Kitabu cha Ibrahimu
Kimetafsiriwa kutoka Kwenye Mafunjo na Joseph Smith
Tafsiri ya baadhi ya Kumbukumbu za maandiko ya kale ambazo zimeangukia mikononi mwetu kutoka kwenye katakombi za Misri. Maandishi ya Ibrahimu wakati akiwa Misri, yanayoitwa Kitabu cha Ibrahimu, kilichoandikwa kwa mkono wake mwenyewe, juu ya mafunjo.
Mlango wa 1
Ibrahimu ataka baraka za mpango wa kipatriaki—Anateswa na makuhani wa uongo katika Ukaldayo—Yehova anamwokoa—Asili ya Misri na utawala wake vinapitiwa upya.
1 Katika nchi ya Ukaldayo, katika makazi ya baba zangu, mimi, Ibrahimu, nikaona kwamba ilikuwa muhimu kwangu kupata mahali pengine kwa makazi;
2 Na, nilipoona huko kulikuwa na furaha na amani kubwa na mapumziko kwa ajili yangu, nilizitafuta baraka za baba, na haki ambayo kwayo ningetawazwa ili kuhudumu katika hiyo; mimi mwenyewe nikiwa mfuasi wa haki, nikitamani pia kuwa mtu mmoja mwenye ujuzi mkubwa, na kuwa mfuasi mkubwa wa haki, na mtu mwenye kumiliki ujuzi mkubwa, na kuwa baba wa mataifa mengi, mtawala wa amani, na nikitamani kupokea maelekezo, na kushika amri za Mungu, nikawa mrithi mwenye haki, Kuhani Mkuu, nikishikilia haki zilizokuwa mali za mababu.
3 Ilitunukiwa juu yangu kutoka kwa baba; ikaja chini kutoka kwa mababu, kutoka mwanzo wa wakati, ndiyo, hata kutoka mwanzo, au kabla ya msingi wa dunia, hadi wakati huu uliopo, hata haki ya uzaliwa wa kwanza, au mtu wa kwanza, ambaye ni Adamu, au baba wa kwanza, kupitia akina baba hadi kwangu mimi.
4 Nilitafuta kutawazwa kwangu katika Ukuhani kulingana na utawazo wa Mungu kwa mababu juu ya uzao.
5 Baba zangu, wakiwa wamegeuka kutoka kwenye uadilifu wao, na mbali na amri takatifu ambazo Bwana Mungu wao aliwapa, wakiwaabudu miungu ya wapagani, walikataa kabisa kuisikiliza sauti yangu;
6 Kwa kuwa mioyo yao ilikuwa tayari kufanya uovu, na waligeuka kabisa kwa mungu wa Elkena, na mungu wa Libna, na mungu wa Mahmakra, na mungu wa Korashi, na mungu wa Farao, mfalme wa Misri;
7 Kwa hiyo mioyo yao iligeukia kwa kafara za wapagani kwa kuwatoa watoto wao kwa sanamu hizi zisizosema, na hawakusikiliza sauti yangu, bali walidhamiria kuutoa uhai wangu kwa mkono wa kuhani wa Elkena. Kuhani wa Elkena alikuwa pia kuhani wa Farao.
8 Sasa, kwa wakati huu ilikuwa ni desturi ya kuhani wa Farao, mfalme wa Misri, kutoa sadaka juu ya madhabahu iliyokuwa imejengwa katika nchi ya Ukaldayo, kwa ajili ya kuwatolea sadaka miungu hawa wakigeni, wanaume, wanawake, na watoto.
9 Na ikawa kwamba kuhani alitoa sadaka kwa mungu wa Farao, na pia kwa mungu wa Shagrili, hata kwa jinsi ya Wamisri. Sasa mungu wa Shagrili alikuwa jua.
10 Hata sadaka ya shukrani ya mtoto kuhani wa Farao aliitoa juu ya madhabahu ambayo ilikuwa imesimama kwenye mlima ulioitwa Mlima wa Potifa, juu ya kilele cha nyanda za Olishemu.
11 Sasa, kuhani huyu alikuwa ametoa juu ya madhabahu hii wanawali watatu kwa mara moja, ambao walikuwa mabinti wa Onita, mmoja wa wazao halisi moja kwa moja kutoka viuno vya Hamu. Wanawali hawa walitolewa sadaka kwa sababu ya uadilifu wao; wao hawakukubali kupiga magoti na kuwasujudia mungu wa miti au wa mawe, kwa sababu hiyo wakawauwa juu ya madhabahu hii, nayo ilifanyika kwa jinsi ya Wamisri.
12 Na ikawa kwamba makuhani wakanikamata kwa nguvu, ili wapate kuniua mimi pia, kama walivyowafanya wanawali wale juu ya madhabahu hii; na kwa sababu hiyo muweze kuwa na ufahamu wa madhabahu hii, nitawarejesha kwenye picha mwanzoni mwa kumbukumbu hii.
13 Ilikuwa imetengenezwa katika umbo la kitanda, kama vile vilivyokuwako miongoni mwa Wakaldayo, nayo ilikuwa imesimama mbele za miungu wa Elkena, Libna, Mamakra, Korashi na pia mungu kama yule wa Farao, mfalme wa Misri.
14 Ili upate kuwa na ufahamu wa miungu hawa, nimekupa picha zao katika michoro mwanzoni, kwa jinsi ya michoro iliyoitwa na Wakaldayo Raloni, ambayo huashiria picha inayowakilisha neno, au maandiko ya hieroglifu.
15 Na wakati walipokuwa wakiinua mikono yao juu yangu, ili wapate kunitoa sadaka na kuutoa uhai wangu, tazama, nikapaza sauti yangu kwa Bwana Mungu wangu, naye Bwana akanisikiliza na kunisikia, na akanijaza ono la Mwenyezi, na malaika wasimamao mbele ya uso wake wakasimama karibu yangu, na haraka wakazifungua kamba zangu;
16 Na sauti yake ilikuwa juu yangu: Ibrahimu, Ibrahimu, tazama, jina langu ni Yehova, nami nimekusikia, na nimeshuka kuja kukuokoa, na kukuondoa kutoka nyumba ya baba yako, na kutoka kwa ndugu zako wote, kwenda katika nchi ya ugenini ambayo wewe huifahamu;
17 Na hii ni kwa sababu wao wameigeuza mbali mioyo yao kutoka kwangu, wakimwabudu mungu wa Elkena, na mungu wa Libna, na mungu wa Mamakra, na mungu wa Korashi, na mungu wa Farao, mfalme wa Misri; kwa hiyo nimeshuka ili kuwajilia wao, na kumwangamiza yeye aliyeuinua mkono wake dhidi yako, Ibrahimu, mwanangu, kuutoa uhai wako.
18 Tazama, nitakuongoza kwa mkono wangu, nami nitakuchukua, ili kuliweka jina langu juu yako, hata Ukuhani wa baba yako, na uwezo wangu utakuwa juu yako.
19 Kama vile ilivyokuwa kwa Nuhu ndivyo itakavyokuwa kwako; lakini kupitia huduma yako jina langu litajulikana duniani milele, kwa kuwa Mimi ndimi Mungu wako.
20 Tazama, Mlima wa Potifa ulikuwa katika nchi ya Uru, ya Ukaldayo. Na Bwana akaivunja madhabahu ya Elkena, na ya miungu ya nchi, na akawaangamiza kabisa, na kumpiga yule kuhani hata akafa; na palikuwa na maombolezo makubwa katika Ukaldayo, na pia katika baraza la Farao; ambapo Farao maana yake ni mfalme kwa damu ya kifalme.
21 Sasa huyu mfalme wa Misri alikuwa ni kutoka uzao wa viuno vya Hamu, na alikuwa mshiriki wa damu ya Wakanaani kwa kuzaliwa.
22 Kutoka uzao huu wametoka Wamisri wote, na hivyo damu ya Wakanaani ililindwa katika nchi;
23 Nchi ya Misri ikiwa imegunduliwa kwa mara ya kwanza na mwanamke, aliyekuwa binti wa Hamu, na binti wa Egipto, jina ambalo katika Kikaldayo liinamaanisha Misri, ambalo linamaanisha kile ambacho kimekatazwa;
24 Wakati mwanamke huyu alipoigundua nchi hiyo ilikuwa chini ya maji, mwanamke ambaye baadaye aliwafanya wanawe wakae ndani yake; na hivyo, kutoka Hamu, ilichipuka jamii ile ambayo iliidumisha laana katika nchi.
25 Sasa serikali ya kwanza ya Misri ilianzishwa na Farao, mwana mkubwa wa Egipto, binti wa Hamu, na ilikuwa kwa jinsi ya serikali ya Hamu, ambaye alikuwa patriaki.
26 Farao, akiwa mtu mwenye haki, akaanzisha ufalme wake na kuwahukumu watu wake kwa hekima na haki siku zote za maisha yake, akitamani kwa dhati kuiga mfano ule ulioanzishwa na mababu katika kizazi cha kwanza, katika siku za utawala wa patriaki wa kwanza, hata katika utawala wa Adamu, na pia Nuhu, baba yake, ambaye alimbariki kwa baraka za dunia, na kwa baraka za hekima, lakini akamlaani yeye kuhusiana na Ukuhani.
27 Sasa, Farao akiwa wa nasaba ambayo kwayo hakuweza kupata haki ya Ukuhani, licha ya kuwa Mafarao walisingizia kuwa nao kutoka kwa Nuhu, kupitia kwa Hamu, kwa ajili hiyo baba yangu alidanganyika kwa ibada zao za sanamu;
28 Lakini nitajaribu, hapo baadaye, kuonyesha kwa kuchora utaratibu wa kupanga miaka na matukio ukirudi nyuma kutoka mimi mwenyewe hadi mwanzo wa uumbaji, kwa kuwa kumbukumbu zimekuja mikononi mwangu, ambazo nimezishika hadi wakati huu.
29 Sasa, baada ya kuhani wa Elkena kuwa amepigwa naye akafa, ukaja utimilifu wa mambo yale ambayo yalikuwa yamesemwa kwangu juu ya nchi ya Ukaldayo, kwamba patakuwa na njaa katika nchi.
30 Hivyo njaa ikaenea sawia katika nchi yote ya Ukaldayo, na baba yangu akateseka vikali kwa sababu ya njaa, naye akatubu uovu ambao aliudhamiria dhidi yangu, wa kuutoa uhai wangu.
31 Lakini kumbukumbu za mababu, hata mapatriaki, juu ya haki ya Ukuhani, Bwana Mungu wangu alizihifadhi mikononi mwangu mimi mwenyewe; kwa hiyo ufahamu wa mwanzo wa uumbaji, na pia wa sayari, na wa nyota, kama zilivyojulikana kwa mababu, nimezitunza hadi siku hii, nami nitajaribu kuandika baadhi ya mambo haya juu ya kumbukumbu hii, kwa manufaa ya wazao wangu watakaokuja baada yangu.