Mlango wa 2
Yakobo anashutumu tamaa ya utajiri, kiburi, na uasherati—Wanadamu wamekubaliwa kutafuta utajiri kwa kusudi la kuwasaidia wanadamu wenzao—Bwana anaamuru kwamba hakuna mtu miongoni mwa Wanefi anayeruhusiwa kuwa na zaidi ya mke mmoja—Bwana anafurahia katika usafi wa kimwili wa wanawake. Karibia mwaka 544–421 K.K.
1 Maneno ambayo Yakobo, kaka wa Nefi, aliwazungumzia watu wa Nefi, baada ya kifo cha Nefi:
2 Sasa, ndugu zangu wapendwa, mimi, Yakobo, kulingana na jukumu langu kwa Mungu, kutukuza ofisi yangu kwa ufahamu, na ili niyaondolee mavazi yangu dhambi zenu, naja hapa hekaluni siku hii ili niwatangazie neno la Mungu.
3 Na ninyi mnajua mpaka sasa kwamba nimekuwa na bidii katika ofisi niliyoitiwa; lakini siku ya leo nimelemewa sana kwa hamu na wasiwasi wa ustawi wa nafsi zenu zaidi ya vile nilivyokuwa hapo awali.
4 Kwani tazama, hadi sasa, mmekuwa watiifu kwa neno la Bwana, ambalo nimewapatia.
5 Lakini tazama, nisikilizeni mimi, na mjue kwamba kwa usaidizi wa Muumba wa mbingu na dunia na aliye na uwezo wote naweza kuwaambia kuhusu mawazo yenu, jinsi vile mmeanza kutumikia katika dhambi, dhambi ambayo ni ya machukizo zaidi kwangu, ndiyo, na ya machukizo kwa Mungu.
6 Ndiyo, inahuzunisha nafsi yangu na kunisababisha nijitenge kwa aibu mbele ya uwepo wa Muumbaji wangu, kwamba lazima niwashuhudie kuhusu uovu wa mioyo yenu.
7 Na pia inanihuzunisha kwamba lazima nitumie maneno makali nikizungumza kuwahusu, mbele za wake zenu na watoto wenu, ambao wengi wao mawazo yao ni mepesi sana na yenye unyoofu na ya kuvutia mbele ya Mungu, kitu ambacho ni cha kupendeza kwa Mungu;
8 Na nimedhania kwamba wamekuja kusikia neno la kupendeza la Mungu, ndiyo, neno ambalo linaponya nafsi iliyojeruhiwa.
9 Kwa hivyo, inahuzunisha nafsi yangu kwamba ninashurutishwa, kwa sababu ya amri kali ambayo nimepokea kutoka kwa Mungu, kuwaonya kulingana na makosa yenu, kupanua vidonda vya wale ambao wamejeruhiwa, badala ya kuwafariji na kuponya vidonda vyao; na wale ambao hawajajeruhiwa, badala ya kujiburudisha kwa neno la kupendeza la Mungu wamewekewa visu vidunge nafsi zao na kujeruhi mawazo yao mepesi.
10 Lakini, ingawa kazi hii ni kuu, lazima nitende kulingana na amri kali za Mungu, na niwaambie kuhusu uovu wenu na machukizo yenu, katika uwepo wa walio safi moyoni, na moyo uliopondeka, na chini ya tazamo la jicho lenye kupenya la Mwenyezi Mungu.
11 Kwa hivyo, lazima niwaambie ukweli kulingana na udhahiri wa neno la Mungu. Kwani tazama, nilipokuwa nikimuomba Bwana, neno likanijia hivi, likisema: Yakobo, kesho uende hekaluni, na uwatangazie watu neno nitakalokupatia.
12 Na sasa tazameni, ndugu zangu, hili ndilo neno ambalo nawatangazia, kwamba wengi wenu mmeanza kutafuta dhahabu, na fedha, na kila aina ya mawe yenye madini, ambayo yamejaa tele, katika nchi hii, ambayo ni nchi ya ahadi kwenu na kwa uzao wenu.
13 Na mkono wa majaliwa umewapendelea sana, hata kwamba mmepata utajiri mwingi; na kwa sababu wengine wenu mmepata tele zaidi kuliko ndugu zenu mmejiinua juu kwa kiburi cha mioyo yenu, na kukaza shingo zenu na kuinua vichwa vyenu kwa sababu ya mavazi yenu yenye gharama, na kuwatesa ndugu zenu kwa sababu mnadhani kwamba ninyi ni bora kuliko wao.
14 Na sasa, ndugu zangu, je, mnadhani kwamba Mungu anawakubalia katika jambo hili? Tazama, nawaambia, Hapana. Lakini anawahukumu, na mkiendelea katika mambo hili lazima hukumu zake ziwateremkie kwa haraka.
15 Ee kwamba angewaonyesha kuwa anaweza kuwadunga, na kwa tazamo moja la jicho lake anaweza kuwaangusha mchangani!
16 Ee kwamba angewaondolea uovu huu na chukizo. Na, Ee kwamba mngesikiliza neno la amri zake, na msikubali hiki kiburi cha mioyo yenu kuangamiza nafsi zenu.
17 Fikirieni ndugu zenu jinsi mnavyojifikiria ninyi wenyewe, na mfanye urafiki na wote na muwe wakarimu katika utajiri wenu, ili nao wawe matajiri kama ninyi.
18 Lakini kabla ya kutafuta utajiri, tafuteni ufalme wa Mungu.
19 Na baada ya kupokea tumaini katika Kristo mtapokea utajiri, kama mtautafuta; na mtautafuta kwa kusudi la kutenda mema—kuvisha walio uchi, na kulisha wenye njaa, na kuwakomboa wafungwa, na kuwatolea msaada walio wagonjwa na wanaoteseka.
20 Na sasa, ndugu zangu, nimewazungumzia kuhusu kiburi; na wale wenu ambao mmetesa jirani yenu, na kumdhulumu kwa sababu mlikuwa na kiburi mioyoni mwenu, kwa sababu ya vitu vile ambavyo Mungu amewapatia, je, mnasema nini?
21 Je, hamdhani kwamba vitu kama hivi ni vya kuchukiza kwa yule aliyeumba watu wote? Na mwanadamu mmoja ni mwenye thamani machoni mwake kama mwingine. Na wanadamu wote wametoka mavumbini; na aliwaumba kwa kusudi moja, kwamba watii amri zake na kumtukuza milele.
22 Na sasa ninakoma kuwazungumzia kuhusu kiburi hiki. Na kama sio lazima kwamba niwazungumzie kuhusu makosa makuu zaidi, moyo wangu ungeweza kushangilia sana kwa sababu yenu.
23 Lakini neno la Mungu linanipatia mzigo kwa sababu ya dhambi zenu kuu: Kwani tazama, hivyo ndivyo asemavyo Bwana: Watu hawa wanaanza kutenda uovu; hawafahamu maandiko, kwani wanatafuta kisingizio cha kutenda uasherati, kwa sababu ya vile vitu vilivyoandikwa kuhusu Daudi, na Sulemani mwana wake.
24 Tazama, Daudi na Sulemani kwa hakika walikuwa na wake wengi na makahaba, kitu ambacho kilikuwa cha kuchukiza mbele yangu, asema Bwana.
25 Kwa hivyo, hivyo ndivyo asemavyo Bwana, nimewaongoza watu hawa kutoka nchi ya Yerusalemu, kwa uwezo wa mkono wangu, ili niinue tawi takatifu kutoka kwa matunda ya viuno vya Yusufu.
26 Kwa hivyo, mimi Bwana Mungu sitakubali kwamba watu hawa watende kama wale wa kale.
27 Kwa hivyo, ndugu zangu, nisikilizeni, na mtii neno la Bwana: Kwani hakuna mtu yeyote miongoni mwenu ambaye atakuwa na mke zaidi ya mmoja; wala hatakuwa na masuria;
28 Kwani mimi, Bwana Mungu, nafurahia usafi wa kimwili wa wanawake. Na ukahaba ni chukizo mbele yangu; hivyo ndivyo asemavyo Bwana wa Majeshi.
29 Kwa hivyo, watu hawa watatii amri zangu, asema Bwana wa Majeshi, la sivyo nchi italaaniwa kwa sababu yao.
30 Kwani kama, nitainua kizazi kwangu, asema Bwana wa Majeshi, nitawaamuru watu wangu; la sivyo, watatii vitu hivi.
31 Kwani tazama, mimi, Bwana, nimeona huzuni, na kusikia maombolezi ya mabinti za watu wangu katika nchi ya Yerusalemu, ndiyo, na katika nchi zote za watu wangu, kwa sababu ya uovu na machukizo ya mabwana wao.
32 Na sitakubali, asema Bwana wa Majeshi, kwamba vilio vya mabinti wazuri wa hawa watu, ambao niliwaongoza kutoka nchi ya Yerusalemu, kunifikia mimi kwa sababu ya wanaume wa watu wangu, asema Bwana wa Majeshi.
33 Kwani hawatawapeleka utumwani mabinti za watu wangu kwa sababu ya upole wao, la sivyo nitawaadhibu kwa laana kali, hata kuwaangamiza; kwani hawatatenda uasherati, kama wale wa kale, asema Bwana wa Majeshi.
34 Na sasa tazameni, ndugu zangu, mnajua kwamba amri hizi zilitolewa kwa baba yetu, Lehi; kwa hivyo, mlizijua hapo awali; na mmepokea hukumu kuu; kwani mmetenda vitu hivi ambavyo hamkustahili kutenda.
35 Tazama, mmetenda maovu makuu kuliko Walamani, ndugu zetu. Mmevunja mioyo ya wake zenu wapole, na kuvunja tumaini la watoto wenu, kwa sababu ya mifano miovu mbele yao; na vilio vya mioyo yao kwa sababu yenu vinamfikia Mungu. Na kwa sababu ya ukali wa neno la Mungu, unaoshuka dhidi yenu, mioyo mingi ilikufa, ikiwa imedungwa na vidonda vikubwa.