wakati mwingine Yeye atatuambia nini cha kufanya. Wakati mwingine tunaweza kuchagua. “Si vyema kwamba niamuru katika mambo yote” (Mafundisho na Maagano 58:26). Lakini kuna nyakati zingine ambapo inatulazimu tujisalimishe wenyewe kwa Bwana. Kama tutaitunza taswira ya milele, utajiri wa milele utakuwa wetu, “na mambo yote yatafanyika kwa pamoja kwa faida [yetu]” (Mafundisho na Maagano 90:24).