“Familia na Nuru ya Ulimwengu,” Liahona, Jan. 2023.
Kwa ajili ya Wazazi
Familia na Nuru ya Ulimwengu
Wapendwa Wazazi,
Familia ni sehemu muhimu ya mpango wa furaha wa Baba wa Mbinguni kwa ajili ya watoto Wake. Makala katika toleo la mwezi huu zinaweza kukusaidia kuboresha mawasiliano ndani ya familia na kusaidia kuzitatua changamoto katika mahusiano ya kifamilia. Unaweza pia kutumia toleo hili kukusaidia kuwafundisha watoto baadhi ya masomo muhimu kutoka Agano Jipya.
Majadiliano ya Injili
Yesu Kristo ni Nuru Yetu ya Kweli
Shiriki na familia yako baadhi ya mafundisho kutoka katika makala ya Rais Ballard kwenye ukurasa wa 4 kuhusu jukumu la Yesu Kristo kama Nuru ya Ulimwengu. Kama familia, tengenezeni orodha ya vyanzo mbalimbali vya nuru ndani ya nyumba yenu na jadilini mambo mbalimbali ambayo nuru inafanya kwa ajili yetu. Ni kwa njia gani Yesu Kristo, kama chanzo kikubwa zaidi cha nuru ya kiroho, anatusaidia sisi?
Mawasiliano ya Wazi katika Familia
Ni muhimu kuwa umejiandaa kiroho kwa ajili ya changamoto za maisha. Kwenye ukurasa wa 12, soma baadhi ya ushauri kutoka kwa mshauri wa afya ya akili juu ya jinsi ya kuwa na mazungumzo muhimu, na yenye kuimarisha kwa watoto wako. Ni mawazo na mapendekezo gani kati ya haya ungeweza kuyatekeleza pamoja na familia yako?
Kuiandaa Mioyo Yetu kwa ajili ya Neno
Soma makala ya Kaka Camargo kwenye ukurasa wa 38 kuhusu fumbo la mpanzi. Jadiliana na familia yako aina mbalimbali za udongo katika fumbo hili zinaashiria nini. Watoto wadogo wangeweza kuchora vitu kutoka kwenye fumbo na kuzungumza kuvihusu, na watoto wakubwa wangeweza kulisoma fumbo katika Marko 4:3–20 na kushiriki mawazo yao au maswali yao.
Njoo, Unifuate Burudani ya Familia
Kufanya Mambo Magumu kwa Msaada wa Mungu
Kama Mariamu na binamu yake Elisabeti katika Agano Jipya (ona Luka 1:5–55), wakati mwingine tunaombwa kufanya mambo magumu na tunaweza kujiuliza kama tunaweza.
-
Weka chombo kitupu, kama vile ndoo au boksi, mwisho wa chumba.
-
Mpe kila mwanafamilia unyoya.
-
Kuanzia kwenye mwisho wa chumba mkabala kutoka kwenye chombo, mtake kila mwanafamilia kujaribu kuliweka nyoya lake ndani ya chombo kwa kulipuliza hewani wanapopita chumbani.
-
Kufanya iwe ya kushindana zaidi, ruhusu sekunde 30 tu, na tumia mrija kupuliza hewa kwenye nyoya. Endelea kupunguza muda uliowekwa mpaka shughuli iwe isiyowezekana.
Majadiliano: Weka akilini kwamba baadhi ya changamoto zinaweza zisiweze kutatuliwa katika maisha haya, shiriki uzoefu ambao uliimarisha ushuhuda wako kwamba “Yasiyowezekana kwa wanadamu yawezekana kwa Mungu” (Luka 18:27) Ni hatua zipi ndogo ndogo unaweza kupiga kila siku ili kukamilisha majukumu yanayoonekana hayawezekani katika maisha yako?