2023
Ahadi Yetu ya Kuwa Nuru
Januari 2023


“Ahadi Yetu ya Kuwa Nuru,” Kwa Ajili ya Nguvu Kwa Vijana, Jan. 2023.

Njoo, Unifuate

Mathayo 3

Ahadi Yetu ya Kuwa Nuru

Yesu Kristo ni Nuru ya Ulimwengu. Acha tufanye yote tunayoweza ili kushiriki nuru Yake.

Picha
ubatizo

Umati wa watu ulikuja kutoka kila mahali kumwona mtu nyikani aliyevaa mavazi yaliyotengenezwa kwa manyoya ya ngamia na kula nzige na asali. Walivutiwa kusikia mafundisho yake kuhusu Mwokozi, toba, na ubatizo. Baada ya kumsikiliza, watu wengi walitaka kubatizwa. Aliwabatiza wale waliotubu. Jina la mtu huyu lilikuwa Yohana Mbatizaji.

Siku moja, wakati Yohana akibatiza watu katika Mto Yordani, Yesu Kristo alimjia na kumwomba ambatize. Yohana alishangaa. Alijua kwamba Yesu daima alitii amri za Mungu na hakuhitaji kutubu. Ukweli ni kwamba, alifikiri kwamba Yesu anapaswa kumbatiza yeye (ona Mathayo 3:14)! Yesu alimweleza kwamba Mungu amewaamuru watu wote wabatizwe, hivyo Yeye pia alihitaji kubatizwa ili kuonyesha mfano. Yohana alikubali na akambatiza Yesu katika Mto Jordani.

Ubatizo wa Yesu unatufundisha kwamba sisi, pia, lazima tubatizwe. Ulipokuwa unabatizwa, ulifanya agano na kuonyesha utayari wako wa kufuata mfano wa Mwokozi, siyo tu kwenye ubatizo wako bali daima.

Ahadi na Fursa

Kwenye ubatizo, unafanya agano na Mungu na unaahidi kujichukulia juu yako jina la Yesu Kristo. (ona Mosia 5:8–10). Pia unaahidi kushika amri Zake, kusimama kama shahidi wa Mungu “nyakati zote na katika vitu vyote, na katika mahali popote” (Mosia 18:9), na kumtumikia Yeye (ona Mosia 18:8–10; Mafundisho na Maagano 20:37).

Kila wiki Kanisani, unafanya upya agano hili unapopokea sakramenti (ona Mafundisho na Maagano 20:77, 79). Kisha “Unasonga mbele ukiwa na imani imara katika Kristo, ukiwa na mg’aro mkamilifu wa tumaini, na upendo kwa Mungu na wanadamu wote” (2 Nefi 31:20).

Njiani, utakuwa na fursa nyingi za kufuata mfano wa Mwokozi na kuonyesha upendo wako Kwake na kwa wale wanaokuzunguka. Mzee Jeffrey R. Holland wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili amesema: “Tunao majirani wa kuwabariki, watoto wa kuwalinda, masikini wa kuwainua na ukweli wa kuulinda. Tunayo makosa ya kusahihisha, ukweli wa kushiriki na mema ya kufanya. Kwa ufupi, tunayo maisha ya kutoa ya ufuasi wa dhati.”1

Nuru kwa Wale walio katika Uhitaji

Mfano wetu mkamilifu, Mwokozi daima aliwapenda na kuwatumikia wengine na “akazunguka huko na huko akitenda mema” (Matendo ya Mitume 10:38).

Katika nyakati ngumu, Yesu Kristo ni Nuru “ing’aayo gizani” (Yohana 1:5). Yeye pia ametufundisha sisi kuwa nuru. Alisema, “Tazama mimi ni mwangaza ambao mtainua—kwamba mfanye yale ambayo mmeniona nikifanya” (3 Nefi 18:24).

Kama sehemu ya agano lako la ubatizo, wewe unaahidi kuwa uko “radhi kubeba mizigo ya mmoja na ya mwingine, ili iwe miepesi” na “kuomboleza na wale wanaoomboleza … na kuwafariji wale wanaohitaji kufarijiwa” (Mosia 18:8–9).

Unapokutana na mtu mwenye huzuni au aliyekata tamaa, yaweza kuwa wazi jinsi ya kumsaidia. Kuna nyakati zingine, hata hivyo, utakuwa hujui nini cha kusema au cha kufanya. Katika nyakati hizo, unaweza bado kufungua moyo wako. Unaweza kuwasikiliza na kuwasaidia.

Unapowapenda na kuwahudumia wengine, nuru ya Mwokozi inakuwa angavu zaidi ndani yako na itaangaza njia mbele yako. Pia itawavutia wengine wanaotafuta nuru ya Mwokozi. Kwa kusonga mbele na kushika ahadi ulizofanya kwenye ubatizo, utapata njia nyingi ambazo kwazo unaweza kuufanya ulimwengu kuwa bora na angavu zaidi.

Muhtasari

  1. Jeffrey R. Holland, Mkutano mkuu wa Okt. 2012 (Ensign au Liahona, Nov. 2012, 84–85).

Chapisha