“Kujiandaa kwa ajili ya Maagano ya Hekalu,” Kwa ajili ya Nguvu kwa Vijana, Julai 2022.
Dhima na Mimi
Vijana wakielezea jinsi wanavyoishi maneno ya Dhima ya Wasichana na ya Akidi ya Ukuhani wa Haruni
Kujiandaa kwa ajili ya Maagano ya Hekalu
“Nita … fanya na kushika maagano matakatifu, na kupokea ibada na baraka za hekalu takatifu.”
Ninapenda kuhudhuria hekalu! Shukrani kwa hekalu, ninaweza kuwa na familia ya milele, kusaidia kukusanya Israeli, na kupokea maongozi ya kiroho na faraja.
Wakati familia yangu ilipohamia kwenye nyumba yetu mpya, nilishukuru kwamba ilikuwa karibu sana na hekalu. Nina mwonekano mzuri wa hekalu kupitia dirisha la chumba changu cha kulala. Kila siku ninapoona hekalu, ninakumbushwa kujiandaa kufanya maagano ya milele.
Ni muhimu sana kuwa tayari kwa maagano unayofanya hekaluni na kuwasaidia watu walio nje ya pazia kufanya maagano hayo pia. Nimekuwa nikisoma kuhusu hekalu na kujaribu kuwa tayari niwezavyo ili nifanye maagano zaidi. Ndugu yangu ndiyo kwanza amepokea endaumenti yake, na ilikuwa ni uzoefu maalum kwake. Kuona jinsi alivyofurahi kulinifanya nitambue kwamba nataka baraka hizo pia!
Lakini ingawa nina hekalu nje ya dirisha langu, sitaki kulichukulia kawaida. Kwa hivyo ninajaribu kuishi kwa njia ili niweze kustahili kuhudhuria hekaluni.
Wakati hekalu lilipofungwa wakati wa janga hilo, nilikuwa na imani kwamba halitafungwa kwa muda mrefu sana. Kisha hatimaye niliweza kurejea tena hekaluni kwa mara ya kwanza, na ilikuwa ni tukio maalum sana. Nilikuwa na wasiwasi kidogo kwa sababu sikuwa nimefika hapo kwa muda. Lakini mara nilipoingia ndani, nilihisi tu kama mimi ni wa pale. Niliweza kuhisi Roho.
Nina ushuhuda thabiti sana wa mahali patakatifu, na siwezi kusubiri kufanya maagano zaidi na Baba yangu wa Mbinguni.
Mwandishi anaishi Utah, Marekani.