“Vipawa vya Injili katika Guam,” Kwa Ajili ya Nguvu Kwa Vijana, Jan. 2023.
Vipawa vya Injili katika Guam
Katika kisiwa cha bahari, Franchesca anapata urafiki na faraja kupitia injili.
Kwa fukwe zake, maji matulivu na mapango ya kale, kisiwa cha Guam kinasikika kama ndoto ya mapumziko, lakini ni siku ya kawaida katika maisha ya msichana wa miaka 15 Franchesca N.! Yeye anapenda fukwe nzuri za bahari. “Ni burudani kutoka nje na kutalii mazingira ya asili.”
Akiwa amezaliwa na kulelewa Guam, anapenda kufanya vitu nje ya nyumbani. “Mimi ni mtu wa nje ya nyumbani zaidi, hakika sipendi kukaa ndani,” yeye anasema. Anapenda kupiga makasia baharini, kuogelea, na kupanda milima pamoja na wazazi na dada zake wawili. Wanapenda hususan kupanda mahali yalipo mapango ya kale.
“Hakika niko karibu sana na dada zangu. Wao ni rafiki zangu wakubwa,” anasema. Dada yake mkubwa anasoma huko Hawaii. “Mitandao ya kijamii ni nyenzo kubwa inayotusaidia kuwasiliana,” Francesca anaelezea. Yeye anapenda kuwa karibu na kuunganika.
Mfano kwa Wengine
Franchesca ni mwanafunzi wa mwaka wa pili katika shule ya wasichana pekee ya Kikatoliki, ambapo yeye ni muumini pekee wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Kuwa muumini pekee wa Kanisa katika shule yake ilikuwa inaogopesha mwanzoni, lakini sasa amezoea kuonekana tofauti. Kwa nyongeza, wengine wanaomzunguka wanafikiri ni vizuri kwamba yeye ni sehemu ya dini tofauti.
Kwa mfano, rafiki zake walikuwa wakinywa kahawa wakati wa chakula cha mchana, na Franchesca aliweza kuelezea Neno la Hekima kwao.
Franchesca pia amechagua kutoapa ingawa watu wengine shuleni hapo wanafanya hivyo. Yeye anasema, “Nilijaribiwa mara nyingi hapo mwanzoni, lakini kitu ambacho kinaniweka imara ni uhusiano wangu binafsi na Baba wa Mbinguni kupitia maombi.” Anaongeza “Sipaswi kufanya mambo haya, kwa sababu si sahihi na kwa sababu ninawapenda Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo.
Kupata Marafiki
Wakati mwingine inaweza kuwa upweke kuwa muumini pekee wa Kanisa katika shule yake. Alipokuwa mwaka wa kwanza, Francesca alijisikia mpweke sana wakati wa janga la ulimwenguni na hakuwa na marafiki wengi. Alikuwa na wasiwasi kuwaambia wazazi wake kuhusu hili, lakini alipoomba, alihisi msukumo wa kuwaambia jinsi alivyokuwa akijisikia.
Kama familia, waliamua kuomba kwa ajili yake ili aweze kupata marafiki wa kuaminika. Kimuujiza, mara tu walipomaliza maombi yao, walisikia mtu akigonga kwenye mlango wao. Ilikuwa ni mmoja wa rafiki zake kutoka kata tofauti na alikuwa ameleta biskuti! Francesca alijua kwamba Baba wa Mbinguni alikuwa amesikia maombi yake.
Kigingi cha Franchesca kinajumuisha waumini kutoka Guam na visiwa vingine kadhaa. Kata yake ina kikundi kidogo tu cha vijana, lakini kata yake ni kama familia. Waumini wake wana urafiki, na hii inamtia moyo kwenda kanisani kila Jumapili. Wao ni ushawishi na mfano mkubwa wa kuigwa katika maisha yake.
Franchesca pia amepata nguvu katika darasa lake la seminari. “Seminari ni mojawapo ya matukio muhimu katika wiki yangu,” anasema. “Ninapohudhuria seminari, ninahisi kama mashaka yangu yote yametoweka.”
Anapenda kuhudhuria seminari, iwe mtandaoni au ana kwa ana na hakosekani darasani isipokuwa imebidi. Anasema wiki zake zinakwenda vizuri zaidi kwa sababu amechagua kuhudhuria seminari. Kama amekuwa na wiki yenye shughuli nyingi, anahakikisha anaenda seminari kwa sababu huko anajisikia amani.
Vijana pia wanazo shughuli kama mara mbili au tatu kwa mwezi. Franchesca aliwahi kupanga mojawapo ya hizo—usiku wa michezo wenye burudani nyingi za michezo na michezo ya maandiko. Hawajaweza kukutana mara nyingi wakati wa janga la ulimwengu, hivyo wanapokuwa wamekutana, wanakuwa na muda mzuri wa kufurahi.
Wasichana walitengeneza video ya muziki ya wao wenyewe kwa kuoanisha midomo na wimbo wa Kanisa wa vijana wa “Good Day” na wakautuma mtandaoni ili kushiriki upendo na kuwainua wengine. “Mitandao ya kijamii inaweza kabisa kumleta kila mmoja pamoja, hususan nyakati ambapo kwa kweli hatuwezi kumwona kila mmoja.”
Kutazamia Kwenda Hekaluni
Katika mkutano mkuu wa Oktoba 2018, Hekalu la Yigo Guam lilitangazwa. Franchesca anasema, “Vijana walifurahia—sisi sote tuliomba kwa ajili ya hekalu.” Baada ya hilo, kwa hamu aliangalia ujenzi na kusubiria kwa ajili ya hekalu lao wenyewe, ambalo lilikamilika Mei 2022.
Wamekuwa daima wakisafiri kwenda Ufilipino kwa safari za hekaluni siku za nyuma. Ili kulipia safari hizo, walikuwa wakitafuta pesa kwa kuoka mikate na kuosha magari. Kwa sababu ni safari kubwa, wangeipanga ichukue karibia wiki moja. Franchesca anafurahia kuweza kwenda hekaluni mara nyingi zaidi na kupata baraka ambazo zinakuja kutokana na kubatizwa kwa ajili ya mababu.
Faraja kupitia Maombi
Franchesca anasema kwamba yeye ana tabia ya kuwa na hofu sana, lakini maombi yamemsaidia. “Maombi yana nguvu sana. Kuongea tu na Baba wa Mbinguni kunamfariji sana. Yeye anasikiliza na anaweza kusaidia.”
“Ninaposali, siyo kwamba daima jibu linakuja kwangu punde tu,” anasema. “Ni hisia tu ya mwongozo ambayo inanisaidia; ile hisia ya uwepo Wake na upendo Wake. Inanifariji na kunifanya nijisikie vizuri zaidi.”
Ushauri wake kwa vijana wengine ni: “Ombeni kwa Baba wa Mbinguni. Zungumzeni Naye. Hiyo inasaidia sana.”
Anasema mama yake pia ni mtu wa kuhofu sana lakini pia ni msaada mkubwa. “Mama yangu ni baraka kutoka kwa Baba wa Mbinguni, na ameniongoza sana.”
“Familia ni baraka kubwa,” anasema. “Nafikiri kufungua moyo wako kwa familia yako au rafiki kama unapitia kitu fulani ni muhimu.”
Franchesca anataka kila mtu azione baraka za Bwana za kila siku. “Baraka za kila siku zinaweza kuwa rahisi sana. Kwenda shule ni baraka kubwa sana. Kuna baraka nyingi nzuri kama tutatenga muda wa kuzitambua. Nashukuru sana kuwa na injili katika maisha yangu.”