“Kuelekea kwenye Siku Angavu Zaidi,” Kwa Ajili ya Nguvu Kwa Vijana, Jan. 2023.
Msaada wa Kimaisha
Kuelekea kwenye Siku Angavu Zaidi
Tumaini, msaada na uponyaji vinapatikana kwa wale walionusurika unyanyasaji.
Wakati mmoja nilisafiri kwa ndege kutoka eneo lililojaa moshi uliotokana na motopori uliokuwa jirani. Ndege ilipokuwa inaanza kupaa, tulipasua anga lililofunikwa na hewa yenye majivu tukiingia anga lililo safi, na lenye jua angavu. Nilitambua kwamba jua angavu na hewa safi vilikuwepo hapo wakati wote, lakini uwezo wangu wa kuvifurahia ulikuwa umezuiliwa na kitu kilichokuwa nje ya udhibiti wangu. Motopori ule haukuwa kosa langu, lakini bado ulikuwa umeathiri maisha yangu.
Unyanyasaji ni kama hilo. Wale wanaopitia unyanyasaji hawapaswi kulaumiwa kamwe, lakini bado wanalazimika kukabiliana na athari zake. Unyanyasaji unaweza kutia kiwingu hisia zetu juu ya ustahili wetu na kufanya iwe vigumu kuhisi upendo wa Mungu. Inaweza kuchukua muda kwa mwathirika kujichomoa kwenye wingu la uwongo wa Shetani na kujiunga tena na kweli za milele. Lakini tumaini, msaada na uponyaji vinapatikana katika kila hatua ya njia!
Hadithi Moja
Baba yake Stacie1 alikuwa mnyanyasaji. Alimwambia yeye hangekuwa mzuri katika lolote atakapokuwa mkubwa. Alimfanya ajihisi kuwa hana thamani.
Stacie alipoondoka nyumbani kwa ajili ya kwenda chuoni, aliweza kufikiri kwa uwazi zaidi. Alianza kwenda kanisani tena na kuhisi upendo wa Mungu kwake na kwa familia yake. Baada ya muda, alipata ongezeko la amani katika injili na katika uhusiano wake na Mwokozi.
Inakadiriwa kuwa watoto wapatao bilioni moja ulimwenguni kote watapitia aina fulani ya unyanyasaji katika mwaka huu.2 Yawezekana ikawa wewe au wengine unaowajua wanapitia uzoefu huu kama wa Stacie. Nyenzo zifuatazo zinaweza kusaidia.
Kama Wewe Unapitia Unyanyasaji
Kama wewe unaumizwa, tafadhali mwambie mtu kuhusu kile kinachokutokea. Jua kwamba Mungu anakupenda! Na wanafamilia waaminifu, marafiki, na waumini wa Kanisa katika maisha yako wanakupenda pia. Watasimama upande wako na kukusaidia ulishinde hili.
Na tafadhali kumbuka, “Unyanyasaji huo haukuwa, na siyo, na kamwe hautakuwa kosa lako. … Wewe siye anayehitajika kutubu; wewe huwajibiki.”3
Dkt. Sheldon Martin, tabibu bingwa wa Huduma za Familia katika Kanisa, anasema inaweza kuwa ya msaada kwa waathirika kufokasi juu ya kweli zao za milele zilizopita, zilizopo, na zijazo.
-
Zilizopita: “Watu wengi kuliko unaowajua wanajali kukuhusu wewe,” Dkt. Martin anasema, akionyesha kwamba kwanza na zaidi ya yote wewe ni mtoto wa wazazi wa mbinguni. Familia yako ya milele imetawanyika kupita uhusiano wako wa kidunia. Na kwa kuongezea kwenye nguvu na faraja kutoka kwa Baba wa Mbinguni, Yesu Kristo na Roho Mtakatifu, unao mababu upande mwingine wa pazia ambao wanakujali wewe na yawezekana wakakuhudumia.
-
Zilizopo: “Ni SAWA kujipenda mwenyewe jinsi ulivyo sasa,” Dkt. Martin anasema, bila kujali mahali ulipo katika mchakato wa uponaji. Ni kawaida kujisikia hasira, kuvunjika, au kukanganyikiwa. Kuwa mvumilivu kwako wewe mwenyewe.
-
Zijazo: “Mambo yatakuwa mazuri zaidi,” Dkt. Martin anasema. “Ninajua hili kwa sababu ninamjua Mwokozi. Yeye anakujali.” Fanya kile uwezacho ili kukaa karibu na Yeye. Ufanyapo hivyo, utakuwa na uwezo wa kujiweka mbali na uhusiano wenye sumu huku ukiongeza uwezo wa kuhisi amani na upendo Wake.
Ikiwa Unadhani Rafiki Anapitia Unyanyasaji
-
Waulize bayana, “Je, kuna mtu anakuumiza?”
-
Sikiliza kwa makini kile wanachosema. Waonyeshe ukarimu na huruma.
-
Mwambie mtu anayeweza kusaidia, kama vile mwalimu, mzazi, mshauri wa shule au kiongozi wa Kanisa.
-
Endelea kuwa rafiki yao. Watendee kama kawaida. Wasaidie kutengeneza urafiki mwingine mzuri.
Endelea Kusonga Mbele
Leo, Stacie ni mtaaluma mwenye mafanikio mwenye familia yake yenye upendo. Baadhi ya siku bado ni ngumu, lakini anajisikia mwenye furaha tele na mwenye msamaha kwa wengine.
“Ninajua kwamba Yesu Kristo anaweza kuponya vidonda vyetu vyote,” Stacie anasema. Kama kuna kitu kimoja ambacho angeshiriki na waathirika wengine, ni kuishi kwa tumaini.
“Daima kuna tumaini katika Kristo” anasema, “hata katikati ya majaribu ambayo yanaonekana kama vile hayatakuwa na mwisho.”
Bila kujali changamoto unazopitia, endelea kusonga mbele. Yajaze maisha yako kwa wema na imani katika njia yoyote unayoweza. Siku angavu zaidi ziko mbele yako!