Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana
Kuwasaidia Wengine Kwa Urahisi na Kwa Nguvu Waje kwa Kristo
Julai 2024


“Kuwasaidia Wengine Kwa Urahisi na Kwa Nguvu Waje kwa Kristo,” Kwa Ajili ya Nguvu Kwa Vijana, Jul. 2024.

Kuwasaidia Wengine Waje kwa Kristo Kwa Urahisi na Kwa Nguvu

Una njia nyingi za kuonyesha upendo, kushiriki imani yako, na kuwaalika wengine kuja kwa Yesu Kristo.

Yesu Kristo

Siku moja katika mwaka wangu wa kwanza katika shule ya sekondari, rafiki yangu Nedra aliniuliza, “Russ, kwa nini huendi seminari?”

Wakati huo, wazazi wangu hawakuwa wakienda kanisani. Nilihudhuria mara chache na marafiki zangu, na sikushiriki katika seminari. Siku iliyofuata, nilihudhuria seminari saa 12:30 asubuhi. Baada ya hapo, nilienda kila siku—hata asubuhi yenye baridi na yenye theluji.

Mambo niliyojifunza katika seminari yaligusa moyo wangu. Ushuhuda wangu uliongezeka nilipojifunza zaidi kuhusu Yesu Kristo na injili Yake iliyorejeshwa. Hii ilinitayarisha kuhudumu misheni yangu huko Uingereza na kuendelea katika maisha yote ya huduma kwa Bwana na Kanisa Lake.

Nedra kunialika seminari kunanisaidia kuona, kwa njia binafsi, kwamba kuna fursa nyingi kwako za kuwasaidia wengine kuja kwa Bwana Yesu Kristo. Kwa njia rahisi lakini zenye nguvu, unaweza kuonyesha upendo wako, kushiriki imani yako, na kuwaalika wale walio karibu nawe kupata furaha na amani ambayo Mwokozi na injili Yake huleta.

Njoo Umjue Mwokozi

Ili kuwasaidia wengine waje kwa Kristo, kwanza unahitaji kuelewa Yeye ni nani. Yesu Kristo ndiye Mwana wa Mungu na ndiye pekee ambaye angeweza kuwa Mwokozi na Mkombozi wa ulimwengu.

Ni Yeye pekee ambaye angeweza kuishi maisha makamilifu, kulipia dhambi zako, kuteseka “maumivu yako yote na mateso na majaribu.” (Alma 7:11), na kisha kuutoa uhai Wake na kuutwaa tena. Kwa sababu ya Yesu Kristo, watoto wote wa Mungu watafufuka tena na wanaweza kupokea baraka Zake takatifu na tukufu.

Unapoelewa Mwokozi ni nani—na hatima yako ya milele inaweza kuwa nini kwa sababu Yake—utataka kuishi maisha yako kwa njia inayompendeza Yeye. Na hakika inampendeza unapotangaza injili Yake, kwa maneno na vitendo, kwa wale unaochangamana nao kila siku.

Fikia kwa Upendo

Unapokuja kumjua na kumpenda Mwokozi, utatamani kumfuata Yeye na mafundisho Yake kwa ukaribu zaidi, ikijumuisha amri Yake ya “kupendana.” (Yohana 13:34).

Wakati Amoni alipoenda kwa Walamani kuhubiri injili, alijitolea kuwa mtumishi wa Mfalme Lamoni. Amoni alionyesha upendo wa kweli na kujitolea alipolinda kondoo wa mfalme. Vitendo vya Amoni vililainisha moyo wa Mfalme Lamoni. Amoni alipofundisha injili, Roho alimshinda Mfalme Lamoni, na akaongoka (ona Alma 17–19).

Kuwa mwanafunzi wa kweli wa Yesu Kristo kunamaanisha kuwapenda jirani zako kama nafsi yako (ona Mathayo 22:36–40). Ikiwa wanaweza kuhisi kwamba unawapenda na kuwajali, kuna uwezekano watakuwa tayari wewe uwashirikishe mambo unayojua kuwa ya kweli.

Tafuta Ujasiri wa Kushiriki

Kupitia Nabii Joseph Smith, Mwokozi alirejesha ukuhani duniani pamoja na ibada na maagano yote muhimu kwa maendeleo yetu ya milele. Mara ujumbe mtukufu wa Urejesho unapogusa moyo wako, unapaswa kutaka kuupigia kelele kutoka juu ya paa! Unapaswa kujihusisha kwa shauku katika kushiriki maarifa ya thamani ya injili iliyorejeshwa na kila mtu. Ninapenda kufanya hivyo!

Wengine wanaweza kuwa na wasiwasi kwamba wengine hawatapendezwa au watakataa kile wanachoshiriki. Ndio, hilo linaweza kutokea. Baada ya Abish kukimbia kutoka nyumba hadi nyumba akiwaambia watu kwamba nguvu za Mungu zimemjia Mfalme Lamoni na nyumba yake, wengine waliamini, lakini wengine wengi walichagua kutosikiliza (ona Alma 19:17–31).

Iwe wanaikubali au la, zawadi kuu zaidi unayoweza kumpa rafiki au mwanafamilia—au hata adui—ni injili ya Yesu Kristo. Omba ujasiri, na kisha, inapofaa, shiriki kile unachojua kuwa kweli.

Toa Mwaliko wa Dhati

Nilipokuwa nikihudumu kama rais wa Misioni ya Kanada Toronto, nilisaidia wamisionari wangu kadhaa kumfundisha mfanyabiashara mashuhuri. Baada ya somo letu, nilimwalika kusali na kumuuliza Baba wa Mbinguni kama ujumbe wetu ni wa kweli.

“Sijui jinsi ya kusali,” alisema.

Nilimwambia kwamba alichohitaji kufanya ni kupiga magoti na kumwomba tu Baba wa Mbinguni kuthibitisha ukweli kwake.

“Unaweza kufanya hilo! Nilimtia moyo.

Tulipiga magoti pamoja na yule mtu akaanza sala yake. Alipomaliza akasema, “Ni nini kinatokea? Sijawahi kuhisi kitu kama hiki hapo awali.”

“Hivyo ndivyo Baba wa Mbinguni hujibu sala,” nilisema. “Umeuliza, naye amejibu.”

Mimi huwafundisha wamisionari na wauminii kote ulimwenguni kwamba uongofu huanza na kile watu wanachohisi. Unapowaalika wengine kuisikia injili, waalike pia kusali na kuomba ili wahisi ukweli katika mioyo yao. Kama watamuuliza Mungu (ona Yakobo [Biblia] 1:5) kwa moyo wa dhati, kwa nia ya kweli na imani katika Kristo, wanaweza kupokea uthibitisho wa ukweli kwa uwezo wa Roho Mtakatifu (ona Moroni 10:4–5). Inasisimua na inafurahisha kuwasaidia wengine wagundue ukweli wao wenyewe.

Kumbuka Kwamba Kila Nafsi ni ya Thamani

Hujui kitakachotokea unapowasaidia wengine kuja kwa Kristo kwa kupenda, kushiriki, na kualika. Walamani, kwa mfano, walionekana kuwa watu wasiowezekana kabisa kuikubali injili, lakini wakaongolewa mno kiasi kwamba “hawakuanguka kamwe.” (Alma 23:6–7).

Hupaswi kutarajia matokeo haya kila wakati unaposhiriki injili. Lakini kwa urahisi na kwa nguvu, unaweza kushuhudia ukweli na kusaidia kuwatambulisha watoto zaidi wa Baba wa Mbinguni kwenye injili ya urejesho.

Unapotambua jinsi kila mmoja wa watoto wa Baba wa Mbinguni alivyo wa thamani Kwake, utataka kufanya kila kitu unachoweza kuwasaidia wengine waje kwa Kristo na kuingia katika nuru ya injili Yake na kwenye njia ya maisha yasiyo na mwisho na uzima wa milele.

Je, ni uzoefu gani mkubwa zaidi unaweza kuwa nao maishani?