“Tafuta kwa Bidii Nawe Utapata,” Liahona, Jan. 2024.
Tafuta kwa Bidii Nawe Utapata
Bwana amefunua jinsi gani tunaweza kutafuta ukweli na mwelekeo katika maisha yetu.
Wakati mke wangu, Regina, na mimi tuliporudi nyumbani Brazil baada ya kuhudumu katika misheni ya Angola Luanda kutoka mwaka 2016 hadi 2019, tulikuwa na uamuzi muhimu wa kufanya. Tulikuwa tumeuza nyumba yetu kabla ya kwenda misheni. Mwaka mmoja baada ya kurudi nyumbani, tulipaswa kuamua kati ya kununua au kupanga nyumba. Je, tungewezaje kuchagua kilicho sahihi kwetu?
Maamuzi ya namna hii ni miongoni mwa kazi, shughuli na mashaka mengi ya kila siku ambayo huja kwetu sote. Nyakati zingine, vinaweza kutupoteza kutokana na baraka tukufu na nafasi ambazo ni injili ya Yesu Kristo ya urejesho pekee hutupatia. Katika uso wa dhamira nyingi na wajibu, inaweza kuwa changamoto kujua kile kilicho cha kweli au mwelekeo tunaopaswa kuchukua. Hii yawezekana ikatusababishia kwa ghafla tukahisi kuzidiwa na mahitaji makubwa.
Kwa shukrani mpendwa Baba yetu wa Mbinguni hajatuacha peke yetu tujitafutie wenyewe kilicho cha kweli au kile tunachopaswa kufanya.
Chanzo cha Ukweli Wote
Kabla ya kuondoka dunia hii, Mwokozi wetu, Yesu Kristo, aliwaahidi wafuasi Wake kwamba Baba angempeleka Mfariji, au Roho Mtakatifu, ili kuwabariki wao. Mfariji, Yesu alisema, “atawafundisha mambo yote, na kuwakumbusha mambo yote” (Yohana 14:26).
Kazi kuu ya Roho Mtakatifu ni kuwa mfunuzi wa ukweli (ona Yohana 16:13). Baba yetu wa Mbinguni ndiye chanzo ya ukweli wote uliofunuliwa, iwe unakuja kupitia manabii, waonaji na wafunuzi au kwetu binafsi kupitia Roho Mtakatifu. Kadiri tunavyojitahidi kuwa na mwenza wa Roho Mtakatifu, Baba yetu wa Mbinguni atatuongoza kuvuka nyakati za changamoto
Omba, Tafuta na Bisha
Kwa sababu Baba wa Mbinguni anataka kututia moyo, kutufundisha, kutuelekeza na kutujenga, tunaalikwa, “kuomba, nasi tutapewa; tafuteni, nayi mtapata, bisha, nanyi mtafunguliwa” (Mathayo 7:7; ona pia Luka 11:9; 3 Nefi 14:7).
Nefi aliposikia maneno ya baba yake, Lehi, kuhusu ono la Lehi la mti wa uzima, Nefi alisema “nilitamani pia kwamba nipate kumwona, na kusikia, na kujua juu ya mambo haya, kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, ambaye ni zawadi ya Mungu kwa watu wote ambao wanamtafuta Yeye” (1 Nefi 10:17).
Kutafuta ukweli kunahitaji bidii. Tunapokuwa na bidii, tunajitahidi bila kukoma, kwa dhati, na kwa nguvu kuujua ukweli na mapenzi ya Mungu kwa ajili ya maisha yetu. Bidii katika kutafuta ukweli kutoka kwa Bwana kunatusogeza karibu zaidi na Yeye katika hatua zote za maisha yetu.
Nabii Joseph Smith alijifunza mapema katika maisha yake kwamba moja ya njia zenye tija zaidi ya kutafuta ukweli ni kwa uaminifu kutafuta majibu ya maswali (ona Joseph Smith—Historia ya 1:10, 18). Tunaweza tukauliza maswali haya yafuatayo katika kutafuta ukweli. Majibu huwakilisha mpangilio tunaoweza kuufuata ili kuujua ukweli.
Tunamgeukia Nani kwa ajili ya Ukweli?
Mwishoni mwa Kitabu cha Mormoni, nabii Moroni anamwalika kila mmoja kumwomba Mungu kwa moyo wa dhati, na nia halisi na imani katika Kristo, “kama vitu hivi ni vya kweli.” Moroni anashuhudia kwamba Mungu “atafunua ukweli juu ya [Kitabu cha Mormoni] kwako kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Na kwa uwezo wa Roho Mtakatifu mtajua ukweli wa vitu vyote.” (Moroni 10:4–5).
Mungu Baba yetu wa Mbinguni ameanzisha njia halisi na inayopatikana ambayo watoto Wake wanaweza kumuomba (ona Yakobo 1:5) na kusonga karibu zaidi na Yeye kila siku, kila saa—hata katika nyakati zote . Njia hii rahisi na yenye nguvu ni sala.
Mafundisho ya Alma kwa mwanawe Helamani hutumika kikamilifu kwetu: “Mlilieni Mungu kwa ajili ya msaada wako wote.” Katika “matendo yako yote … na popote uendako … , acha mawazo yako yote yaelekezwe kwa Bwana; ndio, acha mapenzi ya moyo wako yawekwe kwa Bwana milele” (Alma 37:36). Alma pia alifundisha, “Shauriana na Bwana katika matendo yako yote, na atakuongoza wewe maisha yako yote” (Alma 37:37). Hatuhitaji wakati maalumu au mahali maalumu pa kusali. Ingawa haitawezekana daima kusali kwa sauti, tunaweza daima kuwa na sala katika mioyo yetu (ona Alma 34:27).
Majibu tunayopokea kutokana na sala zetu siyo kwamba yatakuwa kile tulichokitarajia. Nyakati zingine, yawezakuwa tofauti kabisa na mapenzi yetu. Sala zetu pia zaweza kuchukua muda mrefu zaidi kujibiwa. Wakati mwingine zikakutana na ukimya kwa muda. Lakini Baba wa Mbinguni anajali shida zetu. Majibu Yake daima yatakuwa kwa faida yetu. Tunahitaji tu kusonga mbele kwa imani katika Yesu Kristo. (Ona Luka 11:9–13.)1
Mwokozi wetu na Mkombozi ametamka kwamba hatutamfikia Baba wa Mbinguni isipokuwa tumepitia kwake Yeye. “Mimi ndimi njia, na kweli na uzima.” Yesu alisema. ‘”Mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi” (Yohana 14:6). Hii inafutilia mbali mbadala mwingine wowote ule au kikwazo chochote, katika mawasiliano yetu na Mungu. Hii ndiyo sababu sala zote, mazungumzo, shuhuda, madarasa na mambo mengine mengi tunayofanya—Kanisani, nyumbani pamoja na familia zetu, au wenyewe peke yetu—yanafanyika katika jina la Yesu Kristo.
Mtazamo Wetu Unapaswa Kuwa Upi?
Ili kupata ukweli, tunapaswa kuwa wadhati na kuwa na nia ya kweli. Kwa unyenyekevu tunapoliita jina la Baba wa Mbinguni , tunajitoa wenyewe kuwa tayari kutenda kulingana na majibu tunayopokea na tunaongeza uwezo wetu wa kufanya hivyo.
Udhati na nia halisi hutusukuma sisi kufanya vitu ambavyo Baba wa Mbinguni angetutaka tufanye, na sio kile tunachotaka sisi kifanyike. Kwa dhahiri kabisa tunamwonyesha Baba wa Mbinguni tumaini letu Kwake tunapokuwa tayari kuwa “watiifu, wapole, wanyenyekevu, wavumilivu, wenye upendo tele, walio tayari kukubali vitu vyote ambavyo Bwana anaona sahihi kuviweka juu yetu [sisi]” (Mosia 3:19). Kupitia mitazamo hii, tunakuja kuelewa na kutumaini kwamba Baba wa Mbinguni daima atafanya yaliyo bora kwa ajili yetu.
Je, Majibu Yatakujaje?
Katika kuamua kama tununue au tukodi nyumba, mke wangu na mimi tulisali, tulitafakari na kuzungumza sana kuhusu hilo. Mwishowe, hisia zilikuja katika akili zetu na mioyo yetu kwamba tusinunue nyumba. Tulifuata kwa imani kulingana na jibu tulilopokea, bila kujua kitu gani kinakaribia kutokea katika maisha yetu.
Takribani miezi 18 baadaye, mnamo Aprili 2022, niliitwa kama Kiongozi Mkuu wa Sabini. Baada ya mkutno mkuu wa Aprili 2022, tulikuwa na wiki tatu tu kuondoka Brazil kwa ajili ya kupangiwa kazi. Kuishi katika nyumba ya kukodi kwa wakati huo ilifanya mchakato wa kuhama kuwa rahisi. Leo, Regina na mimi tunaweza kwa uwazi kabisa kuona Bwana aliongoza uamuzi wetu.
Nefi pia alipokea kulingana na matamanio yake. Kwa bidii akiutafuta ukweli na kuamini na kutumaini kwamba Baba wa Mbinguni angemfunulia ukweli , Nefi alibarikiwa kuona vitu vile baba yake alivyoviona. Aliona mti wa uzima, ambao uliwakilisha upendo wa Mungu—upendo ambao “ni wa kupendeza zaidi ya vitu vyote” na “unafurahisha moyo kwa shangwe” (1Nefi 11:22,23).
Kupitia Roho Mtakatifu, Baba yetu wa Mbinguni anafunua ukweli ambao unapatikana kwa watoto Wake wote. Bwana alifunua kupitia Nabii Joseph Smith kwamba Roho Mtakatifu aweza kuongea mawazoni mwetu na mioyoni mwetu (ona Mafundisho na Maagano 8:2), “kujisukuma … kwenye hisia [zetu] (Mafundisho na Maagano 128:1), kusababisha vifua vyetu “viwake ndani yetu [sisi]” (Mafundisho na Maagano 9:8), kujaza nafsi zetu na shangwe, kuyaangaza mawazo yetu au kuzungumza amani katika mioyo yetu inayotatizika (ona Mafundisho na Maagano 11:13; 6:14–15, 22–23).
Ninashuhudia kwamba ukweli wa Mungu unafukuza mashaka na hofu na kuimarisha shuhuda zetu. Pamoja na Nefi, ninatamka, “Kwani atafutaye kwa bidii atapata” (1 Nefi 10:19). Mungu ataufunua ukweli kama kwa bidii tutautafuta, kwa kuwa Yeye “ni mwenye kuwazawadia wale wamtafutaye kwa bidiii” (Waebrania 11:6). Na atafanya hivi kwa uwazi kabisa kwamba hataacha mashaka yoyote kwamba mkono Wake unaongoza maisha yetu