“Kushinda Ukosekanaji wa Kusudi la Kiroho—Nifanye Nini Sasa?,” Liahona, Jan. 2024.
Vijana Wakubwa
Kushinda Ukosekanajiwa Kusudi la Kiroho—Nifanye Nini Sasa?
Tunaposonga kuelekea kwa Yesu Kristo, kamwe hatuko bila kusudi.
Kuingia katika ujana mkubwa kulileta msisimko mkubwa kwangu. Nilikuwa nimejiandaa kuanza kujenga maisha ambayo daima niliyataka. Nilihudumu misheni huko Brazil na kisha nilihudhuria chuo kikuu nilipofika nyumbani. Nilimaliza shahada yangu ya kwanza, nilipata kazi nzuri na nilijitahidi kuishi kama mfuasi wa Kristo.
Na bado niko katika hatua hii ya maisha. Ninafanya katika uwezo wangu zaidi katika kumfuata Yeye.
Ninashukuru sana kwa fursa na baraka nilizopata hadi sasa. Lakini nikiangalia nyuma na kuona kwamba nimefanya maagano yote ninayoweza hadi hatua hii (ukiachilia mbali ndoa) na kufikia mafanikio haya makubwa ambayo daima nilikuwa nikiyapanga, wakati mwingine najihisi nimekwama kidogo—nikiwa sina uhakika jinsi gani nitaendelea, hususani kiroho.
Nimewaona vijana wakubwa wanaonizunguka wakipambana pia. Baadhi hata wameacha Kanisa kwa sababu wanahisi ukosekanaji wa kusudi au matarajio yasiyofikiwa. Matendo yao mara nyingi yameongeza orodha ya maswali kwa ajili ya maisha.
Hata hivyo, sasa hivi, maswali yangu makubwa kwa Baba wa Mbinguni ni haya: Ni kwa jinsi gani ninaweza kushinda hisia ya ukosekanaji wa kusudi la kiroho? Je, napaswa kufanya nini sasa?
Huku nikiwa najiuliza maswali haya, nimejifunza kweli chache muhimu ambazo zimenisaidia kuongoza chombo wakati huu wa kukosa uhakika.
Usiruhusu Bughudha Zikutoe katika Njia
Wakati huu wa kutojua wapi pa kugeukia au nini cha kutegemea, nimetambua jinsi gani bughudha za ulimwengu zinavyoweza kwa urahisi kuanza kujichukulia kipaumbele juu ya mambo ya kiroho. Dada Rebecca L. Craven, Mshauri wa Pili katika Urais Mkuu wa Wasichana, alisema, “Ulimwengu umejawa na bughudha ambazo zinaweza kuwadanganya hata wateule, kuwasababishia wao kuwa wa kawaida katika kuishi maagano yao.”1
Nimewaona hata vijana wengine wakubwa wakipambana na shuhuda zao baada ya kurudi kutoka katika misheni zao. Pia nimewaona jinsi gani baadhi yao wamefikia hatua kubwa kama kuhitimu chuo kikuu au kuoa/kuolewa na hatimaye kuachana na mambo ya muhimu zaidi pale wanapokuwa hawatoi nafasi kwa ajili ya injili ya Yesu Kristo katika njia yao mpya ya kila siku.
Mimi pia nimepita katika mabonde na milima ya kiroho. Imekuwa ni vigumu nyakati zingine kuwa na hamasa na kutokuwa mvivu inapokuja kwenye tabia za kiroho, hususani wakati baraka kadhaa haziji haraka inavyotarajiiwa. Daima nataka kuendelea na kuwa bora—mimi sitaki kudumaa kiroho. Lakini wakati mwingine hujihisi kama ninakwenda tu na mtiririko pasipo lengo.
Hata hivyo, ninatenga muda kwa ajili ya Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo kila siku, hususani katika njia zilizo ndogo na rahisi (ona Alma 37:6), ninahisi faraja na utulivu ambavyo injili Yake inaniletea, hata wakati ulimwengu unapokuwa haujatulia.
Rais Russell M. Nelson alisema: “Ninawasihi kumwacha Mungu ashinde katika maisha yenu. Mpe sehemu nzuri ya wakati wako. Unapofanya hivyo, tambua kile kinachotokea kwenye msukumo wako chanya wa kiroho.”2 Kwa hiari ninapochagua kuwa na imani katika Yesu Kristo kila siku na kutenga muda kwa ajili ya tabia zile za kiroho ambazo huniunganisha mimi na Yeye, ninakumbuka nyakati nzuri za kiroho na kuhisi hali mpya ya kusudi, tumaini kwa siku za baadaye, na imani.
Tafuta Ushawishi Mzuri
Wakati mwingine nilipokuwa nahisi kukosa kusudi ilikuwa mwaka wangu wa mwisho wa chuo kikuu. Maisha yalikuwa magumu Ilikuwa wakati wa janga la ulimwenguni kote, hivyo nilipata msongo wa mawazo, wakati nikuwa nimekwama nyumbani. Kulikuwa siku za kukosekana kwa mwelekeo na muunganiko katika maisha yangu.
Hata nilitatizika na Kanisa wakati huu. Mara nyingi nilijibiringisha kitandani ndani ya nguo zangu za kulalia ili kusikiliza mkutano wa sakramenti kwenye mtandao kwa sababu hiyo ndiyo jitihada pekee niliyoweza kuifanya.
Katika kipindi hiki cha giza , niliitafuta familia yangu na marafiki na kuwaelezea jinsi gani nilivyokosa kusudi na msongo wa mawazo niliohisi. Sikuhisi kama nilibakiwa na tumaini lolote kwa siku za baadaye na sikujua jinsi gani mambo yatakavyokwenda. Na hapo ndipo waliponiambia kwamba walikuwa wananiombea na kunisaidia ingawa walikuwa mbali na mimi.
Nilipokuwa nawatafuta wapendwa wangu ambao walikuwa na imani kubwa na kadiri nilivyoomba kwa Baba wa Mbinguni kwa kiasi kidogo tu cha hamasa ya kiroho, nilihisi msaada wenye nguvu na upendo.
Nimegundua kwamba ninapokuwa ninafokasi sana kwenye matarajio yangu yasiyotimilika, mashaka yangu, au mapambano yangu, imani yangu inavurugika. Ninapoteza njia ya baraka katika maisha yangu. Lakini kwa dhati ninapojihusisha na mema kwa kusoma baraka yangu ya patriaki, kusikiliza jumbe za mkutano mkuu na kutumia muda wangu na wapendwa wangu ambao hunishawishi katika mema, ninafokasi upya katika tofauti za kimiujiza za injili ya Yesu Kristo zinazofanyika katika maisha yangu.
Hata kama huna njia iliyo wazi mbele yako wakati mwingine, au mambo hayaendi kama ulivyopanga, bado kuna mengi sana katika maisha yako na fursa nyingi ili kukusaidia kusonga kwenye njia ya agano. Daima kuna mambo ya kujifunza na nafasi zaidi ya kukua, hususani kiroho. Sali kwa Baba wa Mbinguni kwa ajili ya mwelekeo. Atakusaidia kutafuta na kupata ushawishi mwema na fursa ambazo zimekuzunguka kwa ajili ya ukuaji na kujifunza (ona Makala ya Imani 1:13).
Endelea Kujitahidi
Hali yetu binafsi ya kiroho inaweza wakati mwingine kwenda katika mawimbi—juu na chini. Wakati mwingine tunaweza kuhisi kuwa imara katika imani yetu na shangwe ya injili. Lakini wakati mwingine tunaweza kupambana ili kujua wapi kwa kugeukia baadaye. Tunaweza kupambana pale changamoto zinapokuja, maswali yanapoibuka, au baraka zinapochelewa, hususani tunapokuwa tunafanya tuwezacho katika kuishi injili. Katika nyakati hizi ngumu, mara nyingi nawaona watu wakichukua moja ya njia hizi mbili: moja ni ile wanayomfikia Mwokozi, na moja ni ile wasiyomfikia.
Wakati mwingine ninalinganisha nyakati hizi na hadithi ya Musa na nyoka wa shaba (ona Hesabu 21:8–9). Waisraeli walipokata tamaa ya kupona baada ya kuumwa na wale nyoka wenye sumu kali, Musa aliwapa njia rahisi ya kuokoka: kwa urahisi tu angalia nyoka wa shaba ambaye alimwakilisha Yehova. Hilo ndilo pekee walilopaswa kufanya. Jicho mara moja tu na wangeishi. Lakini wengi walichagua kutoangalia na wakaangamia. (Ona 1 Nefi 17:41).
Hadithi hii ilinifanya mimi nifikiri kuhusu jinsi gani sisi tunabeba uzito mchungu wa kukata tamaa na chuki kutokanna na kutotimizwa kwa matarajio yetu kwa wakati, wakati tiba iko tu mbele yetu!
Chanzo kikuu cha kuhisi tumaini, amani na imani kwa ajili ya siku zetu za baadaye ni kwa kumwangalia Yesu Kristo (ona Helamani 8:14–15; Yohana 3:14–17).
Nimekuwa daima mkosoaji mkali wa nafsi yangu ninapofanya makosa. Lakini kwa sababu kwa kweli nimekuwa nikijitahidi kujifunza kuhusu na kuamini katika Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo, najua daima naweza kuwatumainia kwa ajili ya msamaha, ukuaji na uponyaji katika nyakati ngumu Ninajua hilo ninapokuwa ninawaangalia Wao kupitia sala, kujifunza Njoo, Unifuate, kutumia muda hekaluni na kukuza wito wangu, napata hisia za shukrani na kufanywa upya.
Ninapowatafuta Wao, ninaona injili ya Yesu Kristo kwa kile inachomaanisha: kimbilio linalotupatia sisi faraja, usalama na uponyaji kutokana na nyoka wa ulimwengu.
Mzee Jeffrey R. Holland wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili kwa upendo alishuhudia: “‘Uangavu mkamilifu wa tumaini,’ uliotokana na upendo wa Mungu na watu wote—hilo ndilo tunalolitaka kwenu ninyi. … Kinachoambatana na tumaini hilo angavu ni mnong’ono usiokataliwa kwamba Mungu anakupenda, kwamba Kristo ni Mwombezi wenu, kwamba injili ni ya kweli. Uangavu wake utakukumbusha kwamba katika injili kuna daima—kila siku, kila saa—nafasi mpya, maisha mapya, mwaka mpya. Ni muujiza ulioje! Ni zawadi ilioje! Na kwa sababu ya zawadi ya Kristo, vitu muhimu zaidi katika maisha ni vyetu kama kwa uthabiti tutaendelea kuamini na kuendelea kujaribu na kuendelea kutumaini.”3
Sogea upande wa Yesu Kristo
Ujana mkubwa unaleta changamoto nyingi sana, mengi yasiyo na uhakika, na ndiyo, hata matarajio yasiyofikiwa kwa wakati. Lakini injili ya Yesu Kristo daima ina uhakika na daima ni thabiti. Na ahadi Zake na za Baba wa Mbinguni ni za uhakika kadiri daima tunavyoendelea kubaki katika njia ya agano. Ulimwengu unaweza kufanya iwe ngumu sana nyakati zingine kuendelea kufokasi katika Yeye. Lakini tukipiga hatua yoyote mbele ambayo inatufanya tusonge Kwake ni maendeleo. Tunapoelekea upande wa Kristo, kamwe hatuko bila kusudi—tunaelekea upande wa tumaini, amani na shangwe.
Mwandishi anaishi Manchester, Uingereza.