“Acha Kulinganisha! Wewe Unatosha,” Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana, Jan. 2024.
Njoo, Unifuate
Acha Kulinganisha! Wewe Unatosha
Hapa kuna vitu vinne ambavyo tunajifunza kutoka kwa mmojawapo wa kaka zake Nefi.
Kuna mwanafunzi mmoja darasani ambaye daima hujua jibu la kweli. Mtoto kwenye timu ya mpira wa kikapu ambaye daima anakuzidi kiwango. Mtu ambaye kila mtu anataka kuwa rafiki yake. Katika ulimwengu wa kulinganisha, inaonekana kama daima kuna mtu mzuri.
Kulinganisha kunaweza kuwa kugumu hasa linapokuja suala la kuishi injili. Unaweza kudhani kuwa wengine ni wakamilifu zaidi, wana ushuhuda mkubwa, au kuhisi Roho vizuri kuliko wewe. Lakini kujilinganisha namna hii haisaidii.
Kutoka katika Kitabu cha Mormoni, huenda unajua kwamba Nefi alikuwa kiongozi mkubwa na nabii. Ila ni kwa kiasi gani unajua kuhusu kaka mkubwa mwaminifu wa Nefi, Sam? Hakuwa kiongozi mkubwa au nabii kama Nefi, ila hakuhitaji kuwa kama Nefi kuwa mzuri vya kutosha.
1. Sam Aliamini
Nefi alisali na kupata jibu kwa ajili yake kwamba Bwana aliamuru familia yao kuondoka kuelekea nyikani. Na Sam “aliamini katika maneno ya [Nefi]” (ona 1 Nefi 2:16–17). Sam huenda hakuwahi kuwa na ushuhuda mkamilifu. Huenda alikuwa na maswali. Ila alichagua kuamini katika maneno ya kaka yake, na kisha kutenda katika imani yake. Usijilinganishe imani au ushuhuda na watu wengine. Kadiri unavyotenda kwa imani kama Sam alivyofanya, ushuhuda wako kwa Mwokozi utakua kidogo kidogo. Ona pia Mafundisho na Maagano 46:13–14; Alma 32.)
2. Sam Alikuwa Mnyenyekevu
Lamani na Lemueli hawakuwa na furaha kwamba kaka yao mdogo, Nefi, alikuwa anakuwa kiongozi juu yao. Ila Sam, ambaye alikuwa kaka mkubwa wa Nefi pia, lazima alikuwa mnyenyekevu. Alimsikiliza Nefi na kufuata ushauri wake (ona 2 Nefi 5:3–6). Kama wengine walio nawe wataombwa kuongoza na wewe hukuombwa, kuwa mnyenyekevu, na usilinganishe. Waunge mkono, jifunze kutoka kwao, na ufanye uwezalo kuchagua jema.
3. Sam Alikuwa na Subira
Inaweza kuonekana kama vile kila mtu aliyekuzunguka anaishi maisha makamilifu, ila kila mtu hupitia nyakati ngumu. Sam hakuwa wa tofauti. Lamani na Lemueli walimgeuka Sam, kama walivyomgeuka Nefi. Hata walimpiga Sam na fimbo, kama walivyompiga Nefi! (Ona 1 Nefi 3:28; 1 Nefi 7:6.) Ila Sam kwa subira alivumilia majaribu yake. Kupitia hali ngumu si lazima kumaanishe kwamba unafanya jambo baya. Usilinganishe majaribu yako na ya wengine. Kuwa na subira, na uamini katika Bwana. Atakusaidia kuvuka.
4. Sam Alibarikiwa
Lehi, baba yake na Sam, alimwambia Sam, “ Nawe utabarikiwa katika siku zako zote” (2 Nefi 4:11). Sam huenda hakuwa kiongozi au nabii, ila bado kwa uaminifu alimfuata Yesu Kristo, na alibarikiwa kwa hilo. Kwa msaada wa Mwokozi, alikuwa mzuri vya kutosha. Nawe pia unaweza kuwa.