“Unyanyasaji, Kuasiliwa—na Uponyaji,” Liahona, Jan. 2023.
Vijana Wakubwa
Unyanyasaji, Kuasiliwa—na Uponyaji
Familia yangu ilikuwa ya unyanyasaji na yenye vurugu, lakini kupitia Kristo, sasa ninalo tumaini kwa familia yangu ya baadaye.
Nimekulia katika mazingira yenye vurugu. Wazazi wangu wa kibaiolojia walininyanyasa na kunitelekeza na nilipitia changamoto nyingi ngumu. Nilipambana na wasiwasi, suala la taswira ya mwili, kutokuwa na hamu ya kula na hali ya mfadhaiko ambayo ilifanya niwe mfungwa kwa miaka mingi.
Wazazi wangu wa kibaiolojia walikuwa wameunganishwa ndani ya hekalu, lakini mara baada ya mimi kubatizwa nikiwa na miaka minane, walianza kujitenga mbali na Kanisa. Na kadiri walivyozidi kujitenga mbali na maagano yao, ndivyo hali yetu ilivyozidi kuwa mbaya.
Katika umri wa miaka 14, nilikuwa mtunzaji wa mdogo wangu mwenye ugonjwa wa akili na mama yangu. Nilikuwa nimepotea na aliyeshindikana. Nilijichukia mwenyewe na hali yangu na niliamini maisha yangu kamwe hayatabadilika.
Lakini kisha muujiza ulitokea. Mama yangu wa kibaiolojia alitambua kuwa hangeweza kunitunza mimi na alimpigia simu kaka yake huko Singapore kumuuliza kama angeweza kuniasili. Nikiwa na mabegi yaliyofungashwa na machozi machoni, nilipanda ndege kwenda kuanza maisha mapya—huru kutokana na unyanyasaji. Lakini kujirekebisha ili kufanana na familia yangu iliyoniasili na utamaduni mpya ilikuwa vigumu na nilipambana ili kusonga mbele.
Wazazi wangu walioniasili walifanya kila kitu walichoweza ili kunisaidia. Niliwaona wataalamu na madaktari. Pia nilianza kwenda kanisani tena, lakini kujifunza kuhusu Baba wa mbinguni ambaye ananipenda na ana kusudi kwa ajili yangu ilikuwa vigumu, kwa sababu sikuliamini hilo baada ya yote niliyokuwa nimevumilia.
Sikuwa na furaha. Sikujua jinsi ya kupona kutokana na yaliyopita na bado nilijihisi nisiye na tumaini kuhusu yajayo.
Kutamani Kupona
Siku moja, nilikuwa natafakari kuhusu jinsi gani maisha ya duniani yalivyo mafupi. Sikutaka kutumia maisha yangu bila furaha. Nilihitaji kujifunza kutokana na majaribu yangu, kutumia kanuni za injili nilizokuwa nimefundishwa na kumwalika Kristo katika maisha yangu.
Nilichukua hatua ya imani na nilianza kupiga magoti na kumwomba Baba wa Mbinguni kila siku kwa ajili ya nguvu ya kuwasamehe wazazi wangu wa kibaiolojia, kubadili woga wangu kuwa imani, kupata uponyaji na furaha pamoja na kutambua upendo katika maisha yangu. Nilikwenda kwenye chuo cha Kanisa na kuanza kujifunza maandiko na kutumia kweli za injili katika maisha yangu.
Kwa kweli nilitafuta nguvu ya uponyaji ya Yesu Kristo na Upatanisho Wake. Na baada ya muda, maisha yangu yalianza kubadilika. Kadiri nilivyokuwa mvumilivu, kadiri nilivyopokea matibabu ya wataalamu na madawa, na kujaza maisha yangu kwa Roho kila siku, nilianza kupona: Nilihisi kujichanganya zaidi na kuwa zaidi mimi. Nilijihisi salama. Niliwahudumia wengine. Nilipenda, nilisamehe na kujikubali mwenyewe. Nilijenga mahusiano yenye afya na yenye upendo. Nilianza kuhisi upendo wa Baba wa Mbinguni kwangu. Na kwa mara ya kwanza maishani mwangu, nilihisi furaha ya kweli.
Kristo Anatoa tumaini kwa ajili ya Siku Zetu za Baadaye
Siwezi kubadili mambo yangu yaliyopita, lakini kama Mafundisho na Maagano 122:7 inavyosema, “mambo haya yote yatanipa [mimi] uzoefu, na yatakuwa kwa faida [yangu].” Ninajua sasa kwamba Mwokozi alinisaidia wakati wote wa juhudi zangu. Licha ya hayo, nimekua sana kwa sababu ya tamaa yangu ya kubadilika na kwa sababu ninaendelea kumgeukia Yeye.
Kama upo katika hali ngumu kifamilia, jua kwamba unaye Baba Mbinguni anayekujua wewe na anakupenda wewe na atafungua milango kwa siku za baadaye zenye mafanikio. Kabla ya kuasiliwa, nilijiambia mwenyewe kwamba hali zangu kamwe haziwezi kubadilika, na kwamba sitaweza kamwe kuolewa au kuwa na watoto kwa sababu nilikuwa mwoga kwamba wangeteseka kama nilivyoteseka. Lakini nimejifunza kwamba bila kujali mahangaiko tuliyopitia katika familia zetu, tunapomtafuta Kristo, tunaweza kujenga nyumba zetu za baadaye na familia za milele kwa tumaini, kweli za injili na upendo.
Kama Mzee Clark G. Gilbert wa wale Sabini alivyofundisha: “Sisi sote … tunaanza katika sehemu tofauti tukiwa na endaumenti tofauti za maisha. Wengine huzaliwa na kuchangamana kwa hali ya juu, kulikojaa fursa tele. Wengine wanakabiliwa … na mazingira ambayo yana changamoto. … Kisha tunaendelea kwenye mteremko wa maendeleo binafsi. Baadaye yetu itaamuliwa kidogo sana na mahali petu pa kuanzia na itaamuliwa zaidi na mteremko wetu. Yesu Kristo anaona uwezekano wa kiungu bila kujali wapi tunaanzia. … Atafanya kila kitu awezacho kutusaidia kugeuza miteremko yetu ielekee mbinguni.”1
Vyovyote ziwavyo hali zako, kuna tumaini na uponyaji unaopatikana kwa Yesu Kristo! Yeye yupo pamoja nawe na atakuongoza kwenye usalama na furaha pale unapomtafuta Yeye—daima.