Sehemu ya 52
Ufunuo uliotolewa kupitia Joseph Smith Nabii kwa wazee wa Kanisa, huko Kirtland, Ohio, 6Â Juni 1831. Mkutano ulikuwa umefanyika huko Kirtland, kuanzia tarehe 3 na kufungwa tarehe 6Â Juni. Katika mkutano huu ibada maalumu ya kutawazwa katika ofisi ya kuhani mkuu ilifanyika kwa mara ya kwanza, na kujitokeza mara kadhaa kwa roho wa uwongo na wadanganyifu kulitambuliwa na kukemewa.
1–2, Mkutano uliofuata ulipangwa kufanyika huko Missouri; 3–8, Teuzi za wazee maalumu kusafiri kwa pamoja zinafanywa; 9–11, Wazee watafundisha yale ambayo mitume na manabii waliyoandika; 12–21, Wale walioangaziwa na Roho huzaa matunda ya sifa na hekima; 22–44, Wazee mbalimbali wanateuliwa kwenda kuhubiri injili wakati wakisafiri kwenda Missouri kwa ajili ya mkutano.
1 Tazama, hivyo ndivyo asemavyo Bwana kwa wazee ambao amewaita na kuwateua katika siku hizi za mwisho, kwa sauti ya Roho wake—
2 Akisema; Mimi, Bwana, nitafanya yajulikane kwenu yale nitakayo kwamba myafanye kutoka wakati huu hadi mkutano ujao, ambao utafanyika katika Missouri, juu ya nchi ambayo nitaiweka wakfu kwa watu wangu, ambao ni baki la Yakobo, na wale ambao ni warithi kulingana na agano.
3 Kwa hiyo, amini ninawaambia, na watumishi wangu Joseph Smith, Mdogo, na Sidney Rigdon wafanye safari yao haraka kadiri maandalizi yanavyoweza kufanyika ya kuziacha nyumba zao, na kusafiri kwenda nchi ya Missouri.
4 Na kadiri watakavyokuwa waaminifu kwangu, itafanywa ijulikane kwao nini cha kufanya;
5 Na pia, kadiri watakavyokuwa waaminifu, itafanywa ijulikane kwao nchi ya urithi wenu.
6 Na kadiri watakavyokuwa siyo waaminifu, watakatiliwa mbali, hata kama vile nitakavyotaka, kama nitakavyoona kuwa ni vyema.
7 Na tena, amini ninawaambia, na mtumishi wangu Lyman Wight na mtumishi wangu John Corrill wafanye safari yao upesi;
8 Na pia mtumishi wangu John Murdock, na mtumishi wangu Hyrum Smith, wafunge safari yao kwenda sehemu hiyo hiyo kwa njia ya Detroit.
9 Na wasafiri kuanzia hapa wakilihubiri neno njiani, wakisema si kitu kingine isipokuwa yale ambayo manabii na mitume wameyaandika, na yale watakayofundishwa na Mfariji kwa njia ya kusali kwa imani.
10 Na waende wawili wawili, na hivyo ndivyo wafundishe njiani katika kila kusanyiko, wakibatiza kwa maji, na kuwawekea mikono kando kando ya maji.
11 Kwani hivyo ndivyo asemavyo Bwana, nitaimaliza na kuifupisha kazi yangu katika haki, kwani siku zaja ambazo nitaileta hukumu kwa ushindi.
12 Na mtumishi wangu Lyman Wight ajihadhari, kwani Shetani anataka kumpepeta kama makapi.
13 Na tazama, yule aliye mwaminifu atafanywa kuwa mtawala juu ya vitu vingi.
14 Na tena, nitatoa kwenu utaratibu katika mambo yote, ili msidanganyike; kwani Shetani amezagaa katika nchi, na anaenda akiwadanganya mataifa—
15 Kwa hiyo yule aombaye, akiwa roho yake imepondeka, huyo hukubaliwa nami kama anatii ibada zangu.
16 Yule asemaye, akiwa roho yake imepondeka, na ambaye lugha yake ni ya unyenyekevu na yenye kujenga, huyo ni wa Mungu kama anatii maagizo yangu.
17 Na tena, yule atetemekaye chini ya uwezo wangu atafanywa kuwa imara, naye atazaa matunda ya sifa na hekima, sawa sawa na kweli na mafunuo ambayo nimewapa ninyi.
18 Na tena, yule aliyeshinda na asizae matunda, hata sawa sawa na utaratibu huu, siyo wangu.
19 Kwa hiyo, kwa utaratibu huu mtazijua roho katika hali zote chini ya mbingu.
20 Na siku zimefika itakapofanyika kwa wanadamu sawa sawa na imani yao.
21 Tazama, amri hii imetolewa kwa wazee wote ambao nimewateua.
22 Na tena, amini ninawaambia, mtumishi wangu Thomas B. Marsh na mtumishi wangu Ezra Thayre wafanye safari yao pia, wakilihubiri neno njiani katika nchi hii hii.
23 Na tena, mtumishi wangu Isaac Morley na mtumishi wangu Ezra Booth wafunge safari yao, pia wakilihubiri neno njiani katika nchi hii hii.
24 Na tena, watumishi wangu Edward Partridge na Martin Harris wafunge safari yao pamoja na watumishi wangu Sidney Rigdon na Joseph Smith, Mdogo.
25 Na watumishi wangu David Whitmer na Harvey Whitlock pia wafunge safari yao, na wahubiri njiani, pia katika nchi hii hii.
26 Na watumishi wangu Parley P. Pratt na Orson Pratt wafunge safari yao, na wahubiri njiani, pia katika nchi hii hii.
27 Na watumishi wangu Solomon Hancock na Simeon Carter pia wafunge safari yao katika nchi hii hii, na wahubiri njiani.
28 Na watumishi wangu Edson Fuller na Jacob Scott pia wafunge safari yao.
29 Na watumishi wangu Levi W. Hancock na Zebedee Coltrin pia wafunge safari yao.
30 Na watumishi wangu Reynolds Cahoon na Samuel H. Smith pia wafunge safari yao.
31 Na watumishi wangu Wheeler Baldwin na William Carter pia wafunge safari yao.
32 Na watumishi wangu Newel Knight na Selah J. Griffin wote wawili watawazwe, na pia wafunge safari yao.
33 Ndiyo, amini ninaambia, na hawa wote wafunge safari zao kwenda sehemu moja, katika njia zao tofauti, na pasiwepo mtu mmoja kujenga juu ya msingi wa mwingine, wala katika njia ya mwingine.
34 Yule aliye mwaminifu, ndiye atakayetunzwa na kubarikiwa kwa matunda mengi.
35 Na tena, ninawaambia, acha watumishi wangu Joseph Wakefield na Solomon Humphrey wafunge safari yao katika nchi za mashariki;
36 Na wafanye kazi pamoja na familia zao, wasitangaze lolote ila yale ya manabii na mitume, kile ambacho wamekiona na kusikia na kwa hakika zaidi wanachoamini, ili kwamba unabii uweze kutimia.
37 Katika matokeo ya kuvunja sheria, na kile kilichowekwa juu ya Herman Basset kiondolewe kutoka kwake, na kuwekwa juu ya kichwa cha Simonds Ryder.
38 Na tena, amini ninawaambia, Jared Carter atawazwe kuwa kuhani, na pia George James atawazwe kuwa kuhani.
39 Na wazee walio salia wachunge makanisa, na kulitangaza neno katika maeneo yanayo wazunguka; na wafanye kazi kwa mikono yao wenyewe kwamba pasiwepo kufanyika kwa ibada za sanamu wala maovu kutendwa.
40 Na wakumbukeni katika mambo yote maskini na wenye shida, wagonjwa na walioteseka, kwani yule asiyefanya mambo haya, huyu siyo mwanafunzi wangu.
41 Na tena, watumishi wangu Joseph Smith, Mdogo, na Sidney Rigdon na Edward Partridge wachukue hati ya uthibitisho pamoja nao kutoka katika kanisa. Na ipatikane moja pia kwa ajili ya mtumishi wangu Oliver Cowdery.
42 Na hivyo ndivyo, hata kama nilivyosema, kama mtakuwa waaminifu mtajikusanya pamoja ninyi wenyewe kufurahi juu ya nchi ya Missouri, ambayo ndiyo nchi ya urithi wenu, ambayo sasa ni nchi ya adui zenu.
43 Lakini, tazama, Mimi, Bwana, nitauhimiza mji katika wakati wake, na nitawavika taji waaminifu kwa shangwe na furaha.
44 Tazama, Mimi ni Yesu Kristo, Mwana wa Mungu, nami nitawainua siku ya mwisho. Hivyo ndivyo. Amina.