“Wakati mwingine nafikiri wazazi wangu wanazidisha ukosoaji juu yangu. Ninawezaje kuwajibu kwa heshima?” Kwa Ajili ya Nguvu Kwa Vijana, Jan. 2023.
Maswali na Majibu
“Wakati mwingine nafikiri wazazi wangu wanazidisha ukosoaji juu yangu. Ninawezaje kuwajibu kwa heshima?”
Tumieni Muda Pamoja
Wazazi wako wanatoa ushauri na masahihisho kwa sababu wanakupenda na wanataka kukusaidia ili ufanikiwe. Wakati masahihisho hayo yanapoonekana kutokuwa ya haki, pata muda wa kujadiliana uso kwa uso na wazazi wako katika wakati ambapo ninyi wote mmetulia. Unaweza kupata muda wakati ninyi yote mnafanya kitu mnachopenda kukifanya pamoja, kama vile kupika au kufanya mazoezi. Hii inasaidia kumwalika Roho katika maongezi yenu.
Rebekah M., 17, Maryland, Marekani
Kumbuka kuwa Wanakupenda
Kama utakumbuka kwamba wazazi wako wanakusahihisha na kukushauri kwa sababu wanakupenda, ni rahisi zaidi kukubali masahihisho yao. Kusema sala fupi ya haraka ili kumwomba Roho akusaidie kubaki mwenye heshima na mnyenyekevu kutakusaidia wewe kuwasiliana nao vyema zaidi.
Lauren M., 16, Texas, Marekani
Uaminifu Unaponya
Maongezi mazuri na ya uaminifu yanaweza kutatua aina zote za migogoro. Kaa chini na wazazi wako na uongee nao. Waambie kile kinachokuumiza na sikiliza kile kinachowahuzunisha au kuwakatisha tamaa. Tumia muda zaidi pamoja nao na palilia upendo na amani katika uhusiano wenu na nyumbani kwenu. Unapokuwa umekasirika, mwombe Baba wa Mbinguni ili autulize moyo wako.
Rafaella P., 17, São Paulo, Brazil
Waambie Kuwa Unawapenda
Unaweza kujibu kwa heshima, hata kama ni vigumu. Waambie wazazi wako kuwa unawapenda, kwamba unajali kuwahusu wao na kwamba unajua kuwa wanakupenda. Acha wajue kuwa kile wanachosema kinaumiza hali yako ya kihisia, kiroho, na kiakili. Sali kila mara. Baba wa Mbinguni hakika atakusaidia.
Wellie S., 13, Luanda, Angola
Wao Wanaona Uwezekano Wako
Mungu anategemea yaliyo bora zaidi kwetu na anaweza kuona uwezekano wetu wa kweli. Hii ndio sababu anataka mengi kutoka kwetu. Wazazi wako pia wanaona uwezekano wako na wanataka yaliyo bora kwa ajili yako na kwa wewe kufanikiwa. Wanaweza wasiwe wakamilifu katika kukutia moyo katika maendeleo yako, nawe si mkamilifu katika kuyafikia. Kuwa na maongezi ya uaminifu na upendo na wazazi wako na Roho atakuongoza ili kupata muafaka.
Brooke T., 18, Arizona, Marekani
Kuwa Msikilizaji Mnyenyekevu
Hivi karibuni nimejaribu kuwa msikilizaji mzuri. Ninajaribu kusikiliza kwa utulivu kabisa kile wazazi wangu wanachokuwa wakisema badala ya kubishana au kuwakata kauli. Inahitaji uvumilivu mwingi na unyenyekevu, lakini kufanya hili kunaweza kuimarisha uhusiano wenu na wazazi na kuruhusu uelewa zaidi kwa kila upande.
Kami K., 18, Utah, Marekani