Waasisi katika Kila Nchi
Margaret Anaokoa Siku
Meli ilikuwa inazama! Margaret angeweza kufanya nini?
Margaret alisimama juu ya sitaha na kuangalia nje katika bahari ya bluu iliyokuwa ikimzunguka. Meli ilipigwa juu na chini juu ya mawimbi makubwa.
Familia ya Margaret ilikuwa imeuza karibu kila kitu walichokuwa nacho ili kusafiri kwa meli hadi Marekani. Safari hiyo ingechukua wiki sita. Margaret alihuzunika kuondoka nyumbani kwao huko Wales. Lakini alifurahia nyumba yake mpya pia.
Miezi michache kabla, familia ya Margaret ilikuwa imekutana na wamisionari kutoka Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Margaret na wazazi wake walibatizwa. Na sasa walikuwa wanaenda kujiunga na Watakatifu wengine katika Sayuni.
Safari ilikuwa ngumu hadi sasa. Mama wa Margaret alikuwa mgonjwa. Na baba yake alikuwa mgonjwa kutokana na miaka ya kufanya kazi katika migodi ya makaa ya mawe. Kwa hiyo Margaret aliangalia afya zao. Alimtunza kaka yake mdogo na dada yake mchanga pia. Ilikuwa kazi kubwa. Lakini Margaret hakulalamika.
Nyakati fulani mashua ilitikisika sana juu ya maji kiasi kwamba Margaret alianza kuumwa tumbo. Nyakati zingine aliogopa. Alipoogopa, alifumba macho yake na kumwomba Baba wa Mbinguni kwa ajili ya msaada.
Siku moja Margaret alisikia kelele. “Meli inavuja! Tunazama!”
Kila mtu aliingiwa na hofu. Nahodha alimwambia kila mmoja atafute ndoo. Watu walichota ndoo za maji ili kumwaga nje ya meli.
Margaret alitaka kusaidia. Alipiga magoti kando ya kitanda chake na kusali kwa bidii kadiri alivyoweza. “Tafadhali Baba wa Mbinguni, nisaidie kufikiria njia fulani ya kusaidia.”
Hisia ya amani ilijaza moyo wa Margaret. Alijua Baba wa Mbinguni alikuwa akimwangalia. Angewasaidia.
Kisha akapata wazo.
Alivuta mablanketi mawili ya sufu nyeupe kutoka kwenye kitanda chake na kukimbia kumtafuta nahodha. “Hapa,” alisema. “Weka hizi kwenye shimo ili kuzuia uvujaji.”
Nahodha alipenda wazo la Margaret. Akajaza blanketi kwenye shimo. Kisha akamimina ndoo kubwa ya lami ya moto juu ya mablanketi hayo. Lami ilipopoa, uvujaji ulikoma!
“Asante kwa kutoa blanketi zako,” nahodha alisema. “Mawazo yako ya haraka yameokoa siku.”
Margaret alitabasamu. Alijua Baba wa Mbinguni alikuwa amejibu maombi yake. Safari yake ya uasisi ilikuwa ndiyo kwanza inaanza, na alijua Mungu angemsaidia kila hatua aliyopitia.