2022
Hekalu na Safari Yako ya Milele
Julai 2022


“Hekalu na Safari Yako ya Milele,” Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana, Julai 2022.

Hekalu na Safari yako ya Milele

Jinsi gani tumebarikiwa kuongozwa katika nyumba ya Bwana.

Picha
vijana mbele ya hekalu

Picha na Noel Maglaque

Wewe upo safarini. Ilianza zamani sana ulipoishi na Baba wa Mbinguni kama mwana au binti Yake wa kiroho. Sasa uko hapa duniani na roho yako ikiwekwa katika mwili wa kimwili ili kujifunza yote ambayo yanahitajika ili siku moja kurudi kwa Baba wa Mbinguni na kustahili baraka zote alizonazo kwa watoto Wake. Baadhi ya mambo makuu utakayojifunza katika safari hii ya milele ni katika mahekalu ya Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.

Mahekalu kote Ulimwenguni

Nilipozaliwa mwaka wa 1928, kulikuwa na mahekalu saba tu. Sasa tuna mahekalu mazuri yaliyosambaa kote ulimwenguni. Na kutakuwa mengine zaidi! Mahekalu huleta furaha na nguvu tunazohitaji kwa safari yetu ya milele.

Hakuna majengo mengine duniani—hata yale yenye fahari zaidi—yana kile ambacho mahekalu yanayo. Mwokozi alimwambia Petro kwamba atapewa uwezo na mamlaka ili kwamba “lolote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni”(Mathayo 16:19). Hiyo ni kauli kubwa! Mahekalu yamewekwa wakfu na kutengwa kwa uwezo wa ukuhani kama mahali pa kufanyia ibada takatifu. Maagizo haya yanafaa kwa pande zote mbili za pazia.

Furaha ya Familia za Milele

Mke wangu, Barbara, alikufa karibu miaka minne iliyopita. Lakini kwa sababu tuliingia katika nyumba ya Bwana na kuunganishwa kama mume na mke kwa uwezo wa ukuhani, tumeunganishwa pamoja na watoto wetu saba, wajukuu 43, na zaidi ya vitukuu 100, kwa milele yote. Hekalu ni jambo zuri kiasi gani! Furaha inaujaza moyo wangu kwa sababu familia yangu itakuwa pamoja milele. Na familia yako inaweza kuwa pia.

Ukifikia umri wangu, hutavutiwa sana kuwa na pesa nyingi au kuendesha gari la kifahari. Kitu cha thamani zaidi maishani mwako kitakuwa familia yako—sio tu familia uliyonayo hapa bali pia familia yako katika umilele.

Nguvu ya Ukweli Uliorejeshwa

Unajua wewe ni nani—mwana au binti wa Mungu mwenye uwezo usio na kikomo. Unajua ulikotoka, kwa nini uko hapa, na nini kitatokea katika ulimwengu ujao.

Ninastaajabishwa kwamba kweli hizi zilikuja kama tokeo la ajabu la mvulana mdogo ambaye alipiga magoti na kusali kwenye kichaka cha miti. Baba na Mwana walimtokea Joseph Smith na, hatua kwa hatua, baraka za injili zilirejeshwa.

Nina hisia kali ya shukrani kwa Joseph Smith. Uelewa wetu uliorejeshwa wa mpango wa Mungu, jukumu kuu la Upatanisho wa Yesu Kristo, na umuhimu wa milele wa familia na mahekalu yote yalianza na yeye. Tutaendelea kujenga mahekalu na kutangaza mapya kwani ujumbe mkuu, unaoendelea wa Urejesho unaifunika dunia.

Kweli zilizorejeshwa, hususani kweli tunazojifunza kupitia ibada za hekalu, huweka maisha katika mtazamo na kutupa uwezo wa kutusaidia katika safari yetu ya milele.

Fanya Hekalu Sehemu Ya Maisha Yako

Huenda ikawa vigumu kwako kufikiri kwamba jambo unaloweza kufanya leo litafanya tofauti kubwa miaka kadhaa kutoka sasa au hata baada ya maisha haya. Lakini kumbuka safari ya milele uliyopo. Wakati unapobatizwa na kuthibitishwa, unachukua hatua muhimu katika safari hii.

Unaweza kuwasaidia wale ambao wamekufa kusonga mbele katika safari yao kwa kuwafanyia ubatizo na uthibitisho katika hekalu. Nilifanya hivi mara nyingi nilipokuwa rika lako. Nakumbuka wakati fulani nilibatizwa kwa zaidi ya watu 60. Sikuweza kupata pumzi kati ya ubatizo!

Ikiwa una nafasi ya kwenda hekaluni, fanya hivyo! Nenda mara nyingi uwezavyo. Tafadhali usijisumbue sana katika mambo ambayo yanaweza kuchukua muda wako mwingi na kukuvuruga kutoka kwa kile kilicho halisi na cha milele. Hata kama unaishi mbali na hekalu, zingatia na ujitayarishe sasa kustahili kuingia hekaluni.

Jiandae Sasa kwa ajili ya Baraka Zako za Hekaluni

Mojawapo ya ibada za kwanza za hekalu unazopokea kwa ajili yako mwenyewe ni endaumenti. Hii ni zawadi ya nguvu za ukuhani ipatikanyo kwa watoto wote wa Mungu. Tunapata uwezo huu kwa kupokea ibada na kutii maagano tunayofanya hekaluni kila siku ya maisha yetu.

Unaweza kujiandaa kwa endaumenti yako na ibada nyingine ya hekalu kwa kutafakari, kuomba, na kujifunza kuhusu hekalu. Ikiwa wazazi wako au babu na bibi zako wamewahi kufika hekaluni, zungumza nao kuhusu baraka tukufu. Askofu wako na viongozi wengine watakusaidia pia. Pia natumai utapata marafiki wazuri wanaokuunga mkono. Utakuwa na shukrani siku itakapofika kwako kuhudhuria hekalu na uko tayari kupokea ahadi zote za ajabu na baraka ambazo Bwana anatamani kukupa.

Picha
Yesu Kristo akiwafundisha wafuasi Wake

Kristo Akiwafundisha Wafuasi Wake, na Justin Kunz

Safari Inaendelea

Kusudi la maisha haya ni kujiandaa kwa yajayo. Mpango mkuu wa Baba wa Mbinguni haujaisha wakati wa kifo, kwa sababu roho yako haifi kamwe. Inakwenda kwenye ulimwengu wa roho ili kuendelea kujifunza, kutumikia, na kungoja Ufufuo. Kisha, kila goti litapigwa na kila ulimi utakiri kwamba Yesu ndiye Kristo (ona Isaya 45:23). Kwa sababu ya Upatanisho Wake na Ufufuo, miili na roho zetu zitaunganishwa tena, na safari yetu itaendelea hadi umilele. Hiyo itakuwa baraka tukufu kiasi gani kwetu sote!

Yote yanaposemwa na kufanywa, kila kitu chenye matokeo na umuhimu wa milele hulenga maisha na misheni ya Yesu Kristo. Maarifa na imani yako Kwake itakua unapohudumu katika hekalu. Utahisi upendo Wake usio na kikomo kwako na kupata furaha na nguvu za kiroho katika maisha yako yote.

Chapisha