Kozi za Elimu ya Kujitegemea: Kuunganisha Fedha na Kweli za Injili,” Liahona, Jan. 2024.
Kozi za Elimu ya Kujitegemea: Kuunganisha Fedha na Kweli za Injili
Kozi za elimu ya kujitegemea huwasaidia washiriki kuleta tambuzi za kiroho kwenye mahitaji yao ya kifedha.
Baadhi ya mafundisho ya awali ya Bwana kwa watoto wake ilikuwa ni kuhusu kazi na kujitegemea. Katika Agano la Kale, Yeye aliwaelekeza Adamu na Hawa “Kwa jasho la uso wako utakula chakula” (Mwanzo 3:19). Na kwa Waisraeli, alisema, Siku sita fanya kazi” (Kutoka 20:9).
Leo, makundi yote ya kujitegemea yanayodhaminiwa na Kanisa ulimwenguni kote yanawasaidia watoto wa Mungu kuboresha elimu yao, kuwa wenye kujiamini zaidi, kupata kazi nzuri, kuanzisha biashara na—kama uzoefu ufuatao unavyoonyesha—kusimamia vyema zaidi fedha zao.
Kulipa Zaka kwenye Mapato Finyu
Wakati wa ndoa yake, Deborah kutoka Michgan, Marekani, kamwe hakuwa na matatizo ya kutunza fedha zake. Lakini baada ya yeye na mume wake kuachana, ankara zikawa ngumu kulipika. Ingawa Debora amekuwa akifurahia kuingia hekaluni mara kwa mara, alianza kupata taabu ya kulipa zaka na kuacha kuendelea kwenda hekaluni.
Alitafuta msaada kutoka kwa askofu wake, ambaye alimweleza juu ya mpango wa Kanisa wa madarasa ya kujitegemea juu ya kutunza fedha binafsi, ambao ulikuwa ukifanyika katika kituo cha kigingi chake. Deborah akakubali kwenda, lakini mwanzoni hakuona sababu ya kwenda: “Kusema ukweli, nilijiambia mwenyewe, ‘sijui kwa nini niko hapa. Ninajua jinsi ya kufanya bajeti ya fedha zangu. Nimekuwa na bajeti katika maisha yangu.’”
Deborah alikutana na lile kundi na mwezeshaji. Kwa saa mbili kila wiki, walijifunza kuhusu vyote viwili kipengele cha kimwili cha ustahimilivu wa kifedha (kama kupanga bajeti) na kipengele cha kiroho cha ustahimilivu wa kifedha (kama vile kuwa msimamizi mwaminifu wa kipato). “Kamwe sikuwahi kuunganisha viwili hivi kwa pamoja kwa namna darasa lilivyounganisha,” Deborah anakiri.
Deborah alihisi kwamba maungano yake ya kiagano na Baba wa Mbinguni yalimsaidia kujifunza jinsi gani ya kumjumuisha Yeye katika maamuzi yake ya kifedha. ‘“Baba yangu wa Mbinguni daima amekuwa hapo kwa ajili yangu. … “Ninapaswa kumjumuisha Yeye katika kila kitu.”
Deborah alipofanyia kazi misukumo na maelekezo aliyopokea kutoka kwa kundi lake la kujitegemea, aliweza kuweka kando fedha kwa ajili ya zaka, kulipa ankara zake na hata kujiwekea fedha za akiba, yote haya pasipo kuongeza kipato.
Rais Heber J. Grant (1856–1945) alitoa ushuhuda kwamba mengi zaidi yanaweza kufanyika kwa sehemu inayobaki ya kipato baada ya kulipa zaka kuliko yanavyoweza kufanyika kwa kiasi chote cha mapato hayo kabla ya kulipa zaka: “Ninatoa ushahidi … kwamba wanaume na wanawake ambao wamekuwa waaminifu kikamilifu kwa Mungu, ambao wamelipa zaka zao … wanashuhudia … kwamba Mungu amewapa hekima ambapo wameweza kutumia kiasi kinachobaki cha tisa ya makumi, na imekuwa na thamani kubwa zaidi kwao, na wameweza kukamilisha mengi zaidi kwa kiasi hicho kuliko ambavyo wangeweza kama wasingekuwa waaminifu kwa Bwana wao.”1
Deborah alipokea baraka “vyote kimwili na kiroho” (Mosia 2:41) kadiri alivyoendelea kushika sheria ya zaka na kutumia kanuni za injili katika bajeti yake. Maelekezo kutoka kwa kundi lake la kujitegemea na mwongozo wa kiungu kutoka kwa Roho Mtakatifu vilitoa njia ya yeye kupata kibali na kurudi hekaluni. “Kila kitu ambacho nilisema kwamba sikuweza kukifanya, Yeye alinionyesha kwamba ninaweza kukifanya na zaidi,” anashuhudia. “Kitu unachokifanya leo kinaamua kesho yako, na ninataka kesho yangu kuwa kwamba ninaweza kutembea ndani ya lile Hekalu la Detroit na kuanza kufanya kazi kwa ajili ya mababu zangu tena.”
Kuondokana na Deni
Berry Chu wa Kigingi cha Middle Taipei huko Taiwan alihitaji hekima kupita uelewa wake baada ya kufanya uwekezaji ambao haukufanya vizuri, ukamwachia deni kubwa. Hali hii kwa kiasi fulani ilmwacha Berry akiwa amepooza asijue la kufanya. Lakini Berry alijinyenyekeza mwenyewe na kumtafuta Baba wa Mbinguni katika sala. Kutoka katika sala ile, akapata ujasiri kumwambia mume wake kile kilichotokea. Kwa upole na unyenyekevu, mumewe Berry, Light Tsai, alimhakikishia kwamba wataliangalia kwa pamoja na kulishinda deni hilo. Kwa pamoja, Light na Berry walisali kuomba mwongozo wa Bwana.
Berry na Light walihisi wangefaidika kutokana na kozi za Kanisa za kujitegemea kwa masuala yao binafsi ya kifedha. Licha ya kuzidiwa na deni kubwa, walianzisha mpango wa kulipa. Kwa msaada wa kozi ile, walijifunza “kuweka kipaumbele cha kwanza kuwa zaka … Ili kutunza fedha katika njia nzuri,” Berry anasema. “Pia tulijifunza kuweka bajeti na kuweka kipaumbele matumizi yetu ya lazima tu.”
Siyo tu Berry na Light walijifunza kuweka bajeti ya mapato yao kwa kuwajibika, bali kikundi chao cha fedha binafsi pia kilimshawishi Berry kubadilisha kazi. Mpito huu uliongoza kwenye mshahara wa juu zaidi, ambao angeweza kutumia katika kulipa deni lake.
Wakiwa wameungana katika lengo lao, Berry na Light walitumia marupurupu yao yote, uwekezaji na mapato ya ziada kutokana na kazi zao za muda wote na kazi za muda mfupi kulipia deni la Berry. Pamoja na msaada wa Bwana, walilipia matumizi yao yote na la muhimu zaidi, bado walilipa zaka na kutoa matoleo mengine.
Bwana ametangaza: “Na ni madhumuni yangu kuwa niwapatie mahitaji watakatifu wangu. … Lakini lazima ifanyike katika njia yangu mimi mwenyewe” (Mafundisho na Maagano 104:15–16). Watu binafsi na familia ulimwenguni kote wanagundua jinsi gani anatoa mahitaji yao wanapoweka katika matumizi kanuni za kiroho na kifedha katika kujitegemea.
Kufundisha “Jinsi Gani” Siyo tu “Ni Nini” peke yake
Curtis na Pshaunda Scott, kutoka Texas, Marekani, wote wawili walitaka kuwa wenye busara katika fedha zao, lakini hawakuweza kukubaliana ni kwa jinsi gani. Pshaunda alijua walihitaji bima ya afya, lakini Curtis alijua hawangeweza kuigharamia. Ingawa walipendana wao kwa wao, mtazamo wao tofauti wa kifedha uliweka mpasuko katika ndoa yao. “Ilipofikia kwenye mambo ya kifedha,” Pshaunda anakumbuka, “sidhani kama tulikuwa katika kitabu kimoja, siyo tu kuwa ukurasa mmoja.”
Curtis anakubali. “Pesa daima ilikuwa somo lenye kutuchanganya, na kulikuwa na maongezi muhimu ambayo hatukuwa nayo.”
Askofu wao alipendekeza kwamba Pshaunda na Curtis waanze kuhudhuria kozi ya masuala ya fedha binafsi zinazotolewa na kigingi chao.
Curtis alishangazwa jinsi gani vyema mpangilio wa majadiliano bayana ya darasa lao yalivyofanya kazi kwa upande wake. Yeye aliweza kuelezea mawazo yake na kupata utambuzi kutoka kwa wengine walioelewa hali ya familia yake. Majadiliano ya kikundi yalimsaidia Curtis kugundua siyo tu kanuni za injili lakini pia njia halisi za kuyatumia. Katika miaka sita tangu ubatizo wake, Curtis mara nyingi amekuwa akifundishwa kwamba anapaswa kuongeza imani yake, kuboresha sala zake na kusogea karibu zaidi na Mwokozi, lakini alihisi kwamba kozi za kujitegemea ilimfundisha yeye jinsi gani ya kufanya maboresho hayo.
Curtis alipojifunza kutumia kanuni hizo za injili katika masuala ya kifedha ya nyumbani kwake na katika biashara zake, ndivyo alivyogundua kwa kina zaidi upendo wa Bwana kwake. “Kwa hakika iliimarisha kuamini kwangu na uelewa wangu juu ya matunzo na kujali ambako Baba wa Mbinguni hufanya kwetu,” anasema.
Pshaunda alihisi kwamba kipengele cha kiroho cha kozi ya kujitegemea kilimsaidia yeye kuelewa jinsi gani hata masuala ya fedha yanavyoweza kuingia katika mpango wa Mungu. “Yameimarisha ushuhuda wangu … hatua kwa hatua, mstari juu ya mstari.”
Kujumuisha mafundisho ya Bwana katika maamuzi yao ya kifedha mwishowe yalimleta Curtis na Psaunda pamoja kwenye ukurasa mmoja. “Tulikuwa tunakuwa timu moja,” Pshaunda anasema. “Nisingesema tulikuwa matajiri au kwamba tunazo pesa zaidi, lakini kwa hakika tunaelekea kwenye mwelekeo sahihi.”