2022
Marafiki wa Kambi
Septemba/Oktoba 2022


Marafiki wa Kambi

Hapo awali, Edison alihisi kama yeye hafai.

Picha
boys sitting around campfire at night

Edison alikwatua ardhi. Wavulana wengine wote walikuwa wakizungumza na kuweka hema. Lakini hakumjua mtu yeyote.

Familia ya Edison ilikuwa imeacha kwenda kanisani muda mfupi baada ya wao kuhamia Uhispania. Lakini wavulana kutoka katika kata walikuja na kumwalika aje kwenye safari ya kupiga kambi. Kambi ilionekana kuwa ya kufurahisha, lakini sasa Edison hakuwa na uhakika kwamba alitaka kuwa hapa. Alijiona kama hafai.

Wavulana wawili, Diego na Juan, walimwendea Edison. “Unataka kushiriki hema yetu?” Diego aliuliza.

Edison akashusha pumzi na kutabasamu. “Hakika.”

“Safi sana!” alisema Juan. “Na kisha tunaweza kwenda kuogelea.”

Wavulana walitengeneza hema zao na kukimbilia mtoni. Maji yalikuwa ya baridi, lakini sasa Edison alikuwa akifurahia sana hata hakugundua. Baada ya chakula cha mchana, wavulana na viongozi walikwenda kwenye kupanda mlima. Walirudi jua lilipoanza kutua, wakasaidia kuwasha moto wa kambi.

“Familia yako ikoje?” Juan aliuliza.

Edison alidondosha rundo la matawi karibu na moto. “Wazazi wangu ni wazuri sana. Na dada yangu ni rafiki yangu mkubwa. Tulihamia hapa kutoka Ecuador.”

Diego na Juan walitazamana kwa tabasamu kubwa.

“Sisi pia tunatoka Ecuador!” Juan alisema.

Diego alifungua zipu ya koti lake kuonyesha fulana yake. Ilikuwa na alama ya timu ya soka ya Ecuador juu yake!

“Lo!” Edison alisema. “Kwa hivyo unatamani nini zaidi kuhusu Ecuador?”

Diego na Juan walicheka. “Chakula!” wote wawili walipiga kelele.

Wavulana hao waliendelea kuzungumza juu ya mambo waliyotamani kuhusu Ecuador na yale waliyopenda kuhusu kuishi Uhispania. Edison alipenda jinsi ilivyokuwa rahisi kuzungumza na Diego na Juan.

Kisha mmoja wa viongozi, Kaka Cisneros, akasimama. “Habari zenu! Tunataka kutamatisha usiku huu na mkutano wa ushuhuda.”

Mmoja baada ya mwingine, wavulana na viongozi walisimama na kushiriki shuhuda zao. Maneno yao yaliufanya moyo wa Edison uhisi kama umefungwa kwenye blanketi la joto.

Diego alisimama. “Mimi najua Kanisa ni la kweli. Ninajua kwamba Mungu ni Baba yangu na kwamba Yesu Kristo ni Mwokozi wangu.”

Hisia nzuri zilikuwa zaidi. Nataka kujua hilo pia, Edison alifikiria.

Edison alipofika nyumbani kutoka safarini, maneno ya Diego yalibaki akilini mwake. Alitamani aende kanisani na kujifunza kuhusu Yesu pamoja na Diego na Juan.

Usiku huo wakati wa chakula cha jioni, Baba aliuliza, “Safari ya kupiga kambi ilikuwaje?”

“Ilikuwa nzuri sana!” Edison alisema. “Tuliogelea na kupanda mlima na tukawasha moto. Pia nilipata marafiki wawili kutoka Ecuador!”

“Hiyo ni vizuri sana! Itabidi tuwaalike,” Mama alisema.

Edison alitulia kidogo. “Tunaweza kuanza tena kwenda kanisani?”

Mama na Baba hawakusema lolote kwa muda fulani. Kisha Mama akaguna. “Ikiwa unataka kwenda, ni sawa,” alisema. “Lakini mimi na Baba hatuendi.”

Edison alijilaza kwenye kiti chake. Hakutaka kwenda kanisani peke yake. Labda abaki nyumbani na familia yake.

Kisha Edison akakumbuka hisia changamfu kutoka kwenye mkutano wa ushuhuda. Hata kama familia yake haikutaka kwenda kanisani, Edison alitaka kwenda.

Isitoshe, hangekuwa peke yake. Edison alitabasamu huku akila chakula chake cha jioni. Kisha akapokea simu. Alijua baadhi ya marafiki ambao angeweza kwenda nao kanisani!

Vielelezo na Hollie Hibbert

Chapisha