Maandiko Matakatifu
Moroni 9


Waraka wa pili wa Mormoni kwa mwanawe Moroni.

Yenye mlango wa 9.

Mlango wa 9

Wote Wanefi na Walamani wana tabia mbaya na wamedhoofika—Wanatesana na kuuana—Mormoni anaomba kwamba neema na uzuri uwe kwa Moroni milele. Karibia mwaka 401 B.K.

1 Mwana wangu mpendwa, ninakuandikia tena ili ujue kwamba mimi bado ni mzima; lakini ninaandika kidogo kwa yale ambayo ni mazito.

2 Kwani tazama, nimekuwa na vita vikali na Walamani, ambavyo hatukushinda; na Arkeanto ameuawa kwa upanga, na pia Luramu na Emroni; ndiyo, na tumepoteza idadi kubwa ya watu wetu wazuri.

3 Na sasa tazama, mwana wangu, ninaogopa kwamba Walamani watawaangamiza hawa watu; kwani hawatubu, na Shetani anawachochea siku zote kukasirikiana wao kwa wao.

4 Tazama, ninajaribu kuwafundisha siku zote; na ninaposema neno la Mungu kwa ukali wanatetemeka na kukasirika dhidi yangu; na nisipotumia ukali wanashupaza mioyo yao dhidi yake; kwa hivyo, ninaogopa isiwe Roho wa Bwana amekoma kujitahidi nao.

5 Kwani wamekuwa na hasira sana kwamba inaonekana kwangu kwamba hawaogopi kifo; na wamepoteza mapenzi yao, mmoja kwa mwingine; na wana kiu cha damu na kulipiza kisasi siku zote.

6 Na sasa, mwana wangu mpendwa, hata kwa ugumu wao, acha tuwafundishe kwa bidii; kwani tukikoma kufanya kazi, tungewekwa kwenye laana; kwani tuna kazi ya kufanya kama tungali kwenye hema hii ya udongo, kwamba tuweze kumshinda adui wa haki yote, na kupumzisha nafsi zetu katika ufalme wa Mungu.

7 Na sasa naandika kidogo kuhusu mateso ya hawa watu. Kwani kulingana na elimu ambayo nimepokea kutoka kwa Amoroni, tazama, Walamani wanao wafungwa wengi sana, ambao walikamatwa kutoka kwa mnara wa Sheriza; na kulikuwa na wanaume, wanawake, na watoto.

8 Na waume na baba za wale wanawake na watoto ambao wamewaua; na wanawalisha wanawake nyama za waume zao, na watoto nyama za baba zao; na hakuna maji, isipokuwa machache tu, wanayowapatia.

9 Na ijapokuwa haya machukizo makubwa ya Walamani, hayawezi kuzidi yale ya watu wetu walio Moriantumu. Kwani tazama, wengi wa mabinti za Walamani wamechukuliwa wafungwa na hao; na baada ya kuwanyangʼanya kile ambacho kilikuwa cha thamani sana kuliko vitu vyote, ambacho ni usafi wa kimwili na wema

10 Na baada ya hao kufanya kitu hiki, waliwauwa kwa njia ya kikatili sana, wakitesa miili yao hata hadi kifo; na baada ya kufanya haya, wanakula miili yao kama wanyama wa mwitu, kwa sababu ya ugumu wa mioyo yao; na wanaifanya kama ishara ya ushujaa.

11 Ee mwana wangu mpendwa, inawezekanaje watu kama hawa, ambao hawana ustaarabu—

12 (Na miaka michache tu imepita, tangu wawe wastaarabu na watu wazuri)

13 Lakini Ee mwana wangu, inawezekanaje watu kama hawa, ambao hupendezwa sana na machukizo mengi—

14 Tunawezaje kutumaini kwamba Mungu atajizuia kutoa hukumu yake dhidi yetu?

15 Tazama, moyo wangu unalia: Ole kwa watu hawa. Njoo nje na uwahukumu, Ee Mungu, na ufiche dhambi zao, na uovu, na machukizo kutoka mbele ya uso wako!

16 Na tena, mwana wangu, kuna wajane wengi na mabinti zao ambao wamebaki Sheriza; na sehemu ile ya vyakula ambayo Walamani hawakubeba, tazama, jeshi la Zenefi limebeba, na limewaacha wakizunguka kote ambako wangepata chakula; na wanawake wengi wazee wanazirai na kufia njiani.

17 Na jeshi ambalo liko na mimi ni dhaifu; na majeshi ya Walamani yako katikati ya Sheriza na mimi; na kwa vile wengi walikimbilia jeshi la Haruni wamekuwa madhabuha kwa ukorofi wao wa kutisha.

18 Ee upotovu wa watu wangu! Hawana msimamo na hawana huruma. Tazama, mimi ni mtu tu, na ninazo nguvu tu za mtu, na siwezi tena kulazimisha amri zangu.

19 Na wamejiimarisha kwa upotovu wao; na ni wakorofi sawasawa, bila kuachilia yeyote, si wazee wala vijana; na wanafurahia kila kitu isipokuwa kile ambacho ni kizuri; na kuumia kwa wanawake wetu na watoto wetu juu ya uso wote wa nchi hii kunazidi kila kitu; ndiyo, ulimi hauwezi kusema, wala haiwezekani kuandikwa.

20 Na sasa, mwana wangu, sitaendelea kueleza hii tamasha ya kuogofya. Tazama, unajua uovu wa hawa watu; unajua kwamba hawana msimamo, na wamekufa ganzi, na uovu wao unazidi ule wa Walamani.

21 Tazama, mwana wangu, siwezi kuwapendekeza kwa Mungu asije akaniua.

22 Lakini tazama, mwana wangu, ninakupendekeza kwa Mungu, na ninaamini katika Kristo kwamba utaokolewa; na ninamwomba Mungu kwamba atakuhurumia maisha yako, kushuhudia kurudi kwa watu wake kwake, au uharibifu wao halisi; kwani najua kwamba lazima waangamie isipokuwa watubu na wamrudie.

23 Na ikiwa wataangamia itakuwa kama ilivyotendeka kwa Wayaredi, kwa sababu ya ukaidi wa mioyo yao, wakitazamia kuua na kulipiza kisasi.

24 Na ikiwa kwamba wataangamia, tunajua kwamba wengi wa ndugu zetu wametoroka na kujiunga na Walamani, na wengi zaidi pia watatorokea kwao; kwa hivyo, uandike vitu vidogo zaidi, ikiwa utaachwa na nife bila kukuona; lakini ninaamini kwamba nitakuona hivi karibuni; kwani ninayo maandishi matakatifu ambayo nitakupatia.

25 Mwana wangu, uwe mwaminifu katika Kristo; na vitu ambavyo nimeandika visikusikitishe, na kukuwekea mzigo wa kukuua; lakini Kristo akuinue juu, na kuumia kwake na kifo chake, na kudhihirisha kwa mwili wake kwa babu zetu, na rehema yake na uvumilivu, na matumaini ya utukufu wake na uzima wa milele, yawe katika akili yako milele.

26 Na ninaomba neema ya Mungu Baba, ambaye kiti chake cha enzi kiko juu mbinguni, na Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye huketi kwenye mkono wake wa kulia wa uwezo wake, mpaka vitu vyote vitakapokuwa chini yake, iwe, na kiishi nawe milele. Amina.