“Kupata Ukamilifu kupitia Yesu Kristo,” Liahona, Jan. 2024.
Kuzeeka kwa Uaminifu
Kupata Ukamilifu kupitia Yesu Kristo
Kwa uhuru mpya nilioupata, fursa na matukio ambayo huja kutokana na kuwa kiota kitupu, kwa nini sikuhisi kukamilika? Ni nini kilikosekana?
Machozi yalidondoka nilipokuwa nikiomba kwa ajili ya amani wakati mwanangu mdogo akijaza maombi yake ya umisionari. Hakika nilitaka aende kuhudumu kama mmisionari. Nilitamani sana. Niliendelea kujaribu kujishawishi mwenyewe juu ya hili.
Ninampenda Mwokozi wangu na kiuhalisia nilisisimkwa na fursa hii ya mwanangu kushiriki shangwe tunayoweza kuipata kupitia Yesu Kristo. Walakini katika kina cha moyo wangu niliogopa mwanangu kuondoka. Nilijua kuwa Yeye hakika kamwe hangerudi nyumbani tena baada ya misheni yake. Hata kama angeishi nyumbani, mambo yasingekuwa sawa.
Marafiki zangu waliniambia hatua ya mtoto kuondoka nyumbani ilikuwa nzuri. Mume wangu na mimi tulihamasika na kutazamia uhuru huo na fursa ambazo hatujakuwa nazo kwa muda sasa wakati tukilea watoto wetu.
Kwa uhuru huu mpya tulioupata, nilijitupa mwenyewe katika shughuli nyingi. Nilisaffiri pamoja na mume wangu, nilijifunza kupiga kinanda kwa ajili ya wito wangu, nilicheza pamoja na wajukuu zangu, na nilifanya kazi ya hekalu na historia ya familia.
Nilipata hamasa na nilifanya safari zisizo za kawaida. Nilijiendeleza binafsi. Nilipata mambo mengi mazuri.
Bado daima kulikuwa na kitu kinakosekana. Kitu fulani bado hakikuwepo hapo. Mwanangu alipoondoka, alichukua sehemu kubwa ya moyo wangu ambayo ilionekana siwezi kuijaza.
Takribani mwaka mzima baada ya mtoto wangu kuondoka, nilipata tatizo la hasira ya kushindana na hasira ambayo watoto wangu walinirushia wakati walipokuwa wadogo. Mume wangu alinitazama na kusema, “Michelle, unahitaji kuhudumu.” Nilijisajili kwa ajili ya fursa ya kuhudumu.
Bado moyo wangu uliniuma. Nilipata wakati mgumu kujitupa mwenyewe katika kuhudumu au fursa nyingine yoyote iliyojitokeza. Pamoja na watoto wangu wote kuondoka, nilihisi kama maisha yangu kamwe yasingekuwa makamilifu tena.
Usiku mmoja wakati nikisali kuomba msaada, Roho aliniarifu kwamba nilikuwa nikipitia kipindi cha utupu ambacho huja kutokana na upotevu—kukosa lengo. Nilidhani nimeshughulikia hasa huzuni hiyo kwa kujaza maisha yangu kwa shughuli hizo zote nzuri.
Kutafuta Majibu
Nilipokuwa nikitafuta majibu, nilipata taarifa hii kutoka katika historia ya Nabii Joseph Smith: “Wakati tunapopoteza [kitu au mtu] fulani ambaye tumemweka moyoni inapaswa kuwa tahadhari kwetu. … Mapenzi yetu yanapaswa kuwa kwa Mungu na kazi yake kwa nguvu zaidi kuliko juu ya viumbe wenzetu.”1
Mwangaza huu ulipenya juu ya wingu jeusi juu ya moyo wangu. Nilikuwa nimejaribu kujaza nafasi yangu ya huzuni kwa mambo, shughuli na uzoefu—kuhudumu, kupenda, kufuatilia vipaji. Mambo yote mema, lakini hayakujaza shimo langu lililo wazi. Hawakuponya katika njia ambayo nilihitaji uponyaji.
Nilitambua kwamba aina ile ya amani na ukamilifu inaweza tu kuja kupitia Mwokozi,Yesu Kristo. Yesu alifundisha, “Mimi ndimi njia, na kweli na uzima” (Yohana 14:6). Ni kupitia Yeye tu tunapata shangwe na ukamilifu na amani na kuridhika. Zaburi 16:11 inasema, “Wewe utanionyesha njia ya uzima: mbele za uso wako ziko furaha tele.”
Jinsi Nilivyobadilika
Maisha hayakubadilika mara moja. Moyo wangu haukupona mara moja. Lakini nilijua mahali ambapo fokasi yangu ilipaswa kuwa ili hili litokee.
Sala zangu zilihama. Nilianza kumwomba Baba wa Mbinguni anisaidie kujenga uhusiano imara na Mwokozi. Wakati nilipokata tamaa, ningejikumbusha mwenyewe kwamba Yesu Kristo alikuwa hapo kwa ajili yangu, na kupitia neema Yake ya uwezo wa kulipia dhambi, Yeye angenisaidia. Kujifunza kwangu maandiko kulifokasi zaidi katika kujenga uhusiano na Yeye. Ilichukua muda, lakini niliendelea katika kuelekeza hisia zangu, nguvu zangu na mawazo yangu kwa Yesu Kristo.
Nilipokuwa nikitenda, kile kiza kinene kilianza kuinuliwa. Nilipata shangwe kuu katika matendo madogo madogo ya huduma na upendo kila siku. Nuru na Matumaini viliangaza njia yangu na kujaza utupu ndani ya moyo wangu. Kumweka Mwokozi kwanza kulinipa maana ya kina na furaha kwa kila nyanja ya maisha, kutoka kuhudumu hadi kutumia muda na familia, kutoka kusafiri hadi kukuza vipaji vyangu. Kila kitu kilizidi kuwa kingi zaidi na Kristo akiwa katikati.
Safari ya kila mmoja kupitia nyakati za mabadiliko katika maisha ni ya kipekee. Hata hivyo, ufumbuzi wa huzuni zetu ni kujibu wito wa Kristo anaposema, “Njooni kwangu kwa nia kamili ya moyo wako, nami nitakuponya [wewe]” (3 Nefi 18:32). Ni kupitia Kwake pekee tutapata uponyaji wa kweli, amani, upendo na shangwe.
Mwandishi anaishi Utah, Marekani.