“Nuru Yetu Nyikani,” Liahona, Jan. 2024.
Nuru Yetu Nyikani
Wale ambao kwa dhati husoma Kitabu cha Mormoni, kuishi mafundisho yake, na kusali ili kujua ukweli wake, watahisi Roho Mtakatifu na ongezeko la imani yao katika, na ushuhuda juu ya, Mwokozi.
Kama mvulana mdogo, nilikuwa na ushuhuda juu ya kitabu cha Mormoni. Nilihisi kuvutiwa hususani na hadithi ya kaka wa Yaredi na watu wake katika safari yao kwenda “nchi ya ahadi” (Etheri 2:9).
Wakati walipokabiliwa na uwezekano wa kusafiri ndani ya mashua pasipokuwa na mwanga, kaka wa Yaredi aliuliza, “Tazama, Ee Bwana, utakubali tuvuke maji haya mengi kwenye giza?” Akijibu, Bwana alisema, “Ungetaka nifanye nini ili muwe na mwangaza kwenye boti zenu? (Etheri 2:22, 23).
Kaka wa Yaredi alijua kwamba Bwana alikuwa mwenye uwezo wote. Alijua kwamba Bwana alikuwa chanzo cha mwangaza wote. Alijua kwamba Bwana ameamuru watu wake kumlingana Yeye wakati wa shida. Hivyo, akionyesha imani katika Bwana kaka wa Yaredi alitayarisha mawe madogo16. Utakumbuka kwamba kisha akamwomba Bwana ayaguse mawe yale kwa kidole Chake “ili yapate kutoa nuru gizani” (Etheri 3:4).
Picha ya Bwana akiyagusa mawe yale imebandikwa akilini mwangu tangu niliposoma hadithi ile kwa mara ya kwanza. Ninaweza kuona taswira ile kana kwamba ilikuwa ikitokea mbele ya macho yangu. Pengine hiyo ni kwa sababu taswira ya giza likifukuzwa na nuru ni halisi kwangu mimi.
Ninapokuwa simhisi Roho Mtakatifu, pale ninapokuwa kidogo nje ya tuni na Roho wa Bwana, ninahisi giza. Lakini ninaposoma Kitabu cha Mormoni, nuru hunirudia. Kitabu cha Mormoni kwangu mimi kimekuwa kama mawe yenye kutoa mwanga yaliyoguswa na Bwana. Kimeiangaza safari ya maisha yangu yote.
Nuru Milele
Kama wale walioletwa kwa mkono wa Bwana kwenye Amerika ya zamani, sote tunakabiliwa na dhoruba na giza katika safari yetu kwenye nchi ya ahadi ya kuinuliwa. Lakini Bwana atafanya kwa ajili yetu kile ambacho Yeye alikifanya kwa ajili ya Wayaredi na Wanefi. Yeye atatuongoza na kuangaza njia yetu—kama tutamtii Yeye, kutumia imani katika Yeye, na kuomba msaada Wake.
Bwana alimwambia Nefi, “Nitakuwa pia nuru yenu huko nyikani; na nitawatayarishia njia mbele yenu, kama mtatii amri zangu; kwa hivyo, vile mtakavyotii amri zangu mtaongozwa hadi kwenye nchi ya ahadi; na mtajua kwamba ni mimi ninayewaongoza” (1 Nefi 17:13).
Bwana alimwambia kaka mdogo wa Nefi Yakobo, “INitakuwa nuru kwao milele, wale wanaosikia maneno yangu” (2 Nefi 10:14).
Kuhusu Mwokozi, nabii Abinadi alishuhudia, “Yeye ni nuru na uzima wa ulimwengu; ndio, nuru isiyo na mwisho, ambayo kamwe haiwezi kutiwa giza” (Mosia 16:9).
Juu Yake Yeye Mwenyewe, Mwokozi alitoa ushuhuda , “Mimi ni nuru na uzima wa ulimwengu.” Aliongeza, “Tazama, mimi ndimi nuru; nimewapatia mfano” (3 Nefi 9:18; 18:16).
Kuihisi Nuru
Ninampenda nabii wetu, Rais Russell M. Nelson. Ninayo baraka ya kuhudumu pamoja naye. Anapoingia ndani ya chumba, chumba hicho mara huwa na mwangaza zaidi. Yeye anabeba Nuru ya Kristo pamoja naye.
Nuru ya Kristo ni kitu halisi. Ni “nguvu ya kiungu, uwezo au ushawishi ambao hutoka kwa Mungu kupitia Kristo na hutoa uhai na nuru kwa vitu vyote.” Ni zawadi ya thamani inayoweza kuwaongoza watoto wa Mungu kwa Roho Mtakatifu na injili ya Yesu Kristo.1 Kusoma Kitabu cha Mormoni kunaimarisha nuru hiyo.
Nyakati zingine tunahitaji kutazama nyuma ya maisha yetu ili kukumbuka ni kwa jinsi gani tumesaidiwa kwenye safari yetu. Tunapotazama nyuma, tunaweza kuhisi nguvu ya Mwokozi tena. Wakati maandiko yanaposema, “Kumbuka, kumbuka” (Helamani 5:12), ninafikiri yanatuambia, “siyo ukumbuke tu kile wakati mmoja ulichojua au ulichohisi, badala yake, uhisi nuru hiyo tena.”
Kwa baadhi ya watu, kuhisi nuru ya kiroho huja kwa urahisi. Kwa wengine nuru ya kiroho inaweza kuwa vigumu kuihisi kwa sababu ya mapambano binafsi au kelele za ulimwengu. Lakini kama tutakuwa waaminifu, nuru itakuja—wakati mwingine katika njia tusizotarajia.
Rais Nelson, ambaye ametushauri “kwa sala tujifunze Kitabu cha Mormoni kila siku,”2 ameshiriki njia kadhaa ambazo kwazo Kitabu cha Mormoni kinaweza kutuleta sisi karibu zaidi na Mwokozi na kutusaidia sisi kuhisi nuru ya injili, kupata kweli za injili na kuishi mafundisho ya injili.
Tunaposoma Kitabu cha Mormoni Rais Nelson alisema, uelewa wetu na shukrani zetu juu ya Upatanisho wa Yesu Kristo utaongezeka.
Tutahisi hamu ya “kuzaliwa tena” (Mosia 27:25) kama kitabu kinavyotusaidia kupata badilio la moyo (ona Mosia 5:2).
Tunapokisoma na kujifunza mafundisho ya Kitabu cha Mormoni kuhusu kukusanyika kwa Israeli, tutahisi ongezeko la hamu ya kuwatafuta wafu wetu na kufanya ibada za wokovu na kuinuliwa kwa niaba yao hekaluni.
Tutahisi nuru tunapopokea majibu ya maswali yetu, mwongozo katika kufanya maamuzi na nguvu ya kutubu na kupinga uovu.
Na tunaposoma kweli zinazopatikana katika Kitabu cha Mormoni, tutahisi uponyaji, faraja, urejesho, usaidizi, nguvu, kufarijika na kushangilia kwa nafsi zetu.3
“Ee lakini, hii siyo hali halisi?” Alma aliuliza kuhusiana na kuvimba huku, kuchipua kwa mbegu ya ukweli, ufahamu na ushuhuda. “Nawaambia, Ndio, kwa sababu ni nuru; na chochote ambacho ni nuru, ni kizuri, kwa sababu kinaonekana, kwa hivyo lazima mjue kwamba ni kizuri” (Alma 32:35).
Mtafute Mwokozi Gizani
Rafiki yangu Kamryn akiwa na umri wa miaka 10, alipata ugonjwa hadimu lakini ugonjwa wa kudumu wa macho ambao ulishambulia mboni ya jicho la kulia.4 Kuna wakati, maumivu husika yalikuwa yenye kuendelea na yasiyovumilika, Kamryn hakuweza kuvumilia nuru yoyote. Wazazi wake, waliogopa angeweza kuwa kipofu, wangeweka giza madirisha ya chumba chake cha kulala ili kujaribu kumfariji. Mama wa Kamryn, Janna, anakumbuka:
“Takribani miezi minne baada ya uchunguzi wa afya yake, niliingia ndani ya chumba chake kilichotiwa giza. Macho yangu yalipoizoea hali ya chumba, ningeweza kumwona Kamryn amejikunyata katika mkao wa kijusi tumboni kwenye kitanda chake. Alikuwa katika maumivu makali kiasi kwamba hakuweza kusogea au hata kulia aliposikia mimi ninaingia. Alilala hapo tu na macho yake yote mawili yamefumba na yamevimba.
“Nilipiga magoti pembeni ya kitanda chake, mkono wake nikiushika kwa mkono wangu, nikimbinya mara tatu—ni utambulisho wetu wa ‘Ninakupenda.’ Kwa kawaida yeye angeubinya wangu mara nne akimaanisha ‘nakupenda zaidi,’ lakini hakujibu. Alikuwa katika maumivu makali sana. Machozi yakinitiririka mashavuni, nilimtazama mtoto wangu wa umri wa miaka 10 aliyekuwa mahiri wa kudaka mpira kwa kulala. Moyo wangu ulivunjika.”
Janna alisema kimya kimya, sala ya moyo.
“Nilimwambia Baba wa Mbinguni kwamba nilijua kwamba Yeye anajua lililo bora zaidi, lakini niliomba, ‘Tafadhali msaidie.’ Nilipokaa hapo ninalia, wimbi la joto la uvuguvugu lilinifunika. Nilihisi utulivu wakati wazo kuhusu Mwokozi Yesu Kristo liliponijia akilini: ‘Yeye ni nuru. Mtafute Yeye gizani.”
Janna aliinua kichwa chake na akanong’ona katika sikio la Kamryn: “Unapaswa kumtafuta Mwokozi katika giza.”
Baadaye, Kamryn alipata usingizi akisikiliza nyimbo za dini na maandiko kwenye aplikesheni ya maktaba ya Kanisa.
Ugonjwa wa Kamryn unabaki kimya kwa wakati mwingi, lakini maumivu yanapopanda, Janna na mume wake, Darrin, wanamfariji na tena wanaweka mablanketi kwenye madirisha ya chumba chake cha kulala. Wakati wa nyakati za maumivu makali, Kamryn husema, “Mimi ninamtafuta Mwokozi katika giza.”5
Wakati maisha yanapoonekana kama “nyika yenye giza na kuhuzunisha” (1 Nefi 8:4), sisi pia yawezekana tukahitaji kumtafuta Mwokozi gizani. Ninashuhudia kwamba Kitabu cha Mormoni na ushahidi wake “kwamba Yesu ndiye Kristo, Mungu wa milele,”6 kitatupeleka sisi kwake Yeye. Ninajua kwamba wale ambao wanakisoma kwa dhati Kitabu cha Mormoni, wanaishi kanuni zake na kusali kuhusu ukweli wake watamhisi Roho Mtakatifu na kuongeza imani yao katika, na ushuhuda juu ya Mwokozi.
Na tuonyeshe shukrani kwa ajili ya hiki kitabu “kilicho sahihi zaidi”7 kwa kukisoma, kukithamini na kukitumia li kuimarisha imani zetu na imani za wengine katika Nuru ya Ulimwengu.