2023
Muujiza Mkubwa
Januari 2023


“Muujiza Mkubwa,” Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana, Jan. 2023.

Njoo, Unifuate

Luka 1, 5

Muujiza Mkubwa

Kuna muujiza mmoja ambao ni muhimu kuliko yote.

Kwa Mungu, mambo yote yanawezekana (ona Luka 1:37; Wafilipi 4:13). Lakini je, unaweza kuomba kwa ajili ya jambo lolote na likaja kuwa kweli? Kwa nini baadhi ya watu wanapata miujiza wakati inaonekana kama wengine hawapati? Na haya yote yana maana gani hasa kwako wewe?

Miujiza mitatu ya kale, miujiza mitatu ya siku za leo na muujiza mmoja mkubwa inatufundisha mengi zaidi.

1

Muujiza wa Kale

Picha
Yusufu, Mariamu na mtoto Yesu

Vielelezo na Camila Gray

Mariamu huenda alishangazwa kupita kiasi wakati malaika Gabrieli alipomwambia kuwa angelikuwa mama wa Mwokozi. Haikupaswa kuwa kitu kilichowezekana. Lakini malaika Gabrieli alielezea kwamba Yesu angekuwa Mwana wa Mungu na akasema: “Hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu.” (Luka 1:37). Na malaika alikuwa sahihi. Mariamu alimzaa Mwokozi wa ulimwengu.

Muujiza wa Siku za Leo

Picha
akina dada wamisionari wakimsaidia bibi kizee

Wamisionari wawili wanaohudumu huko Mexico walikuwa wakivuka mtaa wenye magari mengi kila siku. Wakati mwingine wangesubiri dakika 10 kabla ya kupata nafasi ya kuvuka na kwa kawaida ilibidi wakimbie! Ndipo walipokutana na bibi kizee mmoja, aliyetembea polepole sana muumini asiyehudhuria kanisani kikamilifu. Alitaka kuja kanisani pamoja nao, lakini—hapa inakuja sehemu isiyowezekana—alitakiwa kuvuka ule mtaa wenye magari mengi. Na hapana, wamisionari hawangeweza kumbeba na kumvusha (japokuwa nao bila shaka waliliwaza hilo!). Lakini wakapata muujiza. “Tulipoufikia ule mtaa,” mmoja wa wale wamisionari anasema, “hapakuwa na magari yaliyokuja. Tuliweza kutembea polepole sana na kwa usalama tukavuka upande wa pili.”

Haiwezekani? Fikiria Tena!

Kwa Mungu, mambo yote yanawezekana (hata mambo yasiyowezekana!).

2

Muujiza wa Kale

Picha
Yesu Kristo anamponya mwanaume mgonjwa aliyeshushwa kupitia kwenye paa.

Palikuwa na mwanaume “aliyepatwa na ugonjwa wa kupooza,” au asiyejiweza. Aliamini kuwa Mwokozi angemponya. Lakini Yesu alikuwa amezungukwa na watu wengi na ilikuwa vigumu kumfikia. Basi mtu yule alifanya nini? Rafiki zake walimshusha akiwa juu ya kitanda chake kupitia paa la ile nyumba ili amfikie Mwokozi. Hapana, hilo huenda halikuwa jambo rahisi sana. Lakini yeye na rafiki zake lazima walikuwa na imani kubwa. Na ilizaa matunda—Yesu alisamehe dhambi za yule mtu na akamponya (ona Luka 5:17–26).

Muujiza wa Siku za Leo

Picha
kinyonga

Ella W. alikuwa akicheza na rafiki zake katika bustani wakati baadhi ya rafiki zake walipompoteza kinyonga wao wa kufugwa. Hii yawezekana isiwe kitu kikubwa sana. Lakini kumbuka, vinyonga hubadili rangi ili kujifananisha na mazingira yanayowazunguka. Baada ya kutafuta kwa muda, Ella aliamua kwamba ulikuwa wakati wa kuomba kwa imani. Punde waliweza kumpata kinyonga kwenye mti! “Alipokuwa tayari yuko mkononi mwa mtu, tulitoa maombi ya shukrani kwa Baba wa Mbinguni,” Ella anasema.

Miujiza Huja kupitia Imani katika Yesu Kristo

Yasiyowezeka daima yanawezekana kwa Mungu. Lakini tunahitaji kuwa na imani katika Mwokozi (au angalau hata hamu ya kuamini!) na kutenda juu ya imani hiyo kwa muujiza kutokea.

3

Muujiza wa Kale

Picha
Elisabeti, Zakaria na mtoto Yohana Mbatizaji

Elisabeti na Zakaria walikuwa wameoana miaka mingi lakini hawakuwa na watoto wowote. Wakati mwingine, ilionekana kana kwamba maombi yao ya imani hayakuwa yakijibiwa. Na mwishowe, walikuwa wamezeeka sana kuweza kuwa na watoto. Lakini ndipo malaika akamtokea Zakaria na kumwambia kwamba Elisabeti ataweza kupata mtoto. (Ukweli wa kufurahisha: mtoto hatimaye alikuja kuwa Yohana Mbatizaji!) Mwishowe, lisilowezekana lilikuja kuwezekana. Lakini Elisabeti na Zakaria walipaswa kusubiri kwa muda mrefu, mrefu sana (ona Luka 1).

Muujiza wa Siku za Leo

Picha
baraka ya ukuhani

Lindsey M. aliugua ugonjwa wa kifafa. “Kila asubuhi, nilimwomba Baba yangu wa Mbinguni aniondolee mbali kifafa hicho,” Lindsey anasema. Lakini hakikuondoka. Wakati Lindsey akisubiri kuponywa, alipokea baraka ya ukuhani, ambayo ilimletea amani. Na ile amani peke yake ilikuwa ni muujiza. “Tunapomgeukia Baba yetu wa Mbinguni, Yeye bila shaka atakuwa hapo kwa ajili yetu, akisambaza miujiza na kutoa faraja,” Lindsey anasema. Lindsey hatimaye alipokea upasuaji ambao ulimsaidia katika kifafa chake.

Miujiza Huja Kulingana na Mapenzi ya Mungu

Mungu anaweza kufanya mambo yote. Unaweza kuwa na imani kubwa. Lakini miujiza huja kulingana na wakati na mapenzi ya Baba wa Mbinguni na katika njia Yake. Tafuta miujiza mingine njiani, kama vile amani na nguvu ya kuvumilia.

Muujiza Mkubwa

Tumezungumza mengi kuhusu miujiza. Lakini kuna muujiza mmoja ambao ni mkubwa na muhimu zaidi kuliko mingine yote. Muujiza huo ni wakati Mwana wa Mungu alipokuja duniani kama mtoto, baadaye akafundisha na kuponya na kisha akajitolea maisha yake. Yesu Kristo alijichukulia juu Yake dhambi zetu, huzuni na madhaifu yetu. Muujiza Wake unajumuisha siku tatu ndani ya kaburi na kisha ufufuko ambao umeleta maisha baada ya kifo kwa ajili yetu sisi sote. Huo muujiza umebadilisha kila kitu.

Ni rahisi kujikuta tukijaribu kuwa na imani katika muujiza mmoja maalum. Na hiyo inaweza kuwa vigumu tunapokuwa hatujui mapenzi ya Mungu. Kwa hiyo badala ya kufokasi imani yako kwenye muujiza unaoutaka, fokasi juu ya muujiza wa Upatanisho wa Mwokozi. Kuwa na imani kwamba hakuna lisilowezekana kwa Mungu, ikijumuisha kile unachokiombea. Lakini pia uwe na imani kwamba mapenzi Yake ni bora zaidi kuliko ya kwako mwenyewe. Kama maombi yako hayajibiwi katika njia unayoitumainia, Yeye atakuimarisha na kukusaidia uvumilie.

Kikubwa cha Kuchukua

Unapofokasi imani yako juu ya Yesu Kristo, utaelewa kile inachomaanisha kwamba kwa Mungu mambo yote yanawezekana. Utaamini kwamba Baba wa Mbinguni anaweza kujibu maombi yako, nawe utatumainia mapenzi Yake na kupokea amani Yake pale mambo yanapokuwa hayaendi kama yalivyopangwa. Hivyo basi weka imani yako katika Yesu Kristo. Yeye ndiye muujiza. Na mambo yote yanawezekana Kwake Yeye.

Chapisha